Dar es Salaam. Wadau wa sekta binafsi na wachumi wametaja mambo yanayokwamisha kujenga vituo vya kujaza gesi asilia kwenye vyombo vya moto, ni kutokuwepo sera na sheria ya kuisukuma sekta hiyo kufanya uwekezaji huo.
Wamesema sekta binafsi huitaji kuwekeza eneo lenye kuipatia faida, hivyo vipo vikwazo vya kikodi ya uingizaji wa vifaa vya kubadili mifumo ya vyombo vya moto kutumia gesi asilia.
Pamoja na hayo, wamesema hakuna miundombinu rafiki kwa vituo vya mafuta kuanzisha maeneo ya kujaza gesi kwenye magari.
Kauli hizo zimetolewa wakati ambao madereva wanaotumia vyombo vya moto vitumiavyo gesi wakilalamika foleni kubwa kusubiri kupata huduma hiyo.
Solomon Albert, dereva wa bajaji anayetumia gesi amesema Oktoba Mosi, 2024 alitumia zaidi ya saa sita kusubiri nishati hiyo kutokana na foleni.
“Tatizo vituo ni vichache tulikuwa na vituo vitatu, kituo cha TAQA Dalbin kimepata hitilafu, sasa tuna vituo viwili vimebaki ambavyo navyo vimelemewa, ni muhimu Serikali ikaangalia namna ya kutengeneza mazingira kuvutia sekta binafsi kuwekeza kwenye ujenzi wa vituo, kutuepushia adha hii ya kupoteza muda,” amesema.
Amesema bajaji yake ameichukua kwa mkopo na anapaswa kurejesha Sh40,000 kila siku lakini imekuwa vigumu kutokana na muda anaoupoteza kusubiri kujaza gesi.
Mchambuzi wa Sera wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Khadija Ally amesema sababu ya sekta binafsi kutokimbilia kuwekeza kwenye gesi asilia, ni kukosekana msukumo wa kisera na kisheria wa kuifanya sekta binafsi wanapoanzisha vituo vya mafuta miongoni mwa vigezo viwe ni mifumo ya kujaza gesi.
“Ukiangalia miundombinu bado si rafiki kwa vituo vya mafuta kupata hiyo gesi, pia hakuna sera au sheria inayoipa sekta binafsi nafasi ya kuwekeza kwenye gesi asilia.
“Sekta binafsi inavyowekeza fedha inategemea kupata faida, sasa ni kwa namna gani itapata bado hakuna mwelekeo unaoonyesha kama kutakuwa na faida,” amesema.
Khadija amesema kodi kwenye vifaa vinavyotumika kubadili mifumo kwenye magari zinatatiza soko la uhitaji wa gesi kuendelea kupanuka, akisisitiza magari yenye uhitaji yanapokuwa mengi ndiyo wawekezaji huvutiwa kuwekeza.
Amesema hata kampuni zilizojitokeza kubadili mifumo ya mafuta kwenda kwenye gesi nazo zinakwama kutokana na kodi ya vifaa wanavyoingiza kutoka nje.
“Wananchi wanahitaji huduma lakini gharama ya kubadili mifumo ni kubwa,” amesema.
Profesa Anna Sikira wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) uwekezaji ni mdogo kwenye matumizi ya gesi asilia kutokana na wenye mamlaka kutoamua kutenda yale wanayosema kuhusu sekta ya gesi.
“Gesi kama nishati ni muhimu hasa tukiangalia mabadiliko ya tabianchi tunapoelekea ni kubaya zaidi, nchi yetu ina maeneo mengi yaliyoonekana jangwa, watu wanaendelea kutumia kuni na mkaa kama nishati, tungeimarisha gesi kama nishati ingetusaidia,” amesema.
Amesema endapo Serikali ingetekeleza mipango kama inavyopanga kungekuwa na hatua katika matumizi na uwekezaji katika gesi asilia.
“Serikali itende kama inavyosema kwenye suala la gesi tuone mambo yakifanyika, tupo hapa kwa sababu yale yanayosemwa hayafanyiki,” amesema.
Mtaalamu wa masuala ya mazingira, Dk Aidan Msafiri amesema matumizi ya gesi asilia kwenye vyombo vya moto ni muhimu kutokana na kuwa rafiki kwa mazingira.
“Kinachotukwamisha kwenye uwekezaji ni Serikali haikuwa imejipanga vya kutosa kisera, kiutawala au kuwezesha upatikanaji wa rasilimali za watu kuwekeza, kutumia gesi asilia ni jambo zuri lakini tulikurupuka,” amesema.
Dk Msafiri amesema Serikali na wadau hawakufanya utafiti wa kutosha kuangalia idadi ya vyombo vya moto vitakavyotumia gesi ndipo kuwaita wadau kuingia kuwekeza kwenye gesi.
Amesema takwimu za idadi ya vyombo vya moto vilivyopo na vitakavyoingia nchini itatoa taswira ya aina ya uwekezaji unaohitajika kwenye sekta ya gesi.
“Tunapaswa kupunguza vigingi vinavyozuia watu kukimbia eneo la gesi kufanya uwekezaji, kwa sababu ni eneo changa tuondoe kodi ambazo zinaweza kuwarudisha nyuma wawekezaji,” amesema.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huruia Tanzania (OUT), Dk Yohana Lawi amesema uwekezaji katika sekta ya gesi ni suala la kisera.
“Kama Taifa na Serikali, sera yetu katika matumizi ya gesi asilia inatoa kipaumbele kiasi gani na maelekezo gani kwenye matumizi ya gesi asilia, suala la kupata wawekezaji na kupata vituo ni jambo dogo kwa sababu ili wafungue vituo wanahitaji wateja lakini tuna sera gani?” amehoji.
Amesema endapo kuna sera inayoelekeza magari na mitambo viwandani kufikia miaka ijayo ziwe zinatumia gesi asilia kungesaidia kuvutia wawekezaji katika nishati hiyo.
Dk Lawi ametoa mfano wa baadhi ya mataifa yaliyoweka sera ya kuachana na magari yanayotumia petroli na dizeli, badala yake watajikita katika matumizi magari yanayotumia gesi.
Amesema uwepo wa sera inayoelekeza kuhamisha matumizi kutoka kwenye mafuta kwenda kwenye gesi unavutia sekta binafsi kukimbilia kufanya uwekezaji.
“Sekta ya gesi ni eneo linalopaswa kupewa kipaumbele kwani ina uwezo wa kubadili uchumi kwa kiwango kikubwa ndani ya muda mfupi,” amesema.
Amesema uchumi wa gesi ni mkubwa na unakwenda kubadilisha mfumo wa nishati hasa kupunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa na kupunguza utegemezi wa Dola ya Marekani.
“Matumizi ya gesi ni nafuu kuliko petroli na dizeli na matumizi yake yakiwa makubwa yatakwenda kushusha gharama za matumizi viwandani, usafirishaji wa watu na bidhaa, hivyo watu watakwenda kupata bidhaa kwa gharama nafuu,” amesema.
Dk Lawi amesema sababu ya gharama ya bidhaa kuwa kubwa ni kutokana na gharama za usafirishaji na uendeshaji kuwa kubwa, hivyo gesi ikipewa kipaumbele itakwenda kuonyesha mabadiliko kwenye uchumi.
Mkurugenzi wa Mkondo wa Chini wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Emanuel Gilbert akizungumza na Mwananchi amesema mkakati wa kumaliza kero ya madereva kutumia muda mwingi kusubiri huduma hiyo ni kukamilishwa kituo kingine cha kujaza gesi eneo la Sam Nujoma mwishoni mwa mwaka huu.
“Pia kuna wawekezaji binafsi ambao wanaendelea na hatua za awali za kuanza ujenzi wa vituo zaidi. TPDC itaingiza vituo jongefu ifikapo Juni 2025, kwa ujumla tunataraji kuongeza vituo 13 kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha,” amesema.
Kaimu Mkurugenzi wa TPDC, Francis Mwakapalila katika taarifa ya Septemba, 2024 akizungumzia ukuzaji wa matumizi ya gesi asilia nchini alisema hadi sasa wameruhusu kampuni binafsi zaidi ya 30 kujenga vituo vya gesi asilia iliyogandamizwa nchini (CNG) ili kuwezesha matumizi katika maeneo mbalimbali.