Yanga kazi ndo imeanza | Mwanaspoti

KIKOSI cha Yanga usiku wa jana kilikuwa uwanjani kuumana na KMC katika mechi ya Ligi Kuu Bara na sasa kinajiweka sawa kukabiliana na Pamba Jiji, huku kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi akisema kazi ndo imeanza kwani anamalizia ligi kisha kusikilizia droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ajue ataangukia kundi lipi.

Yanga ni moja ya timu 16 zilizopenya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na droo na michuano hiyo na ile ya Kombe la Shirikisho inayoshiriki Simba itafanyika Jumatatu ijayo ambapo timu zitapangwa kabla ya mechi kuanza kupigwa ndani ya Oktoba.

Watetezi hao wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, msimu uliopita walifika robo fainali ya CAF na kocha Gamondi amepania msimu huu kuona timu hiyo inafika mbali zaidi, na pia kutetea mataji inayoyashikilia baada ya awali kurejesha Ngao ya Jamii iliyokuwa imechukuliwa na Simba msimu uliopita.

Chini ya Gamondi, Yanga katika mechi nane (kabla ya jana dhidi ya KMC) za mashindano yote ilikuwa imefunga jumla ya mabao 25 na yenyewe kuruhusu moja tu, kitu kinachompa jeuri Gamondi anayebebwa na uzoefu na kuwa na kikosi kilichokaa pamoja kwa muda mrefu kulinganisha na makocha wa Simba na Azam.

Simba inanolewa na Msauzi Fadlu Davids akiwa ni kocha mpya aliyetua hivi karibuni akitokea Raja Casablanca ya Morocco, huku Azam ipo chini ya Rachid Taoussi kutoka Morocco, tofauti na Gamondi mwenye msimu wa pili, huku akiwa na wachezaji waliozoeana walioongezewa wakali wengine wazoefu.

Yanga imeingiza wachezaji saba wapya, na sita ni wazoefu wa ligi hiyo ambao ni Clatous Chama, Prince Dube, Duke Abuya na Aziz Andabwile wanaotumika kila mara. Pia kuna kipa Khomeny Abubakar na Jean Baleke ambao bado hawajaanza kutumika kikosini, lakini kuna Chadrack Boka beki kutoka DR Congo anayekipiga kila uchao.

Kocha Gamondi alisema anafahamu ugumu utakaoikabili Yanga katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho kwa wapinzani wakuu kama Simba na Azam, ambazo bado hajakutana nazo hadi sasa katika ligi hiyo, licha ya kuzinyuka katika mechi za Ngao ya Jamii, lakini amejipanga kuona kila kitu kinakuwa sawa.

Yanga iliifunga Simba kwa bao 1-0 katika nusu fainali ya Ngao ya Jamii, kisha kuifunga Azam kwa mabao 4-1 na Gamondi alisisitiza kazi kwa msimu wa 2024-25 ndo imeanza na akili ni kuona kila lengo walilojiwekea linatimia ikiwamo kuifikisha timu hiyo mbali katika michuano ya CAF.

Yanga imekuwa ikisema kila mara kwamba inahitaji kwanza kuzoea makundi ya Ligi ya Mabingwa, kisha misimu ijayo huko ndiyo ipange malengo makubwa zaidi, lakini tangu imesema hivyo imecheza makundi mara mbili mfululizo chini ya Gamondi, msimu uliopita walipofika hadi robo fainali na msimu huu.

Mabosi wa Yanga wanaamini kwamba, timu hiyo kuingia makundi kwa sasa ni mafanikio makubwa kwani kabla ya msimu uliopita, walikuwa wakiifukuzia rekodi hiyo kwa takribani miaka 25 tangu ilipocheza mara ya kwanza 1998.

Timu hiyo imepangwa chungu namba mbili pamoja na CR Belouizdad ya Algeria, Pyramids ya Misri na Raja AC ya Morocco ambazo hawezi kupangwa nazo, huku vigogo Al Ahly ya Misri, Esperance ya Tunisia na TP Mazembe ya DR Congo na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini vikiwa chungu namba moja.

Timu nyingine ni Al Hilal ya Sudan, Orlando Pirates pia ya Sauzi, Segrada Esperanca ya Angola na FAR Rabat ya Morocco zikiwa chungu namba tatu na MC Alger ya Algeria, Djoliba ya Mali, AS Maniema ya DR Congo na Stade ‘dAbidjan ya Ivory Coast zikiwa chungu cha nne.

Yanga itarudi uwanjani tena Alhamisi hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, kuikabili Pamba Jiji iliyorejea katika Ligi Kuu baada ya kupita miaka 23 tangu iliposhuka mwaka 2001, huku ikiwa haina mwenendo mzuri hadi sasa kwani imecheza mechi sita na kutoka sare nne kupoteza mbili bila kuonja ushindi wowote.

Related Posts