Wanawake Stendi ya Magufuli walia kunyanyaswa, kuombwa rushwa

Dar es Salaam.  Wanawake wanaofanya kazi za ujasiriamali na usafirishaji katika kituo kikuu cha mabasi Magufuli, jijini Dar es Salaam wameeleza magumu wanayokumbana nayo kituoni hapo.

Wametaja unyanyaswaji kijinsia, kuombwa rushwa ya ngono, kudharauliwa kuwa ni miongoni mwa changamoto zinazowapa wakati mgumu katika kazi zao.

Wanawake hao ambao ni mama lishe, wabeba mizigo, makarani na wauza vinywaji wamesema changamoto hizo zinawakatisha tamaa kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Wamesema hayo katika warsha iliyoandaliwa na Umoja wa Wasafirishaji Abiria Mikoani (UWAM) iliyowakutanisha makumi ya wanawake hao, jana Jumatatu Septemba 30, 2024 katika kituo hicho, hafla iliyohudhuriwa na baadhi ya viongozi wa kituo na wilaya.

Miongoni mwa wafanyakazi hao, Yolanda Moshilo, amesema amewahi kupigana na mwanaume aliyemshika bila ridhaa yake, kwani anaamini ni sehemu ya udhalilishaji.

“Unaweza ukapita mtu akakushika matiti makusudi, hivyo unabidi uwe mkali sana ili watambue ulivyo, kesho wasirudie. Unajua kukaa na wanaume ni vita, wakati mwingine unawalamba makofi ili wajue hupendi.

“Ukijiendekeza watakuzoea vibaya, kwani kukaa sehemu yenye watu wengi kama hii hazikosekani changamoto, hivyo lazima uwe mkali na mwenye msimamo,” amesema.

Aidha, changamoto ya maji vyooni pia ameitaja, kwani ni muhimu kwao kutokana na uwepo wa watumiaji wengi, huku uongozi wa kituo hicho ukisema unaendelea na utatuzi wa changamoto hizo.

Naye Diana Mwakeja ambaye ni karani, amesema lazima kuwe na eneo maalumu kwa ajili ya wanawake wanapokuwa katika siku za hedhi tofauti na vyoo ambavyo kwa sasa vinatumiwa na watu wengi.

Akizungumzia kunyanyaswa kijinsia, amesema: “Mimi binafsi sijawahi kushikwa. Mimi ni mkali sana, ila si jambo zuri. Nawaomba wenye tabia hizi waache, kwani zinadhalilisha sana.”

Mwingine, Jennifer Kimario, ambaye ni karani wa magari yaendayo mikoani amesema kushikwashikwa bila ridhaa ni jambo linalomuumiza.

“Anakuja mtu anakushika na kukuparamia sehemu ya mwili ambayo hujamruhusu, kisa tu ni mwanamke. Inaumiza ukilinganisha wewe ni mtu mzima na ni mama wa watoto.

“Pia rushwa ya ngono nakumbuka kuna dada alikuja kuomba kazi nikamuelekeza pa kwenda, huwezi kuamini aliombwa rushwa ya ngono nikamwambia acha asimpe mwili wake, akaondoka hadi leo hajaja,” ameeleza.

Amesema anataka  hali hiyo ikomeshwe mara moja kwa kutoa rai kwa wanawake wenzake wanaopitia kadhia hiyo waripoti kwa vyombo husika.

Mwenyekiti wa umoja huo wa UWAM, Peter Ndengerio amesema suala la vyoo linapaswa kuongezwa, kwani watumiaji ni wengi hususani mama lishe wanaofanya kazi eneo la chini.

Pia amesema wanawake na wasichana wanaotelekezwa stendi hapo wanatumiwa kingono na baadhi ya wanaume wenye tamaa, huku akisisitiza wawe na tabia ya kuwaripoti wanapokumbana na changamoto hiyo.

“Kuhusu rushwa ya ngono humu ndani inahesabika kama ‘interview ya kazi’ kutokana na baadhi ya wenye mamlaka ya kuunganisha na kutoa kazi kuwaomba walale na wanawake wenye uhitaji wa kazi.

“Huwa wanaoripotiwa na wanashtakiwa, ili kutatua hili tuliamua kukutana na wamiliki wa mabasi kuzungumzia haya, kwa sasa watu wanaelimika tofauti na ilivyokuwa mwanzo,” amesema Ndengerio na kuongeza:

“Tunalenga kutatua tabia hizi hapa kituoni, mfano tulishatengeneza jukwaa la haki za wanawake na watoto maalumu kwa utetezi linawajumbe 30.”

Katika kutatua changamoto hizo, meneja wa kituo hicho, Isaac Kasebo, amesema wale wote wanaohusika na unyanyasaji wakibanika wanachukuliwa hatua kulingana na sheria.

AKuhusu suala la maji kukatika, amesema tayari mkakati wa kuchimba kisima umeanza, ili kupambana na usumbufu wa kukosekana maji pale yanapokatika.

Amesema kuhusu kuwa na maeneo ya kubadilisha mavazi katika siku za hedhi, amesema tayari mchakato umeanza, ili kurekebisbwa kwani kituo hicho kinaendelea kujengwa.

“Kituo hiki bado ni endelevu, hakijakamilika, mkandarasi anaendelea hivyo kuna maeneo mazuri ambayo wanawake watakuwa wanayatumia,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Tarafa ya Kibamba, Beatrice Mbawala amesema magumu hayo, ikiwemo kutojaliwa maeneo ya kazi na rushwa ya ngono wanapaswa kuripoti serikalini ili hatua za kisheria zichukuliwe.

“Rushwa haikubaliki, tutachunguza ili watakaobainika watakumbwa na mkono wa sheria. Pia, tumekuwa tukifanya operesheni ya mara kwa mara kubaini watoto waliotelekezwa tunawaombea vibali wanarudi makwao,” ameeleza.

Warsha hiyo ni sehemu ya mradi wa haki za wanawake na watoto katika sekta ya usafirishajia abiria katika kituo cha Magufuli wenye kaulimbiu isemayo ‘Sekta ya usafirishaji inayozingatia haki na usawa wa kijinsia’.

Related Posts