Prisons yafufuka Ligi Kuu ikiizima Fountain Gate

Baada ya kusota katika mechi tano mfululizo bila ya ushindi, hatimaye Tanzania Prisons imeona mwezi kwa kuonja pointi tatu za kwanza kwa kuikanda Fountain Gate mabao 3-2. 

Kabla ya mchezo huo, Maafande hao walifululiza matokeo ya sare ya bila kufunga kabla ya kupoteza dhidi ya Namungo bao 1-0 na leo ikicheza nyumbani Sokoine imeibuka na ushindi huo.

Hata hivyo, licha ya kuondoa mzimu uliowasumbua kwa dakika 450, haikuwa kazi ndogo baada ya kutanguliwa kufungwa dakika ya 12 bao la Suleiman Mwalimu, kabla ya kusawazisha kwa penalti iliyofungwa na Nurdin Chona.

Dakika ya 37 pia Wajelajela hao walijikuta wakiokota tena mpira wavuni baada ya Kassim Hamis kuwapatia bao la Pili Fountain Gate na kwenda mapumziko wakiwa mbele dhidi ya wenyeji. 

Kipindi cha pili Prisons iliingia kwa kasi ikilazimisha mashambulizi zaidi na dakika ya 48, Ezekiel Mwashilindi aliisawazishia tena timu yake kabla ya Vedastus Mwihambi kuipatia la tatu dakika ya 50 na kudumu hadi dakika ya 90.

Kocha Mkuu wa Prisons, Mbwana Makata amesema pamoja na uchovu waliokuwa nao, lakini vijana wake walipambana kutafuta matokeo na kupata ushindi wao wa kwanza msimu huu.

Amesema matokeo hayo yanaongeza nguvu na ari ndani na nje ya uwanja kujiandaa na mechi nne zijazo nyumbani kuhakikisha wanaendeleza furaha kwa mashabiki. 

“Mechi ilikuwa ngumu kila mmoja ameona tulitanguliwa tukarejesha tukafungwa tukasawazisha, hatimaye tukapata bao la ushindi. Tunaenda kujipanga upya kusahihisha makosa ili tuendelee na ushindi,” amesema Makata.

Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Mohamed Muya amesema wamepokea kwa huzuni matokeo hayo licha ya kukubaliana nayo na kila mchezaji ataenda kujitathimini alichofanya.

“Kuhusu penalti siwezi kuelezea zaidi kila mmoja ameona, tunakubali matokeo, tunaenda kurekebisha tulipokosea kwa kuwa mpira leo una kushinda, sare au kupoteza,” amesema Muya.

Related Posts