Mbeya/Dar. Siku moja baada ya Mwananchi kuchapicha habari kuhusu kuvunjwa kwa msikiti wenye miaka 198 huko Mbalizi, mkoani Mbeya, mkuu wa mkoa huo, Juma Homera amesema msikiti huo hautavunjwa, huku akitoa maelekezo kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuangalia namna ya kuchepusha barabara hiyo.
Wakati Homera akitoa maelekezo hayo, wadau wengine wamejitokeza kutaka historia ya msikiti huo itunzwe, badala ya kubomolewa, kwani jengo la msikiti limekuwepo kabla ya kujengwa kwa barabara hiyo.
Wakati akieleza hayo, mamlaka za Serikali zimebainisha sifa na vigezo vya kitu au eneo kuhifadhiwa kihistoria, lazima liwe na umri wa zaidi ya miaka 100, hivyo msikiti huo unakidhi kigezo hicho.
Msikiti huo uliodumu kwa miaka 198 tangu ulipojengwa mwaka 1826, umekuwa wa kihistoria na kivutio ambapo mbali na waumini kuutumia kwa ibada, umekuwa kumbukumbu na kuenzi kazi na mchango wa wazee wa zamani.
Hata hivyo, juzi, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, alisema msikiti huo utabomolewa ili kupisha ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Mbalizi hadi Mbeya Mjini.
Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba mosi, 2024, mkuu huyo wa mkoa (RC), amesema katika kikao cha Kamati ya Usalama Mkoa iliyo chini yake, pamoja na mambo mengine, kimesitisha kuvunjwa kwa msikiti huo ili ubaki kama historia.
Amesema licha ya msikiti huo mkongwe kuwa katika eneo la hifadhi ya barabara, tayari Tanroads mkoani humo wameelekezwa kuwakwepa wananchi wa eneo hilo pamoja na msikiti huo.
“Tumesitisha kubomolewa kwa msikiti huo ili ubaki kama historia, Tanroads wameshapewa maelekezo kuwakwepa wananchi wa eneo hilo.
“Ule msikiti mkongwe upo ndani ya barabara na kingo za nyuma zipo mita 17.9 na kule katikati ni 22.5, japo ule unaojengwa ndio upo nje ya mita 30, huu wa zamani utabaki kumbukumbu,” amesema Homera.
Awali, akizungumzia jambo hilo, Mkurugenzi wa Makumbusho na Malikale, Makumbusho ya Taifa Tanzania, Adelaide Sallema amesema wanalinda sehemu zote za malikale hata kama hazipo kwenye orodha yao kwa asilimia kubwa.
Amesema kwa kutumia Sheria ya Malikale ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho 2022, sura ya 333 inawapa nafasi ya kukagua maeneo kama yametimiza vigezo na jengo ili liitwe malikale, ni lazima liwe na zaidi ya miaka 100.
“Tukishatambua kama sehemu ina malikale, tunakagua na kuliangalia kama limetimiza vigezo vyote na kuwashauri viongozi wetu kwa kuwaeleza kuwa eneo husika linaweza kuwekewa notisi ya Serikali kwa sababu tunasheria zetu za kulinda malikale,” amesema Sallema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Emmanuel Mbwilo amesema baada ya taarifa za msikiti huo mkongwe kusambaa, walipigiwa simu na Taasisi Urithi wa Ukombozi wa Afrika ambao wamehitaji taarifa na ushahidi kuhusu msikiti huo.
“Waliniuliza kuhusu ushahidi, nikawaambia yupo mzee ambaye aliukuta ukiwa na matope, hivyo kilichobaki watakaa na Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) kuamua nini wafanye kulingana na kile kitakachobainika.
“Japo hapa ni vita ya maendeleo na urithi na hata wenye imani yao ni kama wamekubali maendeleo, kwa kuwa wameshajenga msikiti mwingine pembeni, kuna kipande kitakatwa hakina fidia, kwingine ndio panabaki,” amesema Mbwilo.
Mkuu huyo ameongeza kuwa zipo kesi nyingi za namna hiyo, akitolea mfano wa kaburi moja lililopo mkoani Iringa, akibainisha kuwa kutokana na ukongwe wake, baadhi ya miradi ilichepushwa na kuliacha katikati.
“Yapo majengo mengine ya kikoloni japokuwa yenyewe hayapo maeneo ya barabara, mfano kuna Kanisa Katoliki kule Ilembo, lakini kuna kaburi kule Iringa liliachwa katikati, miradi ikachepusha,” amesema.
Baadhi ya watu wametoa maoni yao kuhusu kuvunjwa kwa msikiti huo kupitia akaunti ya Instagram ya Mwananchi. Mmoja wao ni Madaraka Nyerere ameyehoji: “Hiyo mbona historia muhimu. Mbona barabara ya Kawawa (Magomeni) ilisanifiwa na kuacha msikiti?”
Naye Mzena Aron amehoji: “Hakuna namna wakachepusha barabara? Kwanini wavunje msikiti unaobeba historia katika eneo hilo?”