LICHA ya Yanga kuendelea kupata ushindi katika Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini mashabiki wa timu hiyo wanaonekana kutoridhishwa na idadi ya mabao yanayofungwa japo kocha Miguel Gamondi amesisitiza anachoangalia ni pointi tatu pekee.
Mabingwa hao watetezi walianza kuifunga Kagera Sugar 2-0, kisha 1-0 dhidi ya KenGold na ushindi kama huo dhidi ya KMC ambayo msimu uliopita iliichapa 5-0 pale Chamazi.
Wakati mashabiki wa Yanga wakiwa hawana furaha licha ya timu yao kushinda, lakini kuna maajabu 48 ambayo yametokea kwa chama lao hilo linaloongoza kwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara 30.
Ushindi wa juzi wa bao 1-0 ilioupata Yanga dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, umeifanya timu hiyo kuandika rekodi mpya inapocheza nyumbani baada ya kufikisha jumla ya michezo 48 bila kupoteza.
Rekodi hiyo ya Yanga imejitokeza tangu mara ya mwisho ilipofungwa na Azam FC bao 1-0, Aprili 25, 2021 na kuanzia hapo haijapoteza ikicheza nyumbani katika Ligi Kuu. Tena bao hilo lilifungwa katika dakika ya 86 kwa shuti la mbali la Prince Dube ambaye wakati huo alikuwa akichezea Azam kabla ya sasa kutua Jangwani kuiendeleza rekodi ya kutofungwa nyumbani tena.
Hadi sasa Yanga imecheza jumla ya michezo 48 na kati ya hiyo imeshinda 43 na sare tano.
Katika michezo hiyo 48, Yanga imefunga jumla ya mabao 111, huku eneo la kujilinda likiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18 tu.
Hiyo ni rekodi mpya ukiachana na ile ya kucheza mechi 49 mfululizo za Ligi Kuu kwa ujumla bila ya kupoteza iwe nyumbani au ugenini kuanzia Aprili 25, 2021 ilipofungwa na Azam 1-0. Rekodi yao ya mechi 49 ilivunjwa na Ihefu ambayo hivi sasa ni Singida Black Stars kwa kupoteza mabao 2-1, Novemba 29, 2022.
Katika mechi hizo 49 za Ligi Kuu Bara ilizocheza Yanga kabla ya rekodi yake kutibuliwa, ilishinda 39 na kutoka sare 10, huku safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ikifunga jumla ya mabao 83 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 16.
Pia Yanga imeendeleza rekodi ya kufanya vizuri katika michuano mbalimbali kwani haijapoteza mchezo wowote tangu mara ya mwisho ilipotolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Aprili 5, 2024.
Yanga ilitolewa na Mamelodi kwa penalti 3-2, baada ya suluhu ya michezo yote miwili na kuanzia hapo kikosi hicho cha kocha Miguel Gamondi kimecheza jumla ya michezo 23 mfululizo ya mashindano mbalimbali, imeshinda 22 na kutoa sare mmoja.
Sare hiyo ilikuwa ni ya 0-0 dhidi ya JKT Tanzania, mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Aprili 24, mwaka huu.
Kuonyesha ubora wa kikosi hicho cha Gamondi, katika michezo hiyo 23 iliyocheza bila ya kupoteza, imefunga jumla ya mabao 55 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne tu, jambo linaloonyesha wazi inajua kufunga na wakati huohuo ikizuia pia.
Akizungumzia kiwango cha timu hiyo kwa sasa, Gamondi amesema Ligi Kuu Bara imeanza kwa ushindani mkubwa ingawa wao kama benchi la ufundi malengo yao ni kuhakikisha wanapata pointi tatu katika kila mchezo, tofauti na wengi wanavyozungumza.
“Kila mchezo ni mgumu na hauwezi kushinda kwa idadi kubwa ya mabao siku zote, ikitokea kufanya hivyo tutafanya ila kwa michezo ya hivi karibuni tulitengeneza nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia, japo tunaendelea kufanyia kazi udhaifu huu,” amesema Gamondi.
Kwa upande wake aliyekuwa kocha wa zamani wa kikosi hicho, Hans van der Pluijm, amesema rekodi ya Yanga kucheza michezo mingi bila ya kupoteza nyumbani inachangiwa na ubora na uzoefu wa wachezaji waliopo kwenye timu hiyo na sio vinginevyo.
“Sio rahisi, kwa sababu ushindani ni mkubwa na kila timu imejipanga, hii inaonyesha ni kwa jinsi gani wana benchi bora la ufundi na viongozi wenye jicho la kutafuta wachezaji ambao leo tunawaona pia wanafika mbali hata katika michuano ya kimataifa,” amesema Pluijm.
Nyota wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila amesisitiza anachokiona katika timu hiyo kuwa ni ubora wa wachezaji waliopo japokuwa tangu msimu huu umeanza ameona ushindani ukiwa mkubwa tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita, jambo linaloonyesha sio rahisi.
“Pongezi kwao kwa sababu sio rahisi, msimu uliopita walianza kwa kasi kubwa ya kufunga mabao mengi, naona msimu huu imekuwa ni tofauti kutokana na kila timu kujipanga vizuri, nizisihi timu nyingine kuendeleza ushindani huu hata zikikutana zenyewe kwa zenyewe,” amesema Lunyamila.