Mume atuhumiwa kumuua mkewe, dada wa kazi kwa kuwanyonga na kuwatoboa macho

Tanga. Polisi Mkoa wa Tanga linamtafuta Alii Bagidai (60),  mkazi wa Barabara ya 4, Wilaya na Jiji la Tanga kwa tuhuma za kumuua mkewe Saira Mohammed (50) na binti wa kazi anayejulikana kwa jina moja Asha (20) kwa kuwanyonga na kamba ya katani shingoni, kisha kuwatoboa macho.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Almachius Mchunguzi jana Jumatatu Septemba 30, 2024 imeeleza tukio hilo limetokea jana saa 1:00 usiku na baada ya mtuhumiwa kufanya kitendo hicho alitoroka.

Kamanda Mchunguzi ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa mahali atakapooneka mtuhumiwa huyo, ili akamatwa na sheria ichukue mkondo wake.

Aidha, amewaasa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, kwani kufanya hivyo ni kinyume na sheria za nchi.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa, Lumumba Allen Shemdoe amesema bado hawafahamu chanzo cha tukio, ila waliokutwa na tukio hilo wote ni wananchi wa mtaa wake.

“Tulipofika eneo la tukio baada ya kuchungulia tukaona mwanamke amelala chini akiwa na kamba shingoni, ila tulipochungulia mbele tukaona mfanyakazi wa kike naye anakamba shingoni, polisi wakaja tukavunja mlango tukakuta wote wamefariki,” amesema Mwenyekiti Shemdoe.

Endelea kufuatilia Mwananchi

Related Posts