Stand United ‘Chama la Wana’ ya Shinyanga imeanza kwa kishindo Ligi ya Championship kwa kushinda mechi mbili na kuvuna pointi sita, huku wafungaji wa mabao mawili ya timu hiyo wameapa kuendelea kuwa tishio kwa timu pinzani msimu huu.
Katika mechi mbili dhidi ya Kiluvya United na Transit Camp FC, Chama la Wana limefunga mabao mawili yakipachikwa na Andrew William na Nassoro Iddi, huku ikiwa haijaruhusu wavu wake kutikiswa.
William amesema siri ya mwanzo huo mzuri ni sapoti wanayoipata kutoka kwa mashabiki wao na kusikiliza na kufuata maelekezo wanayopewa na benchi la ufundi na kuyafanyia kazi kwa ufanisi na kuzitendea haki mbinu za kocha.
“Nawapongeza wana Shinyanga kwa kutuunga mkono kwa wingi katika michezo yetu, wanaonyesha wana umoja na sisi, jambo hili limetuongezea morali na ujasiri, nasi hatutawaangusha, tutaitumia kutupa hamasa na kuendelea kushinda mechi zetu,” amesema William.
Iddy amesema “Kufunga bao katika mchezo wa kwanza ni jambo zuri na linanipa mwanga wa kuwa na mwanzo mzuri, nitazidi kupambana kuipa timu yangu ushindi, mashabiki waje sisi tupo tutapambania timu yao kwa sababu tuna malengo ya kupanda Ligi Kuu.”
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Daud Macha, amesema licha ya mwanzo huo mzuri bado kikosi chao hakijawa na makali katika eneo la umaliziaji kwani wanawakosa baadhi ya washambuliaji kutokana na changamoto ya kadi na majeraha huku akitamba watakuwa tishio kikosi chao kikitimia.
“Tukipata washambuliaji wetu halisi wana Shinyanga watafurahi na wataona timu inavyocheza, inaweza ikawa ndiyo Barcelona ya Shinyanga kwa mwaka huu. Benchi tumejiandaa vizuri wachezaji tulionao na jinsi tulivyosajili wote wana uwezo wa kufanya matokeo yakabadilika,” amesema Macha.
“Kwa jinsi tunavyoandaa timu na vijana, wakienda vile benchi la ufundi tunavyotaka na uongozi ukapata utulivu na sapoti ikawepo kubwa, tunaona bila shaka tunaweza kuvuna pointi sita katika mechi zetu mbili zijazo na kuendelea kupata matokeo mazuri,” amesema.