Iran yaishambulia Israel kwa makombora ya masafa marefu – DW – 02.10.2024

Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari amesema shambulizi la makombora kiasi 180 lililofanywa na Iran jana Jumanne lilinuia kuwaua maalfu ya raia wa Israel na halikuwa la kawaida na wala halikutarajiwa. Jeshi la Israel pia limelilaani shambulizi hilo likiliita kuwa ongezeko baya na la hatari la machafuko. Hagari amesema Iran na washirika wake wanataka kuingamiza Israel na kutakuwa na matokeo na hatua za kujibu shambulizi hilo.

Rais wa Marekani Joe Biden amesema Marekani inaiunga mkono kikamilifu Israel kufutia shambulizi hilo la makombora ya masafa marefu, akilieleza kuwa limeshindwa na lisilo na tija yoyote. Akizungumza na waandishi habari katika ikulu yake mjini Washington, Biden amesema kuna mazungumzo yanayoendelea kuhusu jinsi Israel itakavyojibu shambulizi la Iran na kwamba athari kwa serikali ya mjini Tehran zitaonekana. Biden amesema atazungumza na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Msemaji wa jeshi la Israel, Daniel Hagari
Msemaji wa jeshi la Israel, Daniel HagariPicha: dts Nachrichtenagentur/IMAGO

Urusi yaikosa Marekani

Wakati huo huo, Urusi inasema sera ya Marekani kuelekea Mashariki ya Kati imeshindwa kabisa. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Urusi Maria Zakharova amesema katika taarifa yake aliyoiandika kwenye mtandao wa Telegram kwamba utawala wa rais Biden umefeli Mashariki ya Kati na kinachoendelea ni tamthilia ya umwagaji damu inayoendelea kushika kasi. Ameongeza kusema kauli zisizoeleweka za ikulu ya Marekani zinaonyesha Marekani iko katika hali ya kutokuwa na msaada kabisa katika kuitafutia ufumbuzi migogoro.

Wizara ya mambo ya nje ya Iran imelitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lichukue hatua za maana kuepusha vitisho dhidi ya amani na usalama wa Mashariki ya Kati.

Baraza la usalama litafanya kikao cha dharura leo Jumatano kujadili ongezeko la machafuko Mashariki ya Kati. Msemaji wa ofisi ya balozi wa Uswiwi katika Umoja wa Mataifa, nchi ambayo inashikilia urais wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, amesema Uswisi imepanga mkutano huo ufanyike saa nne asubuhi saa za New York.

Watu wakijificha kando ya barabara mjini Tel Aviv baada ya king'ora kulia kufuatia shambulizi la Iran
Watu wakijificha kando ya barabara mjini Tel Aviv baada ya king’ora kulia kufuatia shambulizi la IranPicha: Tomer Appelbaum/REUTERS

Soma pia: Israel yapeleka wanajeshi wa ardhini Lebanon

Umoja wa Ulaya umetoa wito mapigano yasitishwe mara moja Mashariki ya Kati. Mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo, Josep Borell ametumia maneno makali kulikosoa shambulizi la Iran dhidi ya Israel akitahadharisha katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa X kuhusu mzunguko wa mashambulizi hatari yanayopitiliza mipaka, akiongeza kuwa Umoja wa Ulaya umejitolea kikamilifu na kwa dhati kuepusha vita vya kikanda.

Lebanon yalifungua anga lake

Wakati haya yakiarifiwa, Lebanon imelifungua anga lake baada ya kulifunga mapema jana Jumanne kufuatia shambulizi la Iran nchini Israel. Waziri wa usafiri wa Lebanon Ali Hamieh amesema baada ya kufuatilia na kutokana na pendekezo la watu wanaojali katika mamlaka ya usafiri wa anga, wanatangaza kufunguliwa tena anga na kwa hivyo kuendelea tena safari za ndege. Awali Hamieh alisema anga lingefungwa kwa muda wa masaa mawili na kwamba wangefanya tathmini baadaye.

Iran imesema mashambulizi haya makubwa dhidi ya Israel ni kujibu kuuliwa kwa viongozi wa wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali ya mjini Tehran, akiwamo kiongozi mkuu wa kundi la Hezbollah nchini Lebanon, Hassan Nasrallah.

Hili ni shambulizi la pili la moja kwa moja la Iran dhidi ya Israel bada ya jingine la makombora na droni mnamo mwezi Aprili kujibu hujuma ya kutokea angani ya Israel katika ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus nchini Syria.

(reuters, afp)

Related Posts