Dar es Salaam. Kwa wanaokunywa kahawa leo ni siku yao maalumu ya kujipongeza kwani dunia inaadhimisha Siku ya Kahawa.
Kila mwaka ifikapo Oktoba mosi dunia huadhimisha Siku ya Kahawa Duniani. Kahawa inayotoka Afrika imekuwa ikisafirishwa hadi kwenye vikombe vya chai za asubuhi za kaya zote duniani kwa zaidi ya miaka 600 sasa.
Mchakato wa kuandaa kahawa kwa matumizi mbalimbali ni mfano mzuri wa mabadiliko makubwa.
Wanadamu wamekuwa wakitayarisha kahawa ili kuitumia katika namna mbalimbali: kama kinywaji, kiburudisho, dawa. Haijalishi unakunywa vipi, kahawa inaweza kukupa nguvu, kukufariji, kuku refreshing, kukuweka macho na hata kukupatanisha na wapendwa wako.
Kulingana na rekodi za kihistoria, asili ya kahawa ni Ethiopia, na uvumbuzi wake barani Afrika unakuja na hadithi yenye kuvutia. Karibu na mwaka 700 kabla ya Kristo, kundi la mbuzi lilianza kuonyesha tabia za ajabu ukiwatazama ni kama wana furaha hivi. Aliyekuwa akiwatunza Kaldi, aligundua kwamba walikua wakila aina fulani ya mbegu nyekundu na alihitimisha kuwa hiyo ilikuwa sababu ya tabia yao. Kaldi aliamua kushiriki uvumbuzi wake na Monk, aliyekuwa alihitaji kitu kitakachomsaidia kubaki macho usiku mzima wakati wa maombi yake. Simulizi hiyo inaeleza kuwa Kaldi alimpa Monk mbegu walizokuwa wakila mbuzi wake na kuwa na furaha na uchangamfu, lakini Monk alizikataa na kuzitupa kwenye moto, hapa ndiyo utamu wa kahawa ulipoanzia, kwani harufu ilitoka hapo baada ya zile mbegu kuungua ilikuwa ya kuvutia.
Kuanzia hapo kahawa ilianza kusafiri kaskazini hadi Yemen katika karne ya 15 ambapo mbegu hizo zilikuwa zikijulikana kama “Mocha.” Baadaye kahawa ikawa kinywaji maarufu nchini Misri, Uajemi na Uturuki ikijulikana kwa jina la ‘divai ya Araby’ na migahawa mikubwa ya kuuza kahawa zikaanza kufunguliwa zikijulikana kama ‘Shule ya wenye busara’.
Baadaye, kwenye nchi za kiarabu kukawa mlango wa kuingia kwa kahawa, na mbegu hizi zikaanzisha kilimo kikubwa cha kahawa nchini India Kusini. Mnamo mwaka 1560, kahawa ilianza kusafiri hadi Ulaya na harakaharaka ikawa maarufu, mpaka Papa Clement VIII alisema kwamba kinywaji hicho lazima kiwe cha kishetani. Alipofanyiwa uchunguzi, alikubali sifa za kinywaji hicho kwa ubatizo na kukitangaza kuwa kinywaji cha Kikristo. Kadiri karne ya 1600 ilivyokuwa ikikamilika na nyumba za kahawa zikianza kuibuka kila mahali barani Ulaya, mbegu hizo ziliandika historia.
Hatimaye, baada ya muda mrefu mwaka 2014, Shirika la Kahawa Duniani lilitangaza Oktoba mosi kuwa Siku ya Kahawa Duniani, tukio la kuadhimisha kahawa kama kinywaji na kuleta mwamko kuhusu matatizo yanayowakabili wakulima wa kahawa.
Dhana kahawa kuwa na kilevi
Pamoja na mafanikio hayo, jijini Makka nchini Saudi Arabia, kinywaji hicho kilipigwa marufuku ikidhani kuwa kinalewesha na kusababisha uvivu miongoni mwa wanaoitumia.
Guiness yakitaja kikombe kikubwa cha kahawa duniani
Kwenye kitabu Rekodi za Guinness za Dunia za mwaka 2012, kikombe kikubwa zaidi cha kahawa kilikuwa na ujazo wa galoni 3,487 sawa na mapipa takriban 83 yenye ujazo wa lita 159 kila moja.
Takwimu za Msingi Tanzania zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeonyesha, mauzo ya zao la kahawa nje ya nchi yameongezeka kutoka Sh349.4 bilioni mwaka 2019 hadi Sh542.6 bilioni mwaka 2023.
Aina ya kahawa inayozalishwa Tanzania
Tanzania inazalisha aina mbili za kahawa, Arabika ambayo inachangia wastani wa asilimia 60.9 na Robusta inayochangia asilimia 39.1. Tanzania inashika nafasi ya nne kati ya nchi 25 zinazozalisha kahawa barani Afrika.
Maeneo ya kilimo cha Arabika nchini Tanzania ni pamoja na Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Iringa, Mbeya, Kigoma, Manyara, Mwanza, Katavi, Mara, Njombe, Songwe, Rukwa, Geita na Ruvuma wakati Robusta inalimwa katika mikoa ya Kagera na Morogoro.
Tanzania ni moja ya nchi tatu duniani ambazo zinazalisha Arabika ya Kolumbiani laini. Colombia na Kenya ni wazalishaji wengine wawili wa kahawa ya ubora huu maalumu, ambao unachangia asilimia 9 ya uzalishaji wa kahawa duniani.
Takriban asilimia 90 ya uzalishaji wa kahawa Tanzania unatoka kwa wakulima wadogo wa kahawa takriban 320,000 wenye wastani wa miti 200 ya kahawa na ukubwa wa shamba wa ekari 0.5 – 2. Asilimia iliyobaki ya kahawa inazalishwa kwenye mashamba makubwa ya kahawa 101 yaliyosajiliwa.
Imeandikwa na Kalunde Jamal kwa msaada wa mtandao