Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza ongezeko la makusanyo ya kodi kwa asilimia 15 kati ya Julai na Septemba 2024 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Pamoja na hilo, imewaita wanaofanya biashara vyumbani kujisajili ili walipe kodi kabla hatua hazijaanza kuchukuliwa.
Kwa mujibu wa TRA, makusanyo ya Julai hadi Septemba mwaka huu ilikiwa na lengo la kukusanya Sh7.42 trilioni lakini imekusanya Sh7.79 trilioni ikiwa ni ongezeko la asimilia 104.9.
Katika kipindi kama hicho mwaka jana, TRA ilikusanya Sh6.57 trilioni.
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba mosi, 2024, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema alipoapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan moja ya maagizo aliyopewa ni kuhakikisha anaziba mianya ya ukwepaji kodi na kukusanya kodi inayotakiwa kutumika nchini.
“TRA imefanikiwa kila mwezi kuvuka lengo walilojiwekea ndani ya kipindi hiki ambapo tulikuwa na ufanisi wa asilimia 104, Agosti ufanisi wa asilimia 104 na Septemba ufanisi uliongezeka hadi kufikia asilimia 105,” amesema Mwenda.
Mwenda amesema katika miezi hiyo mitatu, makusanyo ya Septemba mwaka huu yalikuwa Sh3.18 trilioni, kiwango ambacho hakijawahi kukusanywa tangu TRA ianzishwe licha ya kuwapo mwezi mkubwa wa Desemba ambao uliwahi kuiingizia Serikali Sh3 trilioni.
Amesema vitu vingine vilivyochochea ufanisi huo ni Sera nzuri za uwekezaji na maagizo ya Rais Samia ambayo amekuwa akiyatoa huku akitaka yatekelezwe kupitia kuwafanya walipakodi kuwa wabia na si kuwa madui.
Amewahakikishia walipa kodi kuwa wataendelea kuwasikiliza na kuwafuata walipo na kupitia siku maalumu ya Alhamisi ambayo imetengwa changamoto zao zitaendelea kutatuliwa kwa wakati ili kusaidia biashara ziendelee kuongeza, walipa kodi waongezeke, biashara zisifungwe ila ziongezeke nyingine.
‘Niwahakikishie Tutaweka mazingira sawa ya kufanya biashara kwa kutowapendelea wachache wasilipe kodi wanazostahili kulipa na kutowaonea wanaostahili kulipa kodi, kodi ndiyo zinachangia maendeleo ya nchi yetu,” amesema Mwenda.
Mwenda amesema wapo wengi wanaolipa kodi zao vyema na wapo ambao wamekuwa wakikwamisha jitihada hizo huku akiwataka kuwaunga mkono wenzao katika ulipaji kodi ya Serikali ili kuweka mazingira sawa ya biashara.
Akitolea mfano kwa watu ambao mauzo yao ya mwaka hayazidi Sh11 milioni amesema makadirio yao ya kodi ni Sh250,000 kwa mwaka kiasi ambacho ni kidogo huku akisema kufanya hivi kunaweza kufanya nchi kuwa na uwezo wa kukusanya Sh4 trilioni kwa mwezi.
Kuhusu mnyumbulisho wa makusanyo hayo Kamshina wa walipakodi wakubwa, Michael Muhoja amesema karibu asilimia 43 ya makusanyo ya TRA inatoka kwao.
“Nipende kuwashukuru walipakodi wakubwa wote kwa namna ambayo tumeshirikiana nao kuanzia Julai hadi Septemba, tumefanya kazi kwa pamoja na nawashukuru kwa kuhakikisha kuwa wametoa mchango wao kwa mujibu wa Sheria,” amesema Mboja.