Moshi/Dar. Mara tu baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kuwahukumu kifungo cha maisha gerezani washtakiwa wanne maarufu, ‘waliotumwa na afande’ mjadala umepamba moto, kuhusu yanayetajwa kuwatuma.
Washtakiwa hao wanne, walitiwa hatiani kwa kosa la kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti, mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam, ambaye mahakamani hapo alitambulika kama XY.
Swali la alipo aliyeweatuma limetawala maeneo mbalimbali, hususan mitandaoni na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amejikuta akipigwa maswali naye akijaribu kuyapangua.
Hiyo ni baada ya Gwajima kuposti katika mtandao wake wa X hukumu ya watu hao ambao jana Jumanne, Septemba 30, 2024 walianza maisha mapya gerezani, na kuibua maswali ya wasomaji.
Mbali na kifungo cha maisha gerezani, mahakama hiyo imewaamuru washtakiwa kumlipa binti mwathirika fidia ya Sh1 milioni kila mmoja, sawa ana jumla ya Sh4 milioni. Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Zabibu Mpangule.
Washtakiwa kwenye kesi hiyo walikuwa MT 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo ambaye ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba, ambao kwenye video ya tukio hilo la jina walisikika wakidai wametumwa na afanye hivyo.
Mmoja wa wasomaji kwenue ukurasa wa Waziri Gwajima, @Madinda33090112 aliandika kwenye ujumbe: “Tunashukuru kwa wote tuliochukizwa na lile tukio walau mmetufuta machozi. Watanzania hii ndio haki tunayoililia. Sasa swali, vipi kuhusu afande?” aliuliza na Waziri Gwajima akamjibu:
“Najaribu kuwaza kama wewe, kuwa hawa waliosema wametumwa, wao si ndiyo wangethibitisha huko mahakamani ambako mimi na wewe hatukuwepo? Kumbuka mimi na wewe hatuna mamlaka ya kuingilia shauri la mahakamani…”
“Ila wao hao wahukumiwa ndiyo walikuwa na fursa ya kusema tulitumwa na fulani na ushahidi huu hapa na Mahakama iamue. Hivyo naomba niishie hapa kuheshimu maamuzi ya Mahakama kama tulivyosikia na ambaye hajaridhika nadhani huwa kuna fursa ya rufaa. Ahsante sana,” ameandika Waziri Gwajima.
Baada ya jibu hilo, mchangiaji mwingine @JLogolie11479 akaandika “Afande ni muhimu”, na hapo Waziri Gwajima akajibu: “Hao wahukumiwa sasa ndiyo wakate rufaa waihakikishie Mahakama kuhusu kutumwa kwao. Mimi na wewe wasikilizaji tu na wapokea matokeo, maana wakati wakitumwa, sisi hatukuwepo.”
Mchangiaji mwingine, @Orvinhill akaandika: “Mumsaidie huyo binti sasa kisaikolojia ku recover (kurejea katika hali yake ya kawaida). Sio kazi rahisi lakini jitahidini.”
Waziri Gwajima akamjibu: “Hili linazingatiwa vema kupitia wataalamu wa ustawi wa jamii na wanasaikolojia. Ahsante sana kwa kujali.”
Maswali yaliendelea kuulizwa na @Gibson44178359: “Kwani ukiangalia video? Kwanini mnamlinda yule mama?”
Waziri Gwajima alimjibu akisema: “Ndugu yangu, salaam. Huwa tunapenda kuhukumiana hata pale ambapo ni pa kuongea na kueleweshana kwa haki kuhusu utaratibu.
Hali hii huchangia jamii yetu wenyewe kukwama kwenye kushirikiana katika kuelimishana mambo mbalimbali. Haya mimi naishia hapa kwa leo,” alihitimisha Waziri Gwajima.
Licha ya Gwajima kuwaacha, mjadala na maswali viliendelea, ambapo @JatJackson amesema: “Mpaka hapo tunasema asante umeonyesha uzalendo ila tunaomba juhudi zisiishie kwa yale matukio yaliyovuja mitandaoni na kupata wapaza sauti pekee, haki iwe inatendeka automatically.
Mchangiaji mwingine @julius_magoti yeye amesema: “Bado jamii inashangaa kwa nini aliyewatuma hajafikishwa mahakamani na Jamhuri? Hivyo juhudi kubwa zinatakiwa zielekezwe katika kuhakikisha anapelekwa mahakamani.”
Katika kurasa za Mwananchi za Instagram na X ilipowekwa taarifa ya hukumu, pia wachangiaji wengi walijielekeza kuhoji juu ya huyo anayedaiwa kuwatuma ambaye alikuwa akitajwa na washtakiwa kama afande.
@amanimlele aliandika: “Vipi kuhusu afande aliyewatuma? Kwani yeye hastahili adhabu kama wenzake waliofungwa maisha, na hapa vijana kuna kitu cha kujifunza sana, maana tamaa za muda mchache zinakosti (zinagharimu) maisha yako yote na unaacha familia yako ikiteseka kwa mambo ya kutumwa.”
merrythomas360, alihoji, swali jepesi ni kwamba aliyewatuma yupo wapi? huku arsenilazaro akiandika: “Kama watatumikia kifungo kweli ni jambo jema, wasiwasi wangu ni kwamba rufaa itawarudisha uraiani. Ila kama tajiri aliyewaajiri hawa vijana, (afande) naye angehukumiwa ingekuwa na maana zaidi. Kwa nini aendelee kuwa uraiani wakati aliowaajiri kwa kazi ovu wanatumikia kifungo cha maisha?”
Mwananchi limezungumza na wanasheria juu ya hukumu hiyo na mijadala inayoendelea. Wakili Fulgence Massawe amesema wapelelezi ndio wanojua ukweli nani alihusika, ingawa hajaona hukumu iliyoandikwa kujua washtakiwa walijiteteaje kuhusu mtu aliyedaiwa kuwatuma, kama kweli kuna mtu alikuwa nyuma yao au zilikuwa ni akili zao tu wenyewe.
“Kama kuna mtu aliyewatuma basi naye alipaswa kushtakiwa kwa mujibu wa sheria kwani katika kosa hilo naye anawajibika kama waliohusika. Katika hali ya kawaida, huwezi kutaja afande na kwamba umuombe msamaha afande kama hakuna chochote kinachowaunganisha na huyo afande,” amesema Wakili Massawe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Vijana (AYL), Emmanuel Ukashu amesema aliyewatuma vijana hao naye alipaswa kuunganishwa kwenye kesi hiyo kwa kosa la kula njama za kutenda kosa hilo.
Hata hivyo, Ukashu amesema katika hilo adhabu yake yeye inakuwa tofauti na waliotekeleza kosa hilo kwani yeye atahukumiwa adhabu kwa kosa hilo la kula njama na si kwa kufanya kitendo.
“Lakini pia haizuii hata kama wengine wameshashtakiwa maana na yeye anaweza kufunguliwa kesi yake peke yake kwa kosa hilo la kula njama,” amesema Ukashu.
Wakati shauku ya wananchi ni kujua kipi kinaendelea kwa afande, ni takribani siku 38 zimepita tangu Jeshi la Polisi lilipoueleza umma kuhusu kufanyika uchunguzi dhidi ya ofisa wake, Fatuma Kigondo.
Agosti 24, 2024, taarifa kwa umma iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alieleza uchunguzi wa kina umefanyika na jalada limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP) kuhusu Fatuma Kigondo anayetajwa kuwa ni afande, akidaiwa kuwatuma vijana hao.
“Jeshi la Polisi lingependa kutoa taarifa juu ya Afisa wa Polisi anayetajwa kwa jina la Fatuma Kigondo, kwamba uchunguzi wa kina ulishafanyika ikiwa ni pamoja na kupata maelezo ya watu mbalimbali pamoja na ya kwake na jalada limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka,” alisema Misime.
Leo Jumanne, Oktoba 1, 2024, Mwananchi limemtafuta Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP, Sylvester Mwakitalu kujua nini kinaendelea juu ya jalada hilo lakini simu yake imeita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe haukupata majibu.
Tukio lenyewe lilivyokuwa
Tukio la msichana huyo lilianza kwa kusambaa kwa picha jongefu katika mitandao ya kijamii Agosti 2, 2024 likionyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti binti huyo aliyejitambulisha kuwa mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam.
Katika kipande hicho cha video, binti huyo alishurutishwa kumwomba radhi mtu aliyetajwa kuwa afande na alisikika akifanya hivyo.
Kipande hicho cha video kiliibua mijadala mikali mitandaoni na kwenye vyombo vya habari. Kauli za kulaani zilitoka kila mahali ikiwemo asasi za kiraia zikiitaka Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika wote.