Akizindua rasmi mpango na bima hiyo mpya ya afya katika Kaunti ya Kakamega, Waziri wa Afya wa Kenya, Debra Barasa, aliutetea mfumo huo aliosema azma yake ni “kuwapa huduma za afya Wakenya wote.”
Mapema wiki hii, Kamati ya Afya ya Bunge iliupa ridhaa mpango huo mpya baada ya hoja za kamati hiyo kuhusu utendakazi kujibiwa.
Soma zaidi: Kenya yarekodi kisa cha kwanza cha maradhi ya mpox
Awali, kulikuwa kumetajwa mapungufu kwenye mfumo mzima wa jinsi ya kubaini kiwango cha fedha watakazochangia wasiokuwa na ajira rasmi, huku wale wenye ajira rasmi wakikatwa asilimia 2.75 ya mshahara ili kuchangia kwenye bima hiyo mpya iitwayo kwa kifupi SHIF.
Hili ni ongezeko kubwa ukizingatia kuwa chini ya mpango wa awali wa Huduma ya Bima ya Taifa (NHIF), waliokuwa na mishahara mikubwa walilazimika kuchangia shilingi 1,700 pekee kinyume na mfumo mpya wa SHIF.
Hakuna atakayekosa huduma
Mfumo huo ulifanyiwa majaribio katika Kaunti za Turkana, Tana River, Narok, Migori, Bungoma, Bomet, Kiambu na Nairobi ili kubaini vigezo vya kuchangia vya wasiokuwa na ajira rasmi.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), Elijah Wachira, alisisitiza kuwa hakuna “atakayekosa huduma hata wakati ambapo mfumo unachukua sura mpya.”
Soma zaidi: Jimbo la Marsabit Kenya lathibitisha kuzuka kwa ugonjwa wa Surua
Kuanzia Jumanne (Oktoba 1), kila mteja wa hospitali za umma aliyekuwa anatumia bima ya NHIF, analazimika kusajiliwa upya na SHA, ambapo azma ya serikali ni kukusanya shilingi bilioni 148 kwa mwaka kupitia mfumo huo mpya wa bima ya SHIF.
Hayo yakiendelea, Seneta Okiya Omutata wa Kaunti ya Busia aliwasilisha malalamiko rasmi mahakamani kupinga utekelezaji wa bima ya afya ya SHIF “kwa kukosa sheria mahsusi ya utendaji kazi.”
Wasiwasi nao ulikuwa umetanda kuhusu azma ya kupunguza gharama za operesheni kutozidi asilimia 5, ikizingatiwa kuwa katika mfumo wa NHIF, kibarua kilikuwa kigumu kusalia chini ya asilimia 15.