MWANDISHI wa Habari za uchunguzi nchini, Erick Kabendera, amesema anakusudia kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa nchini kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ya Dar es Salaam, ambayo ilitupilia mbali shauri lake namba 12799/2024, aliyoifungua dhidi ya kampuni ya huduma za mawasiliano ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Kabendera ameyasema hayo leo tarehe 1 Oktoba 2024, kupitia video yake fupi kwa vyombo vya habari na kueleza kuwa tayari ameshawasiliana na mawakili wake, waliopo nchini Uingereza na Afrika Kusini.
Kabendera amesema hoja ya kufutwa kwa kesi yake kwa maelezo ilifunguliwa nje ya muda, ni kwa sababu alitoka gerezani akiwa mgonjwa na kipaumbele chake na famili yake kilikuwa ni matibabu yake.
Kabendera amesema kuwa ndugu zake walipoona afya yake imedhoofika walidhani ameathiriwa na sumu.
“Nilipotoka jela nilikuwa nadaiwa kiasi kikubwa cha fedha; pili hali yangu ya afya ilikuwa ya mashaka kiasi iliwapa wasiwasi ndugu zangu kwa hiyo kipaumbele cha kwanza kilikuwa afya yangu, lakini kuhusika kwa mtandao wa Vodacom kwenye utekwaji wangu kupo wazi,” amesema.
Kabendera aliishtaki Vodacom kuwa ndiyo iliyofanikisha kukamatwa na polisi nyumbani kwake Julai 29, 2019.
Kabendera alidai kutokana na tukio hilo, amepata madhara mbalimbali yakiwamo ya kiuchumi na yasiyo ya kiuchumi, ya kijamii, maumivu ya kiakili na kimaono, ya kutokufurahia maisha, ya maendeleo binafsi na hadhi yake katika jamii na kutokuaminiwa kitaaluma.
Alikuwa anaitaka kampuni hiyo imlipe Dola 10 milioni za Marekani (takribani Sh. 28 bilioni), kama fidia ya hasara halisi na riba kwa kiwango cha Mahakama (asilimia), kuanzia tarehe ya hukumu mpaka kumaliza malipo yote.
Kadhalika, alikuwa anaiomba Mahakama iamuru Vodacom imlipe fidia ya hasara ya jumla kadri Mahakama itakavyotathmini, gharama za kesi na nafuu nyingine kadri mahakama itakavyoona inafaa.
Vodacom kupitia wakili wake, Gaspar Nyika, Julai 9, 2024 kufuatia wito wa uliyoitaka kufika mahakamani na kuwasilisha utetezi wake wa maandishi, iliwasilisha maelezo yake ya utetezi wa maandishi.
Katika maelezo hayo ya utetezi, kampuni hiyo ilikana tuhuma zote zilizoelekezwa kwake na Kabendera kuhusu ushiriki wake kufanikisha hicho alichokiita kutekwa kwake na ikamtaka mwandishi huyo, kuthibitisha tuhuma hizo.
Sambamba na maelezo hayo, Vodacom iliibua pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo ikiiomba Mahakama iitupilie mbali kesi hiyo bila kuisikiliza, kwa madai kuwa haikuwa na mamlaka ya kuisikiliza kwa kuwa ilifunguliwa nje ya muda uliowekwa kisheria.
Tarehe 9 Septemba 2024, Jaji Salma Maghimba katika uamuzi wake alikubaliana na hoja ya pingamizi la Vodacom, kuwa kesi hiyo iko mahakamani isivyo halali kwa kuwa imefunguliwa nje ya muda uliowekwa katika sheria.
Jaji Maghimbi alisema sheria inaelekeza kesi za aina hiyo zinapaswa kufunguliwa mahakamani ndani ya muda wa miaka mitatu tangu kutokea kwa jambo linalolalamikiwa, lakini Kabendera alifungua kesi hiyo baada ya muda huo kupitia.
Kabendera alitiwa mbaroni na askari polisi nyumbani kwake, Mbweni jijini Dar es Salaam Julai 29, 2019 na kushikiliwa kwa siku kadhaa, kisha akafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.
Kesi hiyo ilimalizika kwa utaratibu wa majadiliano na makubaliano ya kukiri makosa baina yake na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), unaojulikana kisheria kama plea bargaining.
Aliachiliwa huru Februari 24, 2020 baada ya kulipa fidia ya hasara aliyodaiwa kusababisha kwa kukwepa kodi zaidi ya Sh. 173 milioni na faini aliyoamuriwa na Mahakama baada ya kumtia hatiani kwa kukiri makosa yake kulingana na majadiliano na makubaliano hayo na DPP.
Katikati ya mwaka huu, ikiwa ni miaka mitano baada ya kukamatwa na miaka minne baada ya kesi yake hiyo ya uhujumu uchumi kumalizika, ndipo Kabendera akafungau kesi hiyo ya madai ya fidia dhidi ya Vodacom.
Katika kesi hiyo, Kabendera alieleza kuwa simu yake, ilianza kupoteza mawasiliano na kumfanya ashindwe kuwasiliana, kabla ya tukio la kukamatwa kwake.
Pia, Kabendera alieleza juhudi alizofanya kujua chanzo cha hali hiyo, kwa kufanya mawasiliano na mwakilishi wa huduma kwa wateja na hata kutembelea ofisi za kampuni hiyo, lakini hakupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, hali hiyo ilianza Julai 27, 2019, saa 9:00 alasiri alipoiwasha simu yake ambayo alikuwa ameizima tangu jana yake usiku na kwamba ndipo alipobaimi kuwa haikuwa na mtandao.
Hivyo, aliazima simu nyingine akampigia mtoa huduma kwa mteja, kujua mazingira yaliyosababisha kumkatia huduma katika simu yake bila kumjulisha kwanza.
Mwakilishi wa huduma kwa wateja wa Vodacom alimweleza kuwa namba yake ya simu ya Vodacom (+255767456796), ilikuwa na changamoto za kiufundi ambayo ilimhitaji kutoa taarifa katika kituo cha huduma kwa wateja cha karibu kilichopo Tegeta.
Kabendera alimtaka mwakilishi huyo kuelezea tatizo ni nini kabla ya kwenda huko kituoni, lakini mwakilishi huyo alikataa akidai ni suala nyeti ambalo linamtaka aende binafsi kituoni hapo.
Hata hivyo (Kabendera alisita kwenda kituo cha huduma kwa wateja), kwa kuwa kulikuwa kina matukio kadhaa ya watu kutekwa ama kutiwa mbaroni walipokuwa wakitembelea kituo cha huduma kwa wateja tangu mwaka 2016.
Kabendera alidai, Jumatatu ya tarehe 29 Julai 2019 saa 4:00 asubuhi, alipiga tena simu ya huduma kwa wateja akimlalamikia kuwa alikuwa akihitaji kutoa pesa kwenye simu yake hiyo kwa ajili ya kumnunulia dawa mama yake aliyekuwa mgonjwa.
Mwakilishi wa Vodacom aliyemhudumia alimweleza kuwa asubiri kidogo ili amuulize meneja wake, na alirejea dakika chache baadaye na kumweleza kuwa kesi yake ilikuwa nyeti na kwamba ilikuwa juu ya uwezo wao kuitatua badala yake walimshauri atembelee ofisi zao zilizoko Mliman City asubuhi hiyo.
Hata hivyo saa 9:00 alasiri siku hiyo hiyo ya Julai 29, ghafla tu simu yake ilianza kufanya kazi, kisha alipoigiwa simu na mwakilishi wa Vodacom, ambaye alimtaka (Kabendera), amwelezee tatizo lake na baada ya Kabendera kumuelezea kwa takribani dakika tatu, alikata simu akiahidi kumpigia baadaye kidogo.
Baada ya takribani dakika tatu Kabendera alipokea simu iliyopigwa kutoka huduma kwa wateja Vodacom, ambayo aliipokea akabaini kuwa ilikuwa ni sauti ya mwanamume, ambaye alimtaka Kabendera aeleze mahali alikokuwa na kwamba simu hiyo ilikuwa ikihanikiza na kukwaruza kama vile ilikuwa inarekodiwa
“Kabla ya simu hiyo kukatwa mteja wetu alimsikia huyo aliyempigia simu hiyo akinong’ona kuwa alikuwa nyumbani kwake na kuongeza kuwa sogea karibu na nyumba yake.” ilisomeka sehemu nyingine ya hati hiyo ya madai, iliyowasilishwa mahakamani katika kesi iliyofutwa.
Kwa mujibu wa hati hiyo, maelezo hayo yalimstua Kabendera, akakimbia sehemu ya juu ya nyumba yake ambako aliweza kuona magari kadhaa ambayo hakuyafahamu, karibu ya nyumba yake
Kisha lilitokea gari lingine aina ya Toyota Alphard lililoegesha mbele ya magari hayo upande wa kulia mwa nyumba yake, halafu wakashuka watu wanne ambao walijitambulisha kuwa maofisa wa polisi, lakini walikataa kutoa utambulisho. Walimpiga pingu kumshikilia kizuizini kwa siku mbili.
Hati hiyo inaendelea kueleza wakati wa mahojiano, maofisa wa polisi walifika katika chumba cha mahojiano wakiwa na karatasi zilizochapishwa kutoka katika kompyuta za akaunti za pesa ya simu na za namba simu alizokuwa amezipiga kwa mwaka mzima.
Hivyo, walimhoji lengo la kila muamala alioufanya kwa mwaka mzima nyuma yake na pia walimhoji uhusiano wake na watu aliokuwa amewasiliana nao miaka kadhaa.
Kabendera analalamika polisi na Serikali walitoa taarifa kadhaa zenye mgogoro kwa umma kuhusiana na ‘kutekwa’ kwake na kwamba walimtuhumu kwa kutokuwa raia na kumkashfu Rais (wa wakati huo), John Magufuli
“Hatimaye alishtakiwa mahakamani kwa makosa ya utakatishaji fedha, uhujumu uchumi na ukwepaji kodi na matokeo yake walimuweka chini ya ulinzi mkali katika mahabusu ya Gereza la Segerea,” inasomeka hati hiyo ya madai, ya kesi iliyofutwa.