Aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba afikisha siku 681 akiwa rumande

Dar es saalam. Aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya Simba Sport Club, Muharami Sultani (40) na wenzake, wanaendelea kusota rumande kwa siku 681 hadi sasa kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Sultan na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwemo ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 34.89 pamoja na kutakatisha fedha.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, Novemba 21, 2022 na kusomewa mashtaka yao.

Hata hivyo, tangu wafikishwe mahakamani hapo siku hiyo, hadi leo Jumanne Oktoba 2, 2024, washtakiwa hao wamefikisha siku 681, sawa na mwaka mmoja na miezi 10 na siku 11, wakiwa rumande kutokana upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.

Licha ya upelelezi wa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 71/2022 kutokukamilika, pia washtakiwa hao wanaendelea kusota rumande, kutokana na mashtaka yanayowakabili, hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Pia, mashtaka ya kutakatisha fedha hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, leo Jumatano wakili wa Serikali Frank Rimoy ameieleza mahakama hiyo, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea, hivyo Serikali inaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mkazi Mkuu anayesikiliza shauri hilo, Aaron Lyamuya, aliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 15, 2024 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wapo rumande kutoka kesi hiyo kutokuwa na dhamana.

Kesi hiyo imesikilizwa kwa njia ya video huku washtakiwa wakiwa rumande.

Septemba 02, 2024, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama hiyo jalada la kesi hiyo limepelekwa Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kufanyiwa kazi.

Mbali na Sultani, washtakiwa wengine ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zubery Seif; Said Matwiko mkazi Magole; Maulid Mzungu maarufu mbonde (54) mkazi wa Kisemvule ambaye ana undugu na mtuhumiwa Muharami.

Wengine ni John John, maarufu Chipanda (40) mkazi wa Kitunda ambaye kazi yake ilikuwa ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy pamoja na Sarah Joseph.

Awali, washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano, lakini Septemba 23, 2023 Mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) aliwabadilishia hati ya mashtaka kwa kuwaongezea mashtaka matatu likiwemo la kutakatisha fedha na kisha kuwasomea upya mashtaka yao.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni kuongoza genge la uhalifu shtaka linalowakabiliwa watu wote ambapo Inadaiwa tarehe tofauti kati ya mwaka 2016 na Novemba 4, 2022 maeneo tofauti na ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride.

Vilevile, Oktoba 27, 2022 katika eneo la Kivule Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 27.10.

Related Posts