Madereva wasota kujaza gesi kwenye vyombo vya moto

Dar es Salaam. Wakati watumiaji wa gesi asilia kwenye vyombo vya moto wakieleza kukesha kwenye vituo vya kujaza gesi kusubiri huduma, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeeleza mkakati wa kukabiliana na hali hiyo.

TPDC imesema itaingiza nchini vituo jongefu vya kujaza gesi kwenye magari (mobile CNG station).

Changamoto iliyojitokeza jana kwenye vituo vya Ubungo na Tazara imeelezwa inatokana na Kituo cha TAQA Dalbin, kilichopo Barabara ya Nyerere kupata hitilafu ya umeme kwenye mfumo hivyo kuathiri uendeshaji wa kituo hicho.

Kwenye kituo cha Tazara jijini Dar es Salaam, kulikuwa na msururu wa magari na bajaji kuanzia kituoni hadi kuelekea kwenye mataa ya Tazara (umbali wa mita 400).

Baadhi ya madereva waliokuwa wakisubiri kujaziwa gesi leo Oktoba Mosi, 2024 wamesema walikesha kituoni hapo.

“Nipo hapa tangu saa tisa alasiri ya jana (Septemba 30), mpaka sasa sina uhakika wa kupata huduma kwani mbele yangu kuna bajaji zaidi ya 50,” amesema mmoja wa madereva hao.

Katika kituo cha Ubungo baadhi ya madereva wa bajaji walieleza kadhia ya kukwama kurejesha mikopo kwa ajili ya vyombo hivyo kwa kuwa wameshindwa kufanya kazi.

Wanadai kutumia mafuta ni gharama kwani gesi asilia gharama yake ni Sh6,500 kwa kilo nne ambayo hujaza mara mbili tofauti na mafuta ambayo kwa siku hupaswa kulipia Sh30,000.

Mkurugenzi wa Mkondo wa Chini wa TPDC, Emanuel Gilbert amesema taarifa waliyonayo ni kuwa kituo cha TAQA Dalbin kilipata hitilafu lakini wataalamu wa kituo hicho na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wanalifanyia kazi.

Amesema ili kundokana na kero ya madereva kutumia muda mwingi kusubiri huduma hiyo, wanakamilisha kituo kingine cha kujaza gesi eneo la Sam Nujoma mwishoni mwa mwaka huu.

“Pia kuna wawekezaji binafsi ambao wanaendelea na hatua za awali za kuanza ujenzi wa vituo zaidi, TPDC itaingiza vituo jongefu ifikapo Juni 2025, kwa ujumla tunataraji kuongeza vituo 13 kufikia mwisho wa mwaka wa fedha,” amesema.

Dereva wa bajaji Sadat Shabani amesema pampu za kujaza gesi ni chache wakati idadi ya watumiaji ni wengi.

“Nimekuja saa tisa usiku nikaondoka baada ya kuona foleni ni kubwa, nimerudi saa mbili hadi sasa ni saa sita bado sijapata gesi maana yake nitatumia siku nzima kupata gesi,” amesema.

Dereva Pamphily Germanus mkazi wa Gongo la Mboto amesema kwa zaidi ya saa sita amekaa kituo cha Ubungo kusubiri gesi.

“Kwa siku za kawaida tunatumia saa nne kujaza gesi kwenye bajaji mara mbili kwa siku kila unapokuja unapoteza saa mbili ni muhimu tukawa na watu wengi zaidi wanaotoa huduma hii,” amesema.

Related Posts