Mashujaa yaipiga mkwara Singida Big Stars

KIWANGO kizuri ilichoanza nacho msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara ikiwa haijapoteza mchezo na kuvuna alama tisa, kimewafanya mabosi wa Mashujaa FC kupata jeuri na kutamba kwamba wanazitaka nafasi nne za juu huku wakiahidi ushindi kwenye mchezo ujao dhidi ya vinara wa ligi hiyo, Singida Black Stars.
Mashujaa inakamata nafasi ya sita ikiwa na alama tisa ikishinda mechi mbili na sare tatu itaikaribisha Singida Black Stars inayoongoza ligi ikiwa na pointi 13 baada ya kushinda mechi nne na sare moja, mtanange huo utapigwa Ijumaa Oktoba 4, mwaka huu saa 10:15 jioni katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Mwenyekiti wa Mashujaa, Abdul Tika, alisema klabu hiyo kwa sasa ina hamasa kubwa kuanzia kwa wachezaji, benchi la ufundi na viongozi na lengo lao ni kumaliza katika nafasi nne za juu na ili kutimiza hayo wanahitaji ushindi katika mchezo ujao dhidi ya Singida.
“Timu inafanya vizuri kwahiyo na sisi tunapambana ili tufanye vizuri zaidi lengo letu na shabaha yetu kubwa toka awali tulivyoanza tuna timu nzuri na tunatarajia tumalize nafasi nne za juu. Ndiyo dhamira yetu na tuko makini siyo tu kwamba tunaongea kama wenzetu,” alisema Tika.
“Tunamuomba Mungu na tunazidi kujipanga vijana wana morali wako vizuri tunashukuru Mungu, mashabiki watusapoti kama unavyojua mashabiki wa Kigoma wanapenda timu yao mechi iliyopita dhidi ya Azam uwanja ulijaa.”
Winga wa timu hiyo, Emmanuel Mtumbuka alisema siri ya kiwango kizuri walichonacho ni umoja na ushirikiano uliopo kati ya wachezaji, benchi la ufundi na viongozi, huku wakijiwekea utaratibu wa kutopoteza katika uwanja wa nyumbani.
“Sisi malengo yetu ni kushinda mechi zetu uwanja wa nyumbani hakuna kingine zaidi ya kutafuta ushindi tu katika mechi inayokuja japokuwa Singida ni timu nzuri na wanaongooza ligi, tunawaheshimu lakini tunakwenda kupambana kutafuta matokeo ya pointi tatu,” alisema Mtumbuka.
“Timu yetu sisi inazunguka (rotation) sana na hii kama mchezaji inakupa morali, kujituma, nguvu ya kupamabana na kuwa na subira kwa sababu unaamini kwamba wakati wako ukifika utacheza. Wachezaji wote kwa ujumla kila mtu anaona ana nafasi kwenye timu,” alisema.

Related Posts