Anayedaiwa kuchukuliwa na askari kwa mahojiano akutwa ameuawa Zanzibar

“Mwanangu ameuawa, kifo cha kikatili naomba haki itendeke waliofanya hivi wachunguzwe, ni kweli kifo kipo lakini sio cha namna hii…”

Hii ni kauli ya Saada Ramadhan Mwendwa mama mzazi wa Ramadhan Idd Shaaban (48) akianza kusimulia jinsi mwanaye alivyochukuliwa na watu waliojitambulisha ni askari wakidai wanakwenda kufanya mahojiano naye lakini aliokotwa akiwa amefariki dunia eneo la Mbuzini Kijichi Unguja.

Kwa kipindi cha hivi karibuni matukio ya watu kutekwa, kupigwa, kuumizwa na kuuawa yameshika kasi.

Kwa tukio la karibuni zaidi ni lile la Mjumbe wa Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Ali Kibao ambaye alichukuliwa kwenye gari Septemba 6, 2024 akitoka Dar es Salaam kwenda Tanga na mwili wake uliokotwa Ununio uso wake ukiwa umeharibika kiasi cha kutotambulika.

Akisumulia mama huyo huku akitokwa na machozi, Saada ametumia fursa hiyo kumuomba Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuchunguza tukio hilo na waliofanya hivyo wachukuliwe hatua.

Akisimulia mkasa huo nyumbani kwake Chumbuni Oktoba 2, 2024 Saada amesema mwanaye alichukuliwa Septemba 24, 2024 saa 12:00 jioni lakini mwili wake uliokotwa kesho yake Septemba 25 ukiwa umeunguzwa, jicho moja limetobolewa na ulimi umetoka nje ambapo uchunguzi wa polisi ulieleza kuwa ameuawa.

“Siku hiyo mwanangu alikwenda kutembea jioni eneo la Amani Baa, saa 12:00 za jioni walikuja vijana watano wakamfuata alipokuwa amekaa na kumuita kwa jina wakasema wana shida naye waende nje wakazungumze wakidai wao ni askari na wana RB wanamtafuta,. 

“Walipanda naye kwenye gari wakamwambia wanampeleka polisi Mwanakwerekwe lakini walipofika walipitiliza. Saada anasema mwanaye alikuwa na rafiki yake ambaye aliongozana naye kwenda kituo cha polisi ila baada ya kupitiliza alipohoji mbona wamepita walimshusha.

“Walichokifanya ndio hicho kilichotokea, wamempiga mwanangu wamemuunguza moto kwa shoti za umeme na kumtoboa jicho moja la kulia,” amesimulia akieleza kifo cha mwanaye wa kwanza ambaye ameacha mjane na watoto wanne.

Anasema usiku wa siku hiyo mke wake Shaaban alipiga simu baada ya kuona mumewe hajarejea lakini kuna mtu alipokea simu hiyo akasema asiwe na wasiwasi bado anahojiwa na askari akimaliza atarejea nyumbani.

Baada ya kuambiwa hivyo, alitulia lakini kadri muda ilivyoendelea akawa anaingiwa zaidi na wasiwawasi ndipo alinipigia mimi simu akisema kuna muda alimpigia askari wakasema bado wapo naye lakini mpaka sasa hajarejea.

“Baadaye mimi nilipiga simu ikawa haipatikani nikaanza kumtumia meseji, mwanangu upo wapi mbona hujarudi baba, simu haipatikani nikajua ujumbe unaingia kumbe matokeo yake wameshampiga na kumfanyia ukatili huo,” amesema.

Amesema walipoamka asubuhi Septemba 25 walienda kutoa taarifa katika vituo vitatu vya polisi.

Hata hivyo, amesema anashukuru polisi kwani walionesha jitihada za kupiga simu katika vituo vingi kuulizia iwapo kuna mtu wa namna hiyo lakini majibu yalikuwa hapana.

Akiendelea kusimulia, Saada amesema ulipofika mchana alipigiwa simu na mwanawe mkubwa kuwa kuna maiti imeokotwa katika njia ya Mbuzini Kijichi akiwa na vitambulisho na limeonekana kuna jina la Ramadhani Iddi na walipokwenda katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Mnazi Mmoja wakakuta ni yeye.

“Mdomo ulikuwa wazi, jicho limetumbuliwa na mwili wote umechomwa chomwa, ila niliwaambia wanangu tufanye utaratibu kuchukua maiti,” amesema.

“Kwa kweli kilichotokea kwa mwanangu naomba sana, serikali yangu ni sikivu ya Zanzibar na inatupenda wananchi wanyonge, kwa hili nataka isikie kilio changu waliofanya ukatili huu aliyefanya ukatili huu wapatikane haki itendeke,” amesema na kuongeza.

“Mwanagu kaonewa…, kapata mateso ndani ya nafsi yake, kwasababu unapotiwa moto kila mtu anajua, kama ni kifo kila mtu atakufa lakini sio kwa kifo kile, naomba serikali ichukue hatua haina uonevu watu wote ni watu wake, tumeumia familia hatuna pa kulilia serikai ina mkono mrefu itawapata waliofanya kitendo hiki sheria ni kwa watu wote,” amesisitiza.

Saada amesema ameshakuwa na woga hata kwa watoto wake wengine kwasababu hajui kilichofanywa mwanaye kuuawa.

“Sasa sijui kama litaishia kwa Ramadhan au mimi mwenyewe au watoto wangu wengine hadi wajukuu zangu wangu kwakweli tunakosa amani.”

Mama mdogo wa marehemu, Yunes Kitarao amesema jambo hilo lnawasikitisha na kuwaumiza kwanini auawe kwa ukatili wa namna ile.

“Kwanini mtu atekwe, anaambiwa anachukuliwa na askari na wanasema yupo katika mikono salama watamrudisha na kwanini hakurudishwa akiwa mzima, dhamira hiyo imeniumiza sana, mtoto wa dada yangu, sijawahi kusikia amegombana wala kutukana na mtu,” amesema Yunes.

Amesema mambo hayo yamekuwa yakitendeka maeneo mengine sasa na Zanzibar yameanza.

“Haya yanayotukuta ni makubwa, tunachokiomba hawa watu wakamatwe mbona majambazi yanakamatwa, liwe fundisho, bila kufanya hivyo hili jambo litaendelea hata kama sio kwa familia hii lakini kwa wananchi wengine,” amesema huku akipeleka kilio hicho kwa viongozi wakuu wa nchi.

Mjomba wa marehemu ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema kinachowasikitisha zaidi watu hao kujitambulisha wametoka kwenye vikosi na simu ilipopigwa wakajibiwa yupo kwenye mikono salama halafu wakaokota maiti.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Mchomvu bila kufafanua zaidi amesema wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo na ukikamilika zitatolewa taarifa zaidi.

“Tukio hilo lipo uchunguzi bado unaendelea, tukikamilisha tutaeleza zaidi,” amesema Mchomvu.

Related Posts