Kikapu taifa kuunguruma Dodoma | Mwanaspoti

Shirikisho la Kikapu Tanzania (TBF) limesema timu 16 zinatarajia kushiriki katika mashindano ya Ligi ya Kikapu ya Taifa (NBL) kuanzia Novemba, mwaka huu katika viwanja vya Chinangali mjini Dodoma.

Mwenze Kabinda, katibu mkuu wa TBF ameliambia Mwanaspoti kuwa washindi watakaopatikana watawakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa. 

Alisema timu nne zilizofuzu kucheza nusu fainali mwaka jana zimepewa nafasi ya kwanza ya kushiriki mashindano hayo msimu huu, akizitaja kuwa ni JKT, ABC, Dar City (DSM) na Kisasa Heroes ya Dodoma.

Kabinda alisema timu hizo zitaungana na zingine 12 zitakazowakilisha kanda nane za kitaifa ambazo ni Dar es Salaam, Kaskazini, kati, Magharibi, Nyanda za Juu Kusini, kusini, Kanda ya Ziwa na Zanzibar.

Kwa upande wa wanawake alisema timu 12 zitashiriki  zikiungana na nne zilizofika nusu fainali mwaka jana.

Alitaja timu hizo kuwa ni Vijana Queens ambayo ni bingwa  mtetezi, Pazi Queens (DSM) Don Bosco Pantalene (Dodoma) na Fox Divas (Mara).

Wakati huo huo mwenyekiti wa Kamati ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Tabora, Rogers  Kitenge amesema wamepanga ianze Jumamosi, wiki hii katika Uwanja wa JJ Mkunda Spot Complex.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kitenge alisema katika mchezo wa ufunguzi Mboka Kings itacheza na Urambo Sixers.

Alisema ligi hiyo itaendelea Jumapili kwenye Uwanja wa Nzenga kwa mchezo kati ya Igunga Sniper na Nzega Hawks.

Timu zitakazoshiriki katika mashindano hayo upande wa wanaume ni Mboka Kings, Urambo Sixers, Center, TTC Mempihas, Nzega Hawks na Igunga Snipers, huku upande wa wanawake kukiwa na Mboka Queens, Hot Dadaz, Kazima Heat na Nzenga L.M.

Related Posts