Masasi. Diwani wa Chiwale (CCM), wilayani Masasi, Yusuph Mataula amejikuta mikononi mwa vyombo vya dola akitakiwa kusaidia uchunguzi katika sakata la ubadhirifu wa Sh139 milioni.
Fedha hizo ni malipo yaliyopaswa kufanywa kwa wakulima wa korosho wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Nanyindwa Amcos katika msimu wa 2016/17.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ametoa maagizo hayo leo Jumatano, Oktoba 2, 2024, alipohutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Chiwale wilayani Masasi, Mtwara, baada ya kusikiliza kero mbalimbali zinazoathiri maendeleo ya kilimo katika kijiji hicho.
Katika mkutano huo, Bashe alifahamishwa kuwa wakulima kadhaa hawakulipwa kiasi cha Sh139 milioni katika msimu wa 2016/17 hatua iliyosababisha mali za Amcos hiyo ikiwemo trekta na lori kupigwa mnada kwa amri ya mahakama.
“Katika kulipatia ufumbuzi suala hilo, uongozi mpya wa Nanyindwa Amcos, uliamua kulipa Sh10 milioni kila msimu ili kupunguza deni hilo,” mwananchama mmoja wa Amcos hiyo amesema mkutanoni hapo.
Alipotakiwa kuelezea sakata hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Nanyindwa, Anania Kamaghe amesema alikuta taarifa za ubadhirifu huo baada ya kuchaguliwa mwaka huu.
Amesema jitihada za kuokoa mali za chama ziligonga mwamba baada ya kuelezwa uamuzi wa mali kupigwa mnada ulitolewa na mahakama hivyo hakuwa na uwezo kupinga maamuzi ya kisheria.
Alipotakiwa na Waziri Bashe awataje wahusika wa ubadhirifu huo, Kamaghe amesema, “Bodi nzima ya Nanyindwa Amcos, katibu mstaafu wa chama hicho ambaye sasa ni mheshimiwa (diwani) na viongozi wengine 12.”
Diwani huyo alipotakiwa kueleza upotevu wa fedha hizo, amekiri uongozi wake kuhusika na sakata hilo na kubainisha kuwa wajumbe 13 katika uongozi wake walitakiwa kulipa Sh7.4 milioni kufidia fedha hizo za malipo kwa wakulima.
“Siwezi kujua endapo wenzangu wamemaliza kulipa kwa sababu kila mmoja alitakiwa kufanya malipo baada ya kupewa namba ya akaunti. Binafsi, nikipewa muda hadi Jumatatu nitakuwa nimemaliza kulipa sehemu yangu,” amesema.
Baada ya kusikiliza kwa makini, Bashe ameamuru vyombo vya ulinzi na usalama vimchukue ili kusaidia uchunguzi utakaofanikisha kupatikana kwa fedha hizo na wahusika wote wa ubadhirifu huo.
“Fedha zote zipatikane ndani ya wiki na wahusika wajulikane walipo,” amesema, akihimiza madiwani kusimamia Amcos badala ya wenyewe kuwa sehemu ya dhulma.
Katika hatua nyingine, Waziri Bashe ameamuru kukamatwa kwa Afisa Mtendaji wa kijiji mstaafu Hashimu Pahala anayetuhumiwa kushiriki katika kumtapeli shamba la ekari 30, Fatuma Namkumbo licha ya kulipia Sh1.5 milioni na kupatiwa risiti.
Pia, amekiagiza Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi na Mtwara (Mamcu), Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Masasi kuchunguza ubadhirifu unaohusisha mamilioni ya shilingi katika Chama cha Msingi cha Lipumbulu (Amcos).
Katika ubadhirifu huo, taarifa zinaonyesha wakati baadhi ya wakulima hawajalipwa fedha zao baada ya kuuza bidhaa kupitia chama hicho, wengine wamelipwa mara mbili.