Zahera aanza kunogewa Namungo | Mwanaspoti

BAADA ya Namungo kupata ushindi wa bao 1-0 juzi dhidi ya Tanzania Prisons, kocha mkuu wa timu hiyo Mkongomani, Mwinyi Zahera amesema, ameridhika na viwango vya wachezaji walivyovionyesha huku akiwataka kuendelea kupambana zaidi ya hapo.

Zahera aliyekalia kuti kavu la kutimuliwa kikosini humo, amezungumza hayo baada ya timu hiyo kupata ushindi huo ukiwa ni wa pili mfululizo kufuatia kuifunga Coastal Union mabao 2-0, mechi ikipigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Septemba 17.

“Kadri unavyozidi kupoteza mchezo ndivyo ambavyo hata morali ya wachezaji kiujumla inashuka lakini nashukuru mechi hizi mbili zimekuwa na utofauti mkubwa kwa sababu wachezaji wametimiza majukumu yao vizuri, yaliyotupatia matokeo chanya.”

Kocha huyo aliyejiunga na Namungo Desemba 30, 2023 akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Denis Kitambi alisema, moja ya changamoto kubwa iliyopo ndani ya kikosi hicho ni kutokuwa na balansi nzuri katika safu ya uzuiaji na ushambuliaji.

“Michezo miwili ya mwisho ndio tumekuwa na balansi nzuri lakini ukiangalia tangu tumeanza Ligi tumekuwa tukiruhusu bao, sio mwenendo mzuri kwetu ingawa jambo kubwa ni kupata matokeo chanya ili kupunguza presha ambayo ilianza kujitokeza.”

Namungo ilianza Ligi Kuu msimu huu kwa kupoteza michezo mitatu ikichapwa 2-1 na Tabora United, 2-0 dhidi ya Fountain Gate na 1-0 kutoka kwa Dodoma Jiji kisha kuzinduka kuanzia kwa Coastal Union na Prisons.

Related Posts