Tantrade yateuliwa kuwania tuzo za WTPO 2024

Dar es Salaam. Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) imeorodheshwa kuwania Tuzo za Shirika la Kukuza Biashara Duniani (WTPO) mwaka 2024 kati ya mashirika manane ya kitaifa ya kukuza biashara yaliyoteuliwa kuwania tuzo hiyo mwaka huu na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC).

Tuzo za WTPO 2024 zinaangazia utendaji kazi bora wa mashirika ya kutangaza biashara (TPO) kwa kuainisha mipango ya maendeleo ya uuzaji bidhaa nje. Mipango ya maendeleo ya mauzo ya nje yanalenga kujenga uwezo wa biashara zinazouza nje katika muda wa kati na mrefu.

Tantrade ni miongoni mwa mashirika matatu yaliyoteuliwa kushindania kipengele cha ‘Matumizi Bora ya Teknolojia ya Habari’ kwa mpango wake wa kuanzisha tovuti ya biashara Tanzania iliyozinduliwa Julai 8, 2021, ili kutoa mwongozo wa kina na wa wazi kwa wafanyabiashara wanaoshughulika na biashara ya nje, uagizaji na usafirishaji.

Toviti hiyo inalenga kurahisisha mchakato wa biashara kwa kupunguza muda unaopotea na gharama katika kupata vibali na leseni.

Mashirika mengine ya kukuza biashara yaliyoteuliwa katika kipengele hicho ni pamoja na Jamhuri ya Dominika na Uswizi.

Kwa kuteuliwa katika mojawapo ya vipengele vya Tuzo za WTPO, Tantrade inatambulika kwa uwezo wake wa kuimarisha ushindani wa kibiashara wa Tanzania duniani kote.

“Tunajivunia mafanikio haya hadi sasa na tunatarajia matokeo chanya,” limebainisha shirika hilo kupitia taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade, Yusuph Tugutu, leo Jumatatu Septemba 30, 2024.

Tovuti hiyo ya Tantrade imeweka kumbukumbu za bidhaa 70 na ina mpango wa kuzifikia zaidi ya bidhaa 200 ifikapo mwaka 2026. Mauzo muhimu yanajumuisha kahawa, parachichi, korosho, karafuu na ufuta. Tovuti hiyo ina watumiaji zaidi ya 400,000.

Mbali na kipengele cha “Matumizi Bora ya Teknolojia ya Habari”, vipengele vingine viwili ni “Matumizi Bora ya Ubia” na “Mpango Bora wa Kuhakikisha kwamba Biashara ni Jumuishi na Endelevu”, pia zinawaniwa na mashirika mengine duniani kote. Washindi kwa kila vipengele hivyo watatangazwa Oktoba 15, 2024 na ITC.

Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade, Latifa Mohamed Khamis taarifa yake amesema, “Tantrade imechukua hatua ya kuanzisha tovuti ya biashara ya Tanzania, jukumu lake ni kuweka mazingira ya biashara ya uwazi na ufanisi zaidi ambayo kwa upande wake inahimiza ushiriki mkubwa katika biashara ya kimataifa.”

Kama sehemu ya shughuli ya utoaji tuzo, Mkurugenzi huyo wa Tantrade, ataliwakilisha shirika hilo akiungana na wawakilishi wa mashirika ya biashara ya kitaifa zaidi ya 300 katika hafla ya kipekee itakayojadili changamoto wanazokabiliana nazo, kubadilishana uzoefu na kuanzisha uhusiano mpya.

Kaulimbiu ya Tuzo za WTPO 2024 ni “Ubora ni mipango ya maendeleo ya mauzo ya nje.”

Related Posts