Simba SC imeanza msimu wa 2024/2025 kwa kishindo ikilinganishwa na msimu uliopita, ikiwa imecheza mechi sita na kuonyesha kiwango bora licha ya kuwa na wachezaji wapya 14 kwenye kikosi chao.
Ushindi wa mechi nne mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tabora United (3-0), Fountain Gate (4-0), Azam FC (2-0) na Dodoma Jiji (1-0), umewafanya mashabiki wao kuwa na matumaini makubwa na chama hilo.
Pia katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC), Simba wamefanikiwa kutinga hatua ya makundi baada ya kuwashinda Al Ahly Tripol ya Sudan kwa mabao 3-1.
Mshambuliaji wa Simba, Leonel Ateba ambaye tayari amefunga mabao mawili msimu huu, ameweka wazi siri iliyowafanya kuwa na mwanzo mzuri wa msimu.
“Kikubwa ambacho kimetusaidia ni upendo na mshikamano uliojengwa na benchi letu la ufundi chini ya kocha Fadlu Davids. Tumekuwa kama familia na hata wachezaji wa akiba wanatoa sapoti kubwa kwa wale wanaoanza mechi,” amesema Ateba.
Kwa upande wake, kiungo Debora Fernandez aliyesajiliwa msimu huu, ameongeza kuwa moja ya sababu zinazowasukuma kuendelea kufanya vizuri ni jinsi timu ilivyojipanga na jinsi mashabiki wanavyowaunga mkono.
“Mashabiki wetu ni sehemu muhimu ya mafanikio. Wanatujenga kisaikolojia na tunapokuwa uwanjani tunahisi nguvu yao. Pia mshikamano ndani ya timu kuanzia benchi la ufundi hadi wachezaji umekuwa chachu ya mafanikio haya,” amesema Fernandez.
Msimu huu Simba imekuwa na wachezaji wengi wapya, jambo ambalo lilizua wasiwasi miongoni mwa baadhi ya mashabiki. Hata hivyo, kocha Fadlu Davids ameunganisha kikosi na kujenga mazingira mazuri ya kufanya kazi kwa ushirikiano.
“Hatua yetu ya kwanza ilikuwa ni kujenga msingi wa kuaminiana na kuheshimiana ndani ya timu. Hii imetusaidia wachezaji wapya kuzoeana haraka na kuingia kwenye mfumo wa timu,” amesema Davids.
Mshikamano huu umeonekana wazi katika mechi zao, ambapo hata pale mchezaji mmoja anapofanya makosa, wachezaji wenzake wanakuwa tayari kusaidiana. Wakati Simba ilipocheza dhidi ya Azam FC, kulikuwa na hali ya ushirikiano mzuri kati ya safu ya ulinzi, kiungo, na ushambuliaji, hali ambayo iliwanyima Azam nafasi ya kujaribu mashambulizi mengi hatari.
Mbali na ushirikiano wa ndani ya uwanja, wachezaji wa Simba wamekuwa wakionyesha hali ya nidhamu na bidii mazoezini, jambo ambalo limewasaidia kuimarisha uwezo wao binafsi na wa timu kwa ujumla.
Kabla ya mechi yao ya jana dhidi ya Dodoma Jiji, Simba walikuwa na morali ya juu kutokana na matokeo mazuri waliyopata katika mechi zilizopita.
“Tunajua kila mechi ni muhimu, na tunachukua kila mpinzani kwa uzito sawa. Mafanikio haya tuliyopata ni matokeo ya juhudi na umoja wetu kama timu,” amesema Fernandez.
Kwa upande wa mashabiki, wamekuwa na mchango mkubwa katika kuipa timu nguvu.
“Mashabiki wetu wamekuwa sehemu ya timu. Wanatupa nguvu kubwa tunapokuwa uwanjani. Wanajua tunapohitaji sapoti na wao hawachoki kutupa nguvu hizo,” amesema Ateba akifafanua jinsi mashabiki wanavyowasaidia.
Simba wanajivunia kuwa na benchi la ufundi imara ambalo limeweza kuleta mabadiliko chanya, huku Fadlu Davids akiweka mkazo kwenye nidhamu, juhudi, na ushirikiano.
“Tunafanya kazi kama timu moja, na mafanikio ya mwanzo wa msimu huu ni matokeo ya juhudi za pamoja. Tunaelewa kuwa safari bado ni ndefu, lakini tunajivunia kuwa kwenye njia sahihi,” amesema kocha huyo.
Licha ya kuwa na wachezaji wapya, Simba imeonyesha kuwa na uwezo wa kuunganisha vipaji na kujenga kikosi imara.
Mafanikio kwenye mechi za mwanzo yamethibitisha kuwa ingawa walikuwa na changamoto za wachezaji wengi wapya, wameweza kuhimili mikikimikiki ya ligi na mashindano ya kimataifa.
Katika mechi zao za hivi karibuni, Simba wameonyesha uwezo wa kudhibiti mpira na kushambulia kwa kasi, huku wakitegemea zaidi uchezaji wa pamoja kuliko ubora wa mchezaji mmoja mmoja.
“Kila mchezaji ana nafasi yake kwenye timu, na tunafanya kazi kama kundi. Hii inatupa nguvu zaidi,” amesema Fernandez.