Upatikanaji maji Mwanza bado changamoto

Mikoani. Takwimu za Sensa ya Majengo ya Mwaka 2022 zinaonyesha asilimia 24.9 ya majengo  milioni 13.9 (13,907,951) ya Tanzania Bara yana huduma ya maji, huku hali ikiwa tofauti kwa majengo milioni 10.

Kwa mujibu wa sensa hiyo, huduma ya maji katika jengo inahusisha uwepo wa maji ndani ya jengo au kwenye kiwanja cha jengo husika.

Mikoa yenye asilimia kubwa ya majengo yenye huduma ya maji ni Dar es Salaam (asilimia 62.9), Kilimanjaro (asilimia 46.8) na Arusha (asilimia 36.6) na mikoa yenye asilimia ndogo ya majengo yenye huduma ya maji ni Lindi (asilimia 10.3), Singida (asilimia 12.2) na Simiyu (asilimia 12.5).

Idadi hiyo ndogo ya majengo yenye huduma ya maji inaakisi malalamiko ya baadhi ya wananchi nchini kulalamikia changamoto ya maji, wengine wakidai kuikosa kabisa na wengine kuipata kwa mgao.

Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya wananchi hao wamesema kutokana na changamoto hiyo mbali na kuwarudisha nyuma kimaendeleo, pia wapo hatarini  kupata magonjwa kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama.

“Maji ni changamoto sisi tunapata kwa mgawo inaweza kupita siku nne hatujapata au wiki ikapita hatujapata na hata yakija yanakuja kwa kuvizia… hasa usiku watu wakiwa wamelala, ukiamka asubuhi maji hayapo.

“Tunaomba Serikali itusaidie na sisi tupate maji kama wengine kwa sababu kuna wakati tunalazimika kutumia maji yasiyo safi na salama kiasi cha kuhatarisha afya zetu,” amesema Dastani Maila, mkazi wa Nyasaka A Kata ya Kawekamo, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.

Akiunga mkono hoja hiyo, Mkazi wa Mtaa wa Ilhila, Kata ya Buhongwa, jijini Mwanza, Fatuma Omary amesema mbali na kupata maji mara mbili kwa wiki, wakati mwingine hupata maji hata mara moja kwa wiki na kuwafanya wananchi wasio na matenki kutumia maji yanayotiririka mitaroni kutokana na chemchem.

“Sisi tunapata maji mara mbili kwa wiki, hali hii inasababisha tununue vifaa vingi vya kuhifadhia maji, maana wakati mwingine maji yanamaliza hata wiki hayajatoka, kwa hiyo unakuta sebule badala iwe imejaa samani za ndani, inajaa majaba, ndoo na madumu ya maji,” amesema.

Changamoto ya maji pia imelalamikiwa na wananchi wa vijiji vya Nyaholomgo, Ukiriguru, Usagara, Nyashishi, Nyang’homango na Bukumbi Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wakidai wanalazimika kuchangia maji na wanyama, wakiwemo fisi.

Mkazi wa Kijiji cha Nyangholongo, Farida Ally Said amesema kuna kipindi wanapata shida kupata maji, hivyo kulazimika kuchota maji umbali mrefu kwenye visima vya asili vya wazi.

“Kama mvivu, unaumwa au umechoka kufuata maji visimani kuna watu wa baiskeli wanaouza maji Sh1,500 zinakuwa ndoo tatu,” amesema.

Mkazi wa Kijiji cha Usagara, Mabula Bunela amesema kuwa kijiji cha Usagara tatizo la maji safi na salama ni kubwa na la muda mrefu.

“Tunatoa huduma ya kuchota maji na kuwapelekea majumbani kwa kila dumu la lita 20 kwa Sh300 hadi Sh500, tuko watu 12 tunaotoa huduma ya kuchota maji kwa kutumia baiskeli. Pia watu wanafuata wenyewe, tatizo hili ni kubwa, imekuwa hadithi Usagara kupata maji ya Bomba wakati Ziwa Victoria lipo karibu sana,” Bunela.

Naye Ruth Mkandya,  Mkazi wa Kijiji cha Bukumbi ambaye pia ni diwani mstaafu viti maalumu Tarafa ya Usagara, amesema licha ya Kijiji cha Bukumbi kuwa kilometa tatu kutoka lilipo Ziwa Victoria, lakini hawana maji ya bomba, hivyo kuwalazimu kununua  ndoo moja ya maji Sh500.

Changamoto hiyo pia imelalamikiwa na wakazi wa Kitongoji cha Madukani Kata ya Kiluvya wilayani Kisarawe, wakati wa uzinduzi wa rasimu ya katiba ya umoja ulioanzishwa na wanachama 210 wenye lengo la kusaidiana katika masuala ya kijamii na kiuchumi uliofanyika mkoani Pwani.

Mkazi wa Tondoloni, Melina Munis amesema maji yanapatikana katika maeneo mengine, lakini hayafiki kwao, licha ya ahadi za kupata huduma hiyo siku za Ijumaa na Jumamosi, hivyo kuongeza makali ya maisha.

“Tondoloni hatupati maji, hii ni tatizo kubwa kwetu,” amesema Munis.

Mwenyekiti  wa Kitongoji hicho, Godwin Mariki amekiri uwepo wa  changamoto hiyo na kusema ongezeko la watu kutoka 2,900 mwaka 2019 hadi 13,000 kwa sasa linaathiri huduma ya maji, akidai Serikali inatarajia kupeleka hivi karibuni mradi wa maji eneo hilo.

Mbali na changamoto ya maji, wananchi hao wamelalamikia miundombinu mibovu inayowafanya wapate adha ya usafiri, hasa nyakati za usiku na hutumia usafiri wa pikipiki kwa Sh4,000.

“Tunatumia gharama kubwa ya nauli kwa bodaboda kuanzia saa 12:00 jioni tunatakiwa kulipa Sh4,000 kwa safari moja, tunaumia,” amesema Nuru Salumu.

Hata hivyo, Mariki amesema atawasiliana na mamlaka husika kuwezesha daladala kufika eneo hilo, huku katibu wa kikundi cha ujirani na maendeleo,  Martin Mbokosi akidai mabadiliko makubwa yameonekana tangu kuanzishwa kwa umoja huo, ikiwemo kuimarika hali ya ulinzi na kudumisha uhusiano mwema miongoni mwa wanachama.

Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa), Dioniz Kidai akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, amesema hali ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Mwanza ni lita milioni 138 kati ya lita milioni 188 zinazohitajika, hivyo kufanya jiji hilo kuwa na upungufu wa lita milioni 50.

Kidai amesema japokuwa kuna baadhi ya maeneo yanapata mgawo wa maji, mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali huku malengo yakiwa ni kumaliza changamoto hiyo kufikia mwaka 2035.

“Tuna miradi mikubwa mitatu tunayoendelea kuitekeleza ambayo yote ni matokeo ya kukamilika kwa mradi wa maji chanzo cha Butimba ambao unazalisha lita milioni 48 kwa sasa, lakini malengo ni kuuongezea uwezo wa kuzalisha lita milioni 160.

“Tunatekeleza mradi wa ujenzi wa matenki matano ya kuhifadhi na kusambaza maji maeneo ya Nyamazobe, Fumagila, Usagara, Kagera na Bujora. Mradi huu pia unahusisha ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji (bomba) pamoja na ufungaji wa pampu zitakazotoa maji katika vituo vya uzalishaji kwenda kwenye matenki hayo na kuwafikia wananchi,” amesema Kidai.

Ameongeza kuwa, ” mradi wa uboreshaji wa chanzo cha maji Igombe unaotekelezwa kwa ushirikiano baina ya Mwauwasa na Shirika la Maji la Uholanzi (Vitens Evides International (VEI) unahusisha maboresho (upanuzi) wa chanzo cha maji Igombe, miundombinu ya usambazaji maji pamoja na magati takribani 20.

“Pia tunatekeleza mradi wa matokeo ya haraka (Quick win) katika eneo la Sahwa, Kata ya Buhongwa ambao mpaka sasa umefikia asilimia 90 na inahusisha  ulazaji wa bomba la inchi 12 kutoka Kituo cha Sahwa kwenda Buhongwa), kazi hiyo imekamilika kinachoendelea ni kuwaunganishia wateja huduma,” amesema Kidai.

Hata hivyo, Kidai amsema mamlaka hiyo ipo mbioni kuanza kutekeleza mradi wa upanuzi wa chanzo cha Kapriponti, sambamba na kuanza kutekeleza mradi mpya wa chanzo cha maji cha Mwanza Kaskazini na ukikamilika changamoto ya maji jijini humo itakwisha, hivyo kuwaomba wananchi kuwa na subira kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.

Imeandikwa na Saada Amir, Anania Kajuni, Twalad Salum na Sanjito Msafiri.

Related Posts