Hasara 10 za kuchelewa kujiandikisha

Dodoma. Kuchelewa au kushindwa kujiandikisha kwa wakati ili kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 kuna hasara nyingi.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, uandikishaji wapigakura utaanza Ijumaa ya wiki ijayo Oktoba 11-20, 2024 kwa maana zimebaki siku 10.

“Kwa tangazo hili, wananchi wote wanaombwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, kupiga kura, kugombea na kushiriki katika uchaguzi huu ili kupata viongozi bora wa serikali za mitaa kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema Mchengerwa wakati akitoa tangazo la uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024.

Wananchi wanapopoteza fursa hii, wanajinyima haki yao ya kikatiba, wanakosa ushawishi kwenye maamuzi ya uongozi, na wanahatarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Hivyo basi, ni muhimu kwa kila mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura kujitokeza mapema kujiandikisha ili kuhakikisha wanashiriki katika mchakato wa kidemokrasia na kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii zao.

Pia, kujitokeza mapema kujiandikisha kunawasaidia wananchi kuepuka misongamano na changamoto za siku za mwisho za usajili.

Kwa kawaida, hali huwa ngumu zaidi kadiri muda unavyokaribia kwisha, ambapo baadhi ya vituo vya usajili hujaa na kusababisha foleni ndefu na usumbufu kwa watu wanaojitokeza dakika za mwisho.

Pia, kujiandikisha kupiga kura kunawaepusha wananchi na hasara 10 zinazoweza kuwakuta katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi ambao hawakushiriki kuuweka madarakani.

Kukosa haki ya kupiga kura

Hasara kuu inayowakabili wananchi wanaoshindwa kujiandikisha ni kupoteza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.

Kwa mujibu wa sheria, ni wale tu waliojiandikisha kwa wakati katika orodha ya wapigakura watakaoruhusiwa kushiriki katika uchaguzi.

Kukosa fursa hii ni kujiweka pembeni na kupoteza nafasi ya kushiriki katika mchakato muhimu wa kidemokrasia.

Hii ina maana kwamba wananchi hao watashindwa kuchagua viongozi watakaowasimamia kwa miaka mingine mitano, hivyo kutokuwa na sauti katika uongozi wa jamii zao.

Kuweka watu wengine madarakani

Wananchi wanaoshindwa kujiandikisha hupoteza nafasi ya kushawishi matokeo ya uchaguzi.

Kura ni njia ya kuamua nani anakuwa kiongozi, na kwa kushindwa kushiriki, watu wengine watachagua kwa niaba yao.

Pia, inaweza kusababisha viongozi wasiofaa kuchaguliwa na kushika madaraka, hali inayoweza kuwa na athari kwa maendeleo na ustawi wa jamii husika kwenye mtaa, kijiji na kitongoji.

Wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa kila kura ina uzito wake katika mchakato wa kidemokrasia, na mtu anaposhindwa kujiandikisha, anawaachia wengine nafasi ya kufanya maamuzi muhimu kwa niaba yake.

Kuongeza uwezekano wa udanganyifu

Uchelewaji au kushindwa kujiandikisha kwa wapigakura huweza kuongeza uwezekano wa udanganyifu katika uchaguzi.

Mantiki ya hoja hii ni kwamba, kuna uwezekano wa kutoa mwanya kwa watu wasio na sifa za kupigakura kuingizwa kwenye orodha hizo au kwa mbinu za udanganyifu kutumiwa.

Usajili wa mapema wa wapigakura unasaidia kuhakikisha kuwa kila kura ni halali na mchakato mzima unakuwa wa haki. Hivyo basi, uchelewaji unahatarisha uadilifu wa uchaguzi na unaweza kuathiri haki ya matokeo.

Kuzuia maendeleo, kukua uchumi

Viongozi wa serikali za mitaa huchaguliwa kusimamia na kuendeleza maeneo yao kwa ngazi za kijiji, mtaa na kitongoji.

Wananchi wanaposhindwa kujiandikisha kupiga kura, wanapoteza fursa ya kuchagua viongozi bora wenye uwezo wa kusukuma mbele maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa maana hiyo kunaweza kusababisha kusuasua kwa miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa miundombinu, huduma bora za afya, elimu, na upatikanaji wa maji safi.

Kukosa viongozi waadilifu na wenye uwezo kutokana na kutokupiga kura kunaweza kupelekea kudorora kwa maendeleo ya jamii.

Kushindwa kuwajibisha viongozi

Wananchi wanaposhiriki katika uchaguzi, wanakuwa na nguvu ya kuwawajibisha viongozi waliowachagua, kwa sababu viongozi hao wanajua kuwa wamechaguliwa na watu, na hivyo wanawajibika kwa wananchi hao.

Hata hivyo, wananchi wanaposhindwa kujiandikisha na kupiga kura, wanapoteza fursa ya kuwawajibisha viongozi wao.

Pia, inaweza kusababisha viongozi kutowajibika ipasavyo kwani wanajua kuwa wananchi hawana sauti au nguvu za kuwaondoa madarakani kutokana na kutoshiriki kwenye mchakato wa uchaguzi.

Kuweka kizazi kijacho katika hali duni

Kushindwa kujiandikisha na kupiga kura kunachangia kudhoofisha demokrasia kwa kizazi kijacho.

Vijana wanaojifunza kutoka kwa wazazi wao na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia watapata ujumbe potofu pale wanapoona wazazi wao hawashiriki kikamilifu katika uchaguzi.

Inaweza pia kusababisha kizazi kijacho kuwa na mtazamo duni kuhusu uchaguzi, demokrasia, na uwajibikaji wa viongozi.

Matokeo yake ni kwamba, demokrasia inakuwa dhaifu, na kizazi kijacho kinaweza kutengwa na masuala ya uongozi na utawala.

Kuwepo viongozi wasiofaa, rushwa kuongezeka

Wananchi wanaposhindwa kujiandikisha kwa wakati, wanatoa mwanya kwa viongozi wasiofaa kuingia madarakani.

Mara nyingi, uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa unahusisha changamoto za kiutendaji zinazoweza kuleta matatizo makubwa kwenye jamii.

Viongozi wasiofaa wanaweza kuendekeza rushwa, matumizi mabaya ya rasilimali, na kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo.

Aidha, rushwa inaweza kuongezeka kutokana na ukosefu wa usimamizi mzuri wa rasilimali za umma, hali inayodhoofisha maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Kuongeza mgawanyiko katika jamii

Wananchi wanaposhindwa kujiandikisha na kushiriki kwenye uchaguzi, wanaweza kuchangia mgawanyiko katika jamii.

Na hii ni kwa sababu kundi la wachache linaloshiriki linaweza kuwa na masilahi yasiyo ya wengi, hivyo kuchagua viongozi ambao hawazingatii mahitaji ya watu wote.

Mgawanyiko huo pia unaweza kusababisha migogoro ndani ya jamii, hasa pale ambapo wananchi wanahisi hawana uwakilishi wa haki katika uongozi wa serikali za mitaa.

Kukosa sauti katika maamuzi muhimu

Viongozi wa serikali za mitaa wanahusika moja kwa moja katika kufanya maamuzi kuhusu miradi ya maendeleo na usimamizi wa rasilimali za umma katika maeneo yao.

Wananchi wanaoshindwa kujiandikisha na kupiga kura wanakosa fursa ya kuwa na sauti katika maamuzi haya.

Kwa maana hiyo, masuala ya msingi kama ugawaji wa ardhi, matumizi ya fedha za maendeleo, na utoaji wa huduma za jamii yanaweza kufanywa bila kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi ambao hawakushiriki katika kuwaweka viongozi hao madarakani.

Kudhoofisha amani, utulivu

Ushiriki mdogo katika uchaguzi unaweza kudhoofisha amani na utulivu wa kisiasa.

Wananchi wanaposhindwa kujiandikisha na kupiga kura, kuna uwezekano wa kuzuka kwa migogoro ya kisiasa, hasa pale ambapo watu wanahisi kuwa viongozi waliochaguliwa hawakupatikana kwa njia ya haki.

Hali hii inaweza kusababisha machafuko au maandamano yanayodai mabadiliko ya uongozi, hali inayoweza kuathiri amani na utulivu wa kijamii.

Related Posts