Umuhimu wa vijana kushiriki uchaguzi serikali za mitaa

Dar es Salaam.  Uchaguzi wa serikali za mitaa ni tukio muhimu katika kuimarisha demokrasia na ushiriki wa wananchi katika utawala wa nchi yao.

Hata hivyo, kuna changamoto ya ushiriki mdogo wa vijana katika michakato ya uchaguzi huo, hali inayohitaji kuangaziwa ili kuliwezesha kundi hilo kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, mwaka 2020, vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 waliwakilisha zaidi ya asilimia 56 ya wapiga kura wote waliosajiliwa nchini.

Hii inaungwa mkono na utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) mwaka 2022, uliobainisha kuwa takriban asilimia 40 ya vijana wenye sifa za kupiga kura hawajishughulishi na masuala ya uchaguzi.

Hii inaonyesha vijana ni kundi kubwa lenye nguvu ya kisiasa, lakini ushiriki wake kwenye uchaguzi umekuwa wa kusuasua.

Tafiti mbalimbali zimeonyesha wengi wa vijana hawashiriki kikamilifu kwenye michakato hiyo kutokana na sababu za kukosa uelewa wa haki zao za msingi za kiraia, kuathiriwa na kukosa imani na mfumo wa kisiasa na kutokuwepo kwa programu za kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kupiga kura.

Hata hivyo, ushiriki wa vijana katika uchaguzi, una umuhimu wa kipekee kwa sababu ndiyo walengwa wakuu wa sera nyingi za kitaifa na kimataifa.

Kushiriki kwao kunawawezesha kuchagua viongozi wanaoelewa changamoto zao, kama ajira, elimu, afya na teknolojia.

Kutokana na umuhimu huo, viongozi wanaochaguliwa katika ngazi ya mitaa wanakuwa na jukumu la moja kwa moja katika kutekeleza sera hizo kwenye jamii za wananchi.

Hivyo, vijana wanaposhiriki, wanapata nafasi ya kuwawajibisha viongozi hao kadiri ya matakwa yao na hivyo kuleta athari chanya katika mchakato wa maamuzi yanayoathiri maisha yao.

Faida za ushiriki wa vijana

Vijana wanaposhiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, wanaweza kufikia matokeo chanya kwenye nyanja za uwakilishi bora.

Ushiriki wa vijana unahakikisha sauti zao zinasikika katika masuala yanayowahusu na kuwa na viongozi wanaowajibika kwa changamoto zinazowakabili.

Pia, vijana wakiwa sehemu ya mchakato wa kuchagua viongozi, wanapata fursa ya kujifunza na kuendeleza uwezo wao wa uongozi na hivyo kuongeza uwezekano wa kuingia kwenye nafasi za uongozi katika siku zijazo.

Kwa kuwa vijana wanaposhiriki katika michakato ya kisiasa, wanaposhiriki uchaguzi wanajenga uwezo wa kuelewa na kuhusika katika maamuzi yanayoathiri maendeleo ya jamii zao kisiasa, kiuchumi na kijamii, na hivyo kuchangia kujenga taifa imara na lenye demokrasia endelevu.

Pamoja na umuhimu wake, vijana wengi bado hawashiriki kwa kiwango cha kuridhisha kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao mwaka huu utafanyika Novemba 27.

Vijana wengi hawapati elimu ya kutosha juu ya haki zao za kiraia na umuhimu wa kushiriki uchaguzi.

Hii inachangia uelewa mdogo wa nafasi yao katika kujenga jamii bora kupitia mchakato wa kisiasa.

Baadhi ya vijana hawana imani na mfumo wa kisiasa, wakihisi kuwa viongozi wanajali masilahi yao binafsi zaidi ya yale ya wananchi, hivyo kukosa motisha ya kushiriki.

Changamoto za kiuchumi kama ukosefu wa ajira hupelekea vijana wengi kujihusisha zaidi na harakati za kujitafutia riziki kuliko kushiriki katika masuala ya kisiasa.

Ili kuongeza ushiriki wa vijana katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kutoa elimu ya kiraia ni jambo muhimu na la lazima kutiliwa mkazo.

Serikali na wadau wake kama mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi za elimu wanapaswa kushirikiana ili kutoa elimu ya kiraia kwa umama, hasa kwa vijana, kuanzia shule za sekondari hadi vyuo vikuu na hata wale ambao hawako shuleni.

Ni muhimu kwa viongozi na vyombo vya uchaguzi kuhakikisha michakato ya uchaguzi inakuwa ya haki, uwazi na inayowajibika, ili kuimarisha imani ya vijana kwa Serikali na mfumo wa kisiasa kwa ujumla.

Serikali na wadau wengine wa maendeleo wanapaswa kuwekeza katika miradi inayolenga kuimarisha uchumi wa vijana, ikiwa ni pamoja na kutoa fursa zaidi za ajira na mafunzo ya ujasiriamali ili kupunguza changamoto za kiuchumi zinazowakabili.

Kwa muktadha huo, vijana wakiwa ndiyo  nguvu ya Taifa, ushiriki wao katika uchaguzi wa serikali za mitaa unatakiwa usiwe wa kutiliwa shaka kwa kuwa ni  muhimu kwa stawi wa jamii na maendeleo kwa jumla.

Wakati takwimu zikionyesha kuwa zaidi ya nusu ya wapiga kura nchini ni vijana, ni muhimu kuweka mikakati madhubuti ya kuwahamasisha na kuwaelimisha ili washiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.

Hii siyo tu itawasaidia kujenga taifa lenye demokrasia ya kweli, bali pia kuwapa uwezo wa kubadili maisha yao kupitia uwakilishi wa viongozi wanaojali masilahi yao.

Hivyo basi, ushiriki wa vijana ni chachu ya mabadiliko na maendeleo endelevu kwa Tanzania.

Kwa kuwa changamoto kubwa inayowakabili vijana ni ukosefu wa ajira, ushiriki wao kwenye uchaguzi unawapa fursa ya kuchagua viongozi watakaolenga kuboresha hali ya ajira na kujenga mazingira mazuri ya ujasiriamali.

Utafiti wa Taasisi ya Uongozi wa Demokrasia Tanzania (TADIP), takriban asilimia 40 ya vijana hawakujitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019.

Miongoni mwa sababu zinazochangia hali hii ni pamoja na ukosefu wa elimu ya uraia, kutokuwa na imani na mfumo wa kisiasa, pamoja na changamoto za kiuchumi ambazo zinawafanya vijana wengi kupoteza matumaini na michakato ya uchaguzi.

Vijana wanapojitokeza kwa wingi na kupiga kura, wanaimarisha mfumo wa uwajibikaji wa viongozi. Viongozi wanakuwa na jukumu la kuzingatia matakwa ya vijana ili kupata ridhaa yao katika chaguzi zinazofuata.

Kwa hiyo, ushiriki wa vijana unaleta uangalizi na uwajibikaji kwa viongozi waliochaguliwa.

Ushiriki wa vijana katika uchaguzi wa serikali za mitaa pia unawawezesha kushiriki katika nafasi za uongozi.

Kura yao inaweza kusaidia kuchagua viongozi vijana wenzao ambao wana uelewa wa karibu wa changamoto zinazowakabili, hivyo kuleta mawazo mapya na mbinu za kisasa za kutatua matatizo.

Kura ya kijana ina nguvu kubwa ya kubadilisha mustakabali wa Taifa, hasa kwenye ngazi ya serikali za mitaa.

Vijana wanapojitokeza kwa wingi kupiga kura, wanakuwa na uwezo wa kuchagua viongozi bora, kuleta mabadiliko ya sera, na kuboresha hali ya maisha yao na jamii kwa ujumla.

Ni wakati sasa wa kuhakikisha kuwa vijana wanatambua nguvu ya kura yao na kutumia haki yao ya kikatiba kwa manufaa ya Taifa.

Related Posts