Tuna Sababu ya Ziada Kuandika Historia ya Sokoine – Rais Samia

Na Lilian Lundo – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuna sababu ya ziada za kuandika historia ya Sokoine ikiwa ni miaka 40 tangu atangulie mbele za haki.

Rais Dkt. Samia amesema hayo leo Septemba 30, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akizindua kitabu cha maisha na uongozi wa Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Edward Moringe Sokoine.

“Kitabu hiki kimeweka kumbukumbu ya kina ya maisha na uongozi wa Sokoine, kimewezesha ndugu, jamaa, marafiki na viongozi wenzake kutoa ushuhuda mwingi kuhusu alivyoishi na pia kimetambua mchango wake kwenye ujenzi wa taifa letu,” amesema Mhe. Rais.

Ameendelea kusema kuwa, mapito ya taifa huchukuliwa kwa mitazamo na tafsiri tofauti tofauti, kwa kuangalia historia ya nchi. Aidha, kupitia maisha ya Sokoine, tunapata uelewa na picha kamili zaidi. Hivyo kuna sababu ya ziada za kuandika historia ya Sokoine ikiwa ni miaka 40 tangu atangulie mbele za haki.

“Tunapoandika tunapata pia fursa ya kuangalia mapito ya nchi yetu kwa undani zaidi, kama ambavyo kitabu hiki kimefanya kuhusu Vita vya Kagera dhidi ya mvamizi Nduli Idi Amin, na katika simulizi nyingine nyingi kwenye kitabu,” amefafanua Mhe. Rais

Aidha amesema kuwa, kitabu hicho hakiandiki historia mpya kuhusu Sokoine, kwani Sokoine alijiandikia historia yeye mwenyewe. Hivyo kitabu hicho kinajaribu kuweka pamoja mapito ya kiongozi huyo wakati akijiandikia historia yake.

“Kupitia kitabu hiki, tunapata fursa ya kumfahamu Sokoine kupitia maisha yake binafsi tangu alipozaliwa hadi kushika madaraka makubwa ya uongozi nchini, akiwa kama kijana wa Kimasai aliyedumisha na kuheshimu tamaduni na mila za jamii yake,” amefafanua Mhe. Rais.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango amemuomba Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwawezesha viongozi wastaafu, fedha na rasimali watu, ili waandike tawasifu zao wakiwa hai.

“Uandishi wa tawasifu baada ya kiongozi kufariki, ni mgumu sana, na unatokana na ukweli kwamba, baadhi ya taarifa binafsi zisizoandikwa sio rahisi wengine kuzifahamu. Kwa hiyo Mhe. Rais, ninawaomba viongozi ambao Mungu amewaruzuku uhai hadi sasa , wajitahidi kuandika kitabu cha tawasifu wangali hai,” amesema Mhe. Dkt. Mpango.

“Mhe. Rais ninaomba serikali yako ione uwezakano wa kuwawezesha viongozi wetu wastaafu, fedha na rasimali watu, ili waweze kufanya kazi ya kuandika tawasifu zao,” amesema Dkt. Mpango

Related Posts