Wazee walilia sheria maalumu, malipo ya pensheni

Dar/Mikoani. Mahitaji ya sheria mahsusi ya wazee, ukosefu wa matibabu kwa wazee na ucheleweshaji wa mafao ya uzeeni, ni miongoni mwa kero zilizotajwa katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani leo Oktoba mosi, 2024.

Siku hiyo inaadhimisha kila Oktoba mosi, ili kukumbuka historia ya Desemba 14 mwaka 1990 ambapo Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia Azimio Namba 45/106 ulitenga siku hiyo kwa lengo la kuijengea jamii uelewa na kupewa hamasa kuhusu kulinda haki, ustawi na maslahi ya wazee. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Tuimarishe huduma kwa wazee, wazeeke kwa heshima.”

Tayari Serikali imesema iko mbioni kutunga sheria ya wazee.

Akizungumzia maadhimisho hayo leo jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), Suzan Lyimo amesema kukosekana kwa sheria ya kulinda maslahi ya wazee nchini ni sababu ya kundi hilo kuendelea kupitia changamoto mbalimbali za manyanyaso, ikiwemo kukosa viti vya kukalia kwenye usafiri wa umma.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kukosa huduma bora na bure za afya, kutokulipwa pensheni kwa wakati kwa wastaafu na hata kama hawakuajiriwa, kukosa makazi vyenye hadhi, na kunyimwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

“Wazee hapa nchini tunaishi hali ya umaskini mkubwa na zaidi ya asilimia 75 huishi vijijini, huku idadi ya wanawake ikiwa ni kubwa zaidi jambo linaloongeza changamoto,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bazecha, Hashim Issa amewataka wazee pamoja na kuendelea kupigania haki zao wasibaki nyuma kuweka mkazo kwenye uchaguzi wa Serikali za Mtaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.

Amesema wazee wanatakiwa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, huku akiwataka kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali na kushinda kwa kishindo.

“Wazee wa Chadema hatutakubali kufanyika hujuma katika maeneo tutakayoshinda kudhulumiwa, tutajua namna ya kupambana kwa kuwa ni raia halali,” amesema.

Kwa upande wa chama cha ACT Wazalendo, kimeitaka Serikali itunge sheria na sera ya hifadhi ya jamii, huku ikitaka pia Serikali kuwaangalia vijana walio chini ya miaka 35 wanaofanya kazi na kupata kipato wachangie fedha Sh20,000 na kuendelea kwenye mfuko huo, ili kuwalea wazee kuanzia umri wa miaka 65.

Akizungumza katika maadhimisho hayo hayo wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu amesema Taifa linahitaji sera ya kuwa na hifadhi ya jamii ili kuwasaidia wazee, kwani hata asilimia 70 ya vijana itakuja kufaidika.

 “Sisi ACT Wazalendo tunaamini hifadhi jamii kwa wote iwe njia bora itakayowezesha kupata pensheni kwa wazee wote, ili wapate kipato cha kuendeshea maisha yao ya kila siku na wapate bima ya afya waweze kuhudumiwa bila ya kujali kipato chao,” amesema Semu.

Amezungumzia kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), Semu amesema umekuwa ni kero kwa wazee na wamekuwa wakicheleweshewa ruzuku zao na wengine wakipunjwa fedha zao.

Meneja wa Shirika la Help Age, Joseph Mbasa amesema wazee wanakabiliwa na changamoto za kiafya na kiuchumi.

“Zaidi ya asilimia 83 ya wazee hawakuwahi kuajiriwa, wengi ni wakulima na wafugaji ambao walikuwa hawana ajira rasmi, hivyo hawapo kwenye mfumo wa pensheni, hawana kiinua mgongo kwa kuwa Serikali haijawahi kuwa na mfumo rasmi wa kuwaingiza kwenye kiinua mgongo,” amesema.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wazee mkoani Mbeya wamesema pamoja na kuitumikia Taifa kwa uzalendo, bado thamani yao ni ndogo, ikilinganishwa na nguvu walizotumia katika utumishi wao.

Raphael Mwasikili, amesema pamoja na ajenda ya Serikali kuwataja wazee kuwapa kipaumbele, lakini waliokuwa watumishi wanaishi maisha magumu kwa kukosa haki zao.

“Mimi ni mstaafu, nilikuwa Wizara ya Afya nikianzia kule hospitali ya Milembe (Dodoma), lakini siridhishwi na malipo ya ziada ya pensheni na hata inapotoka yanakuwa kidogo ambayo hayakidhi mahitaji, hivyo tunaishi maisha magumu,” amesema Mwasikili.

Naye Slivester Lugembe, mkazi wa mjini Maswa amesema wazee wengi wanakosa ushirikiano wa kifamilia au kijamii hasa wanapoishi peke yao baada ya kustaafu au baada ya kupoteza wenzi wao.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis amesema Serikali ipo kwenye mchakato wa kutunga sheria ya wazee itakayoangalia changamoto zote.

“Tunayo sera ya wazee na sasa tupo katika mchakato wa kutunga sheria ya wazee, mchakato utakapokamilika tutaiwasilisha,” amesema alipozungumza kwa simu na Mwananchi.

Akitoa tamko la Serikali kupitia mitandaoni Septemba 30, 2024, Dk Dorothy Gwajima ameitaka jamii hususan wale wote ambao hawajafikia umri rasmi wa uzee, kutambua na kukumbuka kuwa uzee na kuzeeka hauepukiki na kila anayeomba umri mrefu anaombea kufikia uzee, hivyo hawana budi kuwapenda na kuwaheshimu wazee.

Amesema Serikali ipo kwenye hatua za mwisho kukamilisha kuhuisha sera ya wazee.

“Kama ambavyo mmekuwa mkiarifiwa kupitia baraza la ushauri la wazee ambapo, kuhuishwa kwa sera hii ni hatua kuelekea kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za kundi hili ambalo ni tunu ya Taifa letu,” amesema.

Imeandikwa na Tuzo Mapunda, Samwel Mwanga na Pamela Chilongola.

Related Posts