MKUFUNZI wa Shirikisho la Judo la Kimataifa (IJF), Erdan Dogan amewataka makocha na waamuzi wa mchezo huo nchini kuona umuhimu wa kufundisha timu za vijana.
Dogan amekwenda mbali zaidi na kueleza kwamba hakuna nchini iliyofanikiwa katika michezo bila kuwekeza kwenye timu za vijana.
Mkufunzi huyo wa kimataifa kutoka Uturuki amebainisha hayo jana Oktoba Mosi alipokuwa akihitimisha mafunzo ya kimataifa ya makocha na waamuzi wa Judo ya level one yaliyofanyika kwenye kituo cha Olympafrica kilichopo Kibaha Mkuza, mkoani Pwani kwa siku 10.
Miongoni mwa wahitimu 26 wa mafunzo hayo ni nyota wa timu ya taifa, Andrew Thomas, Anangisye Pwele, Abou Mteteko na mwanadada, Asiatu Juma.
Dogan amesema, kuhitimu kwa makocha na waamuzi hao ni mwanzo mzuri wa kuanza kuyafanyia kazi yale waliyofundishwa akisisitiza kuwekeza kwenye timu za vijana.
Mwenyekiti wa Chama cha Judo Tanzania (Jata), Zaid Hamis amesema mafunzo hayo ni chachu ya kuendeleza mchezo wa judo nchini akiwataka wahitimu kuyatumia ipasavyo.
“Yanakwenda kuwaandaa makocha na marefa kufundisha na kuchezesha katika timu za vijana,” amesema Zaidi wakati wa kufungwa mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na kudhaminiwa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kupitia kitengo chake cha misaada (Olympic Solidarity).
Amewasisitiza wahitimu wa mafunzo hayo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kuyatumia vyema kwa kuzalisha wachezaji watakaokwenda kuunda timu za vijana za mchezo huo.
“Naamini maini kufanya hivyo ndivyo kutaufanya mchezo wa judo kusambaa na kuchezwa kote nchini, hivyo ili ufike mbali zaidi ni ninyi makocha na waamuzi kuitumia taaluma mliyoipata kwa vitendo, ” amesema.
Akifunga mafunzo hayo, Makamu wa Rais wa TOC, Henry Tandau amesema Kamati hiyo imekuwa ikiendesha kozi za aina hiyo kwa makocha wa judo, lakini cha kushangaza wahitimu wengi hawafanyii kazi ujuzi wanaoupata kwenye mafunzo husika na kusalia na vyeti nyumbani.
“Hii kozi sio ya kwanza kufanyika hapa nchini, TOC kwa kushirikiana na Chama cha Judo Tanzania chini ya udhamini wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) tumeendesha kozi kadhaa za makocha wa judo, lakini cha ajabu wahitimu hawaufanyii kazi ujuzi wanaopata.
“Safari hii tunahitaji kuona matunda kwa maslahi ys judo,” amesema Tandau.