Mahakama yatupa ombi la Serikali kesi ya Boni Yai, uamuzi Oktoba 7

Dar es Salaam. Dhamana ya Meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo jijini Dar es Salaam, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai bado ni kitendawili baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuipiga kalenda hadi Oktoba 7, 2024.

Jacob mkazi wa Mbezi Msakuzi, ambaye ni mfanyabiashara na mwanasiasa anakabiliwa na kesi ya uchapishaji taarifa za uwongo kwenye mitandao, ambayo upelelezi wake bado haujakamilika.

Ingawa mashtaka yanayomkabili yana dhamana kisheria, tangu aliposomewa mashtakata Septemba 19, 2024 upande wa Jamhuri umekuwa wakiwasilisha maombi kuizuia.

Uamuzi wa maombi ya Jamhuri kuzuia dhamana ya Jacob ulipangwa kutekwa leo Jumanne Oktoba mosi, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga anayesikiliza kesi hiyo.

Hata hivyo, amepanga kuutoa Oktoba 7. Hii ni mara ya tatu kuahirishwa uamuzi huo kutolewa, ya kwanza ilikuwa Septemba 23 na ya pili Septemba 26.

Baada ya kusomewa mashitaka mara ya kwanza alipofikishwa mahakamani, Jamhuri iliwasilisha maombi mawili, mosi mahakama iamuru atoe nywila (neno la siri) za simu zake na ya akaunti yake ya mtandao wake wa X ili vifanyiwe uchunguzi na mpelelezi.

Pili, uliomba Mahakama izue dhamana yake kwa madai kuwa ni kwa usalama wake, ikidaiwa mshtakiwa alimweleza Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Kinondoni, Davis Msangi kuwa baada ya taarifa alizoandika anajua atatekwa na kuuawa.

Maombi hayo yalipingwa na jopo la mawakili wa Jacob likiongozwa na Peter Kibatala, wakidai hoja hizo hazina mashiko na maombi hayo hayakuwasilishwa kwa mujibu matakwa ya kisheria, hivyo mahakama iyatupilie mbali na badala yake impe dhamana mteja wao.

Mahakama ilipanga kutoa uamuzi wa maombi hayo Septemba 23 lakini hayakutolewa siku hiyo kutokana na Jacob kutokufikishwa mahakamani pamoja na mahabusu wengine ikielezwa ni kutokana na hali ya usalama kutokana na siku hiyo ilikuwa imetangazwa kuwapo maandamano ya amani yaliyopangwa kufanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Hakimu Kiswaga alipanga kutoa uamuzi Septemba 26, lakini kabla ya mahakama kutoa uamuzi huo, Jamhuri iliibua maombi mapya.

Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema waliiomba mahakama waondoe ombi la kumlazimisha mshtakiwa kutoa nywila wakidai liliwasilishwa kimakosa kinyume cha sheria.

Kibatala, akisaidiana na John Mallya na Michael Lugina walipinga ombi hilo ambalo hata hivyo Mahakama ililikubali hivyo likaondolewa mahakamani.

Upande wa Jamhuri uliomba kuwasilisha kiapo cha ziada ombi ambalo lilipingwa na jopo la mawakili wa Jacob wakidai halijafuata matakwa ya kisheria na katika hatua iliyofikiwa ya Mahakama kutoa uamuzi haikubaliki kuwasilishwa kiapo cha ziada ambacho ni ushahidi mwingine.

Mahakama ilishindwa kutoa uamuzi iliokuwa imeuandaa kuhusu maombi ya awali, badala yake iliahirisha kesi hiyo mpaka leo Oktoba mosi kwa ajili ya uamuzi wa ombi jipya la Jamhuri kuhusu kuwasilisha kiapo cha ziada.

Mahakama katika uamuzi leo imekubali pingamizi la upande wa utetezi, ikutupilia mbali kiapo cha ziada cha Jamhuri ikisema kimewasilishwa bila kuomba kibali cha Mahakama.

Hakimu Kiswaga amerejea msimamo uliokwishawekwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa kesi mbalimbali ambao ulitupilia mbali kiapo cha nyongeza kilichowasilishwa na mwombaji bila kuomba na kupata kibali cha Mahakama kwanza.

“Katika shauri hili hakuna ubishi kuwa kiapo cha nyongeza kiliwasilishwa bila kibali cha Mahakama. Kwa hiyo ninaendelea kukiondoa kisiwepo kwenye kumbukumbu za shauri hili,” amesema.

Iwapo ingekubaliwa kuwasilisha kiapo cha ziada, maombi ya Jamhuri ya kuzuia dhamana yangeanza kusikilizwa upya.

Baada ya kukataa kupokea kiapo hicho, ilitarajiwa hakimu angesoma uamuzi wa maombi ya awali ya kuzuia dhamana yaliyopaswa kutolewa Septemba 23.

Hata hivyo, Kiswaga ameahirisha uamuzi huo mpaka Oktoba 7.

Jacob anakabiliwa na mashtaka mawili ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.

Anadaiwa Septemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam alichapisha taarifa za uwongo zikimhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) ikidaiwa alimtuhumu kuhusika na mauaji na kuwapoeza watu.

Katika shitaka la pili, anadaiwa Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam alichapisha taarifa za uwongo akiwahusisha wakuu wa upelelezi wa mikoa na utekaji na mauaji ya watu na kutupa miili yao.

Related Posts