Jina Dodoma na kisa cha tembo aliyezama

Dodoma. Mkoa wa Dodoma ndiyo makao makuu ya nchi ya Tanzania, ukiwa umeanzishwa miaka ya 1900.

Pamoja na ukongwe wake mkoa huu hasa Jiji la Dodoma, limebeba mambo mengi ya kihistoria ikiwemo majengo, mitaa na maeneo mengi ya kihistoria ambayo yanatumika mpaka sasa na yana ubora ule ule wa mwanzo.

Miongoni mwa majengo ya kale ambayo pia ni kivutio kwa Jiji la Dodoma ni pamoja na Stesheni za treni zilizopo Ihumwa, Dodoma na Zuzu ambazo zilijengwa kipindi cha mkoloni lakini zinatumika mpaka sasa.

Majengo mengine ni nyumba za kuabudia kama vile Msikiti wa Jamatini, Kanisa kuu la Anglikana, Kanisa la Romani Katholiki, Msikiti wa Makuberi uliopo Kikuyu na kanisa la Romani Katholiki lililopo Bihawana ambalo lina miaka zaidi ya 100 lakini bado linatumika mpaka leo kwa ajili ya ibada.

Eneo lingine ambalo ni la kihistoria ni makaburi ya askari waliopigana kwenye vita ya pili ya Dunia ya mwaka 1934 hadi 1945 ambayo yapo katikati ya jiji pembeni mwa reli ya kati ambayo yanatunzwa mpaka sasa na Umoja wa  Mataifa.

Majengo mengine ni yaliyopo kwenye hospitali ya rufaa ya  Mkoa wa Dodoma yaliyojengwa mwaka 1920 kama Kituo cha afya kilichokuwa kikihudumia wafanyakazi wa Kijerumani.

Kwa mujibu wa Meya wa zamani wa Manispaa ya Dodoma (sasa ni Jiji la Dodoma) kuanzia mwaka 1994 hadi 2001, Peter Mavunde majengo hayo ya kihistoria yameendelea kutumika mpaka sasa kwa sababu yanatunzwa vizuri na waliokabidhiwa kuyatumia.

Anasema sehemu kubwa ya majengo hayo yapo na yanaendelea kutumika isipokuwa kwenye eneo ambalo limebeba historia ya jina la Mkoa wa Dodoma ambapo tembo alizama (Idodomya).

Anasema eneo hilo lipo Kikuyu ambapo historia inaeleza kuna tembo alizama kwenye bustani iliyokuwa inamilikiwa na mkoloni mmoja,  kitendo ambacho kwa lugha ya wenyeji wa Mkoa wa Dodoma yaani Wagogo  walikiiita  Idodomya lakini wazungu walishindwa kulitamka na kuita Dodoma.

Anasema eneo hilo lipo karibu na Chuo Kikuu cha St John’s ambapo kwa kutojua historia, uongozi wa jiji uligawa eneo hilo kwa mtu ambaye alijenga baa.

Mavunde anasema baada ya kuona hivyo wazee wa Mkoa wa Dodoma ambao wanajua historia ya eneo hilo,  waliiandikia barua Halmashauri ya Jiji kuomba eneo hilo litunzwe kwa kuwa limebeba historia muhimu ya jina la Mkoa wa Dodoma.

Anasema jiji lilikubali na sasa eneo hilo limeachwa kwa ajili ya historia na kila anayehitaji kupaona huwa anakwenda kutembelea.

Hata hivyo, kabla ya Idodomya au idodomia, mji huo awali ulijkulikana kwa jina la Calangu au Chalangu.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo kwenye wavuti wa Jiji la Dodoma, kwa miaka mingi mji wa Calangu  haukuwa na wenyeji  maalumu.

Kulikuwa na wahamiaji kutoka maeneo tofauti wakiwamo  Wamanghala, Wabambali, Wayenzele na Wanghulimba.

Related Posts