Wacheza bao walivyoasisi jina la Mwanza

Siku tulifika Mwanza tulipokewa vizuri…

Hizi ni baadhi ya beti za wimbo Mwanza uliowahi kuimbwa na nguli wa muziki wa dansi nchini, hayati Remmy Ongala akiusifu mji huo.

Huwezi kuielezea kanda ya ziwa bila ya kuutaja Mkoa wa Mwanza, eneo lenye maendeleo zaidi sio tu kanda hiyo lakini pia eneo zima la kaskazini magharibi mwa nchi yetu.

Mkoa wa Mwanza una historia ya kuvutia kuhusu asili ya jina hilo.

Kwa mujibu wa Chifu wa Mkoa wa Mwanza, Aron Mikomangwa, jina la Mwanza linatokana na neno la kabila la Kisukuma ‘Ng’vwanza’  linalomaanisha kuendelea kwa jambo.

Wajerumani waliposhindwa kulitamka, ndipo Mwanza likaasisiwa.

Chifu huyo anasema zamani  wenyeji walikuwa na mazoea ya kucheza bao katikati ya mjini maeneo ya Gandhall  kabla hapajajengwa majengo yaliyopo sasa.

Anasema kulikuwa na sehemu ya kukutanikia kwa wachezaji hao na walipokuwa wakija baada ya kutoka kula au kwa jambo lolote , walikuwa wakiulizana mmefikia wapi na bao au mnaendeleaje.

‘’  …walipokuwa wanakuja baada ya kuwa wametoka kidogo au wametoka kula ndio wanaanza kuulizia kwamba mmefikia wapi kwa kilugha ‘Ng’vwanza hangi’ yaani mmetandaza tena hilo bao kuendelea kucheza,” anasema chifu Mikomangwa.

Anaeleza kuwa  Wajerumani walipokuja na kuanza kuwauliza walikuwa wanafanya nini hapo, wakawa wanawajibu: ‘Twanza hangi’  yaani tumeanza tena.

‘’ Kwa hiyo  hilo ndio chimbuko la Mwanza  neno linalomaanisha  tumeanza kutandika tena kete kwa ajili ya kucheza  bao. Lakini kutokana na matamshi, Wajerumani wakaita Mwanza,”anaeleza.

Baada ya Tanganyika kupata uhuru, Mkoa wa Mwanza ulianzishwa rasmi mwaka 1963 ukiwa na wilaya nne za Ukerewe, Geita, Mwanza na Kwimba. Na baadaye kufuatiwa na wilaya za Magu, Sengerema, Misungwi, Ilemela na Nyamagana.

Related Posts