Ulinzi umegeuka nguzo muhimu Simba, Yanga

Uimara wa safu za ulinzi ulioonyeshwa na Simba na Yanga katika mechi za mwanzo za msimu unaashiria ushindani mkubwa ambao utakuwepo baina ya timu hizo mbili katika mashindano mbalimbali ambayo zinashiriki.

Tofauti na mechi za mwanzo za msimu uliopita, safari hii kila timu inaonekana kuwa imara zaidi katika eneo hilo na hilo linathibitishwa na takwimu za ulinzi kwa michezo ambayo kila moja imecheza hadi sasa.

Yanga imeongeza kidogo uimara iliokuwa nao msimu uliopita ambapo hadi sasa imeruhusu bao moja tu katika mechi zote tisa za mashindano ambazo imecheza, mbili katika ngao ya jamii, nne katika Ligi ya Mabingwa Afrika na tatu katika Ligi Kuu.

Msimu uliopita katika mechi tisa za mwanzo, Yanga iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja ambapo ilikuwa ni dhidi ya Zalan FC katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo ilipata ushindi wa mabao 5-1.

Mabadiliko makubwa zaidi kwa safu ya ulinzi yanaonekana kuwa upande wa Simba ambayo katika mechi nane ilizocheza hadi sasa, imeruhusu mabao machache kulinganisha na mechi nane za mwanzo msimu uliopita.

Katika msimu huo, Yanga ilimaliza ikiwa imefungwa mabao 14 katika Ligi Kuu na ilimaliza kwa kutwaa ubingwa wa ligi na pia kutwaa taji la Shirikisho la CRDB.

Kuna badiliko moja katika safu ya ulinzi ya Yanga ambalo linahusu nafasi ya beki wa kushoto ambapo kwa sasa anacheza Chadrack Boka tofauti na msimu uliopita ambapo alikuwa anacheza Joyce Lomalisa.

Wachezaji wengine wanne waliounda safu ya ulinzi ya Yanga hawajabadilika ambao ni Djigui Diarra, Dickson Job, Ibrahim Bacca na Yao Attohoula.

Hadi sasa, Simba imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu ambapo ilifungwa bao moja katika Ngao ya Jamii na lingine kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Msimu uliopita, katika mechi nane za mwanzo za mashindano tofauti, Simba ilifungwa mabao sita ambapo yote ilikuwa ni katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ni msimu ambao haukuwa mzuri kwa Simba kwani ilimaliza ikiwa imeruhusu idadi kubwa ya mabao katika Ligi Kuu ambapo nyavu zake zilitikiswa mara 25.

Wachezaji wawili wapya wameingia katika safu ya ulinzi ya Simba msimu huu ambao ni beki Abdulrazack Hamza na kipa Moussa Camara ambao msimu uliopita walikuwa wakicheza Henock Inonga na Aisha Manula.

Eneo la ushambuliaji linaonekana kuendeleza kile ambacho kila timu ilianza nacho msimu uliopita.

Yanga hadi sasa imefunga mabao 26 katika mechi tisa wakati msimu uliopita ilifunga mabao 23.

Simba hadi sasa imepachika mabao 14 katika mechi nane msimu huu wakati msimu uliopita katika mechi nane ilifumania nyavu mara 11.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema anafurahishwa na ubora wa safu yake ya ulinzi msimu huu na anaamini inachangia kuipa timu mwenendo mzuri.

“Napenda kuona kinachofanywa na safu yangu ya ulinzi lakini timu kiujumla. Tunahitaji kuwa na muendelezo mzuri wa hiki ambacho inakifanya na naamini kuna mambo mazuri zaidi yanakuja,” alisema Davids.

Beki wa Yanga, Dickson Job alisema kuwa kufanya kwao vizuri ni zao la juhudi za timu nzima.

“Siku hizi mpira umebadilika na jukumu la kuzuia na kushambulia ni la timu nzima. Timu yetu inacheza katika namna ambayo kila mmoja anawajibika katika nyakati hizo mbili na ndio maana tunafanya vizuri,” alisema Job.

Related Posts