KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids anafahamu kwamba Oktoba 19 mwaka huu ana kibarua cha kukutana na Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam wakiwa wenyeji.
Wekundu wa Msimbazi wameshinda mechi zote nne za Ligi Kuu Bara tangu ulipoanza msimu huu na bahati nzuri kwao ni kwamba hawajaruhusu nyavu zao kutikiswa, huku langoni kukiwa na kipa Moussa Camara aliyewapokonya namba makipa waliomtangulia kutua kikosini hapo
Lakini katika kuuendea mchezo huo, tayari Kocha Fadlu, raia wa Afrika Kusini ameandika rekodi mpya ndani ya kikosi hicho alichoanza kukinoa msimu huu akichukua mikoba ya Abdelhak Benchikha.
Rekodi mpya aliyoiweka Fadlu zikiwa zimesalia siku 18 kabla ya kucheza na Yanga ni ile ya kushinda michezo minne mfululizo ya mwanzo ya Ligi Kuu Bara bila ya kuruhusu bao.
Fadlu amefanya hivyo ikiwa mara ya mwisho rekodi hiyo iliwekwa msimu wa 2020-2021 na watani wao wa jadi, Yanga ambao msimu huu nao mechi tatu za kwanza wameshinda mfululizo bila ya kuruhusu bao.
Kabla ya Fadlu kufanya hivyo na Simba, tangu msimu wa 2020-2021, hadi sasa ilikuwa ni Yanga pekee iliyocheza michezo minne mfululizo ya mwanzo wa Ligi Kuu Bara bila kuruhusu bao, ikifanya hivyo msimu wa 2021-2022 kwa kuzichapa Kagera Sugar na Geita Gold bao 1-0, kila mmoja wao.
Baada ya hapo Yanga ikacheza mchezo wa tatu na wa nne kwa kuzichapa KMC na Azam FC mabao 2-0 kila mmoja wao na kuanzia hapo hakuna timu nyingine iliyofanya hivyo, hadi Simba msimu huu chini ya Fadlu Davids ilipojiandikia pia rekodi hiyo.
Msimu wa 2020-2021, Simba ilianza Ligi Kuu Bara kwa kuichapa Singida Black Stars mabao 2-1, ikatoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar, kisha ikaichapa Biashara United ya mabao 4-0 na kuhitimisha mchezo wa nne kwa ushindi wa 3-0 mbele ya Gwambina.
Msimu uliofuata wa 2021-2022, ikaanza kwa suluhu (0-0) na Biashara United, ikashinda michezo miwili mfululizo kwa bao 1-0, dhidi ya Dodoma Jiji na Polisi Tanzania, kisha mchezo wa nne ikahitimisha kwa suluhu (0-0) mbele ya Coastal Union.
Msimu wa 2022-2023, ilifungua pazia la Ligi Kuu Bara kwa ushindi wa mabao 3-0, dhidi ya Geita Gold, ikashinda tena 2-0, na Kagera Sugar huku mchezo wa tatu ikatoka sare ya 2-2 na KMC, kisha kuibuka mechi ya nne na ushindi wa 1-0 na Tanzania Prisons.
Msimu uliopita wa 2023-2024, Simba ilianza Ligi Kuu Bara kwa kuichapa Mtibwa Sugar ugenini kwa mabao 4-2, ikaifunga pia Dodoma Jiji 2-0, ikaitandika Coastal Union 3-0, kisha kuendeleza ushindi Mbeya baada ya kuichapa Tanzania Prisons 3-1.
Ukiangalia tangu msimu wa 2020-2021, Simba ilikuwa ikicheza michezo minne mfululizo ya mwanzo ya Ligi Kuu Bara ikiruhusu bao, ukiacha msimu wa 2021-2022 ambao haikuruhusu bao katika mechi nne za kwanza lakini haikiweza kushinda zote nne.
Chini ya Fadlu msimu huu, Simba imeifikia rekodi hiyo iliyokuwa inashikiliwa na Yanga. Ilianza Ligi Kuu Bara kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United, 4-0 mbele ya Fountain Gate zote kwenye Uwanja wa KMC, ikaifunga Azam FC 2-0 kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar kisha kuichapa Dodoma Jiji bao 1-0.
Mbali na hilo, tangu Simba ipoteze bao 1-0, dhidi ya Yanga katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii Agosti 8, mwaka huu, imecheza jumla ya michezo saba ya mashindano mbalimbali, ambapo kati ya hiyo imeshinda sita na kutoka sare mmoja.
Katika michezo hiyo, Simba imefunga jumla ya mabao 14 ikiwa na wastani wa kufunga mawili kwa kila mchezo, huku ikiruhusu moja tu katika ushindi wa timu hiyo wa 3-1, dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya kwenye Kombe la Shirikisho Afrika Septemba 22.
Akizungumzia mwenendo wa Simba hasa baada ya mchezo na Dodoma Jiji, Fadlu amesema walistahili kufunga mabao mengi kutokana na nafasi nyingi walizotengeneza lakini akawapongeza wachezaji kwa kujitoa na kupata pointi zote tatu.
“Ulikuwa ni mchezo mgumu kwetu, tulitengeneza nafasi nyingi na tulipaswa kufunga mabao matatu au manne, tumecheza mechi ngumu mfululizo, Al Ahli Tripoli, Azam na Dodoma Jiji, unapumzika siku mbili ya tatu unacheza hivyo kiukweli niwapongeze wachezaji,” amesema Fadlu akiongeza sio rahisi kucheza mechi tatu ndani ya siku saba.
Nyota wa zamani wa kikosi hicho, Boniface Pawasa amesema, siri kubwa kwa sasa ni jinsi ambavyo Fadlu ameweza kuishi na wachezaji.
“Nafikiri Simba kwa sasa imepata mtu sahihi kwa sababu eneo la benchi la ufundi lilikuwa halijatulia, nampongeza Fadlu kwa hiki anachoendelea nacho, nadhani akipewa muda zaidi tutashuhudia mafanikio makubwa kutokana na uwezo alionao.”
Kabla ya kujiunga na Simba Julai 5, 2024 akichukua nafasi iliyoachwa na Mualgeria, Abdelhak Benchikha, Fadlu raia wa Afrika Kusini, alitoka kuipa ubingwa wa Ligi Kuu ya Morocco, Raja Casablanca akiwa ni msaidizi wa kocha Mjerumani, Josef Zinnbauer anayeifundisha kwa sasa Al-Wehda FC ya Saudi Arabia.