Rorya. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema hakuna sababu ya viongozi wa Serikali na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kukasirika pale vyama vya upinzani vinapowakosoa kwani kwa kufanya hivyo, vyama hivyo vinatimiza takwa la kikatiba.
Simbachawene ameyasema hayo leo Jumatano, Oktoba 2, 2024 kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Utegi wilayani Rorya ambapo vyama vya upinzani vimetengezwa na CCM ili kukupinga hatua ambayo inachochea chama hicho cha CCM kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
“Katika kutupinga wanatimiza wajibu wa kikatiba, lazima tuwasikilize, lazima tuvilee vyama vya upinzani na wanapotupinga tuwasikikilize na tutekeleze yale Watanzania wanayoyataka na kamwe hawawezi kututoa madarakani,” amesema.
Amebainisha kuwa wapinzani siyo watu wabaya, isipokuwa wanawakumbusha kutekeleza yale wanayopaswa kufanya na kwamba pale wanapoyatekeleza kwa ufasaha, wananchi wanazidi kuwaunga mkono, hivyo Serikali inakuwa na uhakika wa kuendelea kushika madaraka huku akiongeza kuwa bila CCM hakuna mpinzani.
Hata hivyo, Simbachawene amesema pamoja na uhuru wa kukosa na kupinga, ni vema vyama vya upinzani vikazingatia misingi ikiwemo masuala ya amani, umoja, mshikamano na utulivu na kwamba Watanzania kamwe wasidanganyike na mtu ambaye anataka kuvunja misingi hiyo.
“Huwezi kuwa na nchi ya kidemokrasia kama Tanzania bila kuwa na upinzani lakini kazi ya upinzani sio kuvuruga nchi, kwa hiyo niwakumbushe wapinzani kuzingatia misingi ya nchi na mjue uwepo wenu unategea CCM,” amesema.
Amesema nchi ya Tanzania ni ya muhimu kuliko vyama vya siasa kwani madaraka na vyeo ni utaratibu tu, hivyo vyama vya siasa havitakiwi kuathiri misingi ya nchi.
Katika hatua nyingine, Simbachawene ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mara kufanya uchunguzi kuhusu ujenzi wa jengo la ukumbi katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya baada ya kutoridhishwa na thamani ya fedha katika mradi huo.
“Mimi sio mhandisi lakini kwa macho ya kawaida kiasi cha fedha kilichotumika na jengo lenyewe ni vitu viwili tofauti, niuagize uongozi wa mkoa kufanya uchunguzi kujiridhisha kuhusu thamani ya fedha na kazi iliyofanyika hapa kabla ya uzinduzi wa jengo,” amesema.
Ametolea mfano wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambayo hadi sasa imegharimu takriban Sh1.5 bilioni huku kukiwa na majengo zaidi ya 16 ambayo mengi yamekamilika ikilinganishwa na ukumbi huo wenye thamani ya Sh1.25 bilioni.
“Hapa kuna jengo moja hata tukisema tulimege, tutapata majengo madogo manne, kule kuna majengo zaidi ya 16, tena makubwa yenye gharama sawa zilizotumika kwenye hii miradi miwili, ni sawa lakini kwa macho ya kawaida thamani ya fedha hailingani,” amesema.
Amesema fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inapatikana kwa jitihada nyingi, hivyo ni vyema miradi inayotekelezwa iakisi hali halisi na kwamba suala la ubora wa miradi pia ni la kupewa kipaumbele.
Awali, akitoa taarifa juu ya mradi huo, mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Ramadhani Mcharo amesema ukumbi huo wa kisasa hadi kukamilika unatarajiwa kugharimu Sh1.25 bilioni.
Amesema hadi sasa ujenzi umegharimu kiaisi cha Sh750 milioni ambapo umefikia asilimia 95 ya utekelezaji wake na kwamba jengo hilo likikamilika litatumika kwenye mikutano yote ya halmashauri hiyo ikowepo mikutano ya baraza la madiwani.
“Tumepokea Sh750 milioni ambazo ndizo tumepokea na ujenzi huu ulianza Januari 2022 kwa mfumo wa force akaunti, ukumbi ukikamilika mbali na kutumika kwenye mikutano lakini pia utakuwa chanzo cha mapato kwani utakuwa ukikodoshwa kwa shughuli mbalimbali kwa wananchi,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amekumbusha wananchi kuwa tayari kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa, Novemba 27, 2024.
“Ili kupiga kura au kupigiwa kura kwenye uchaguzi huu, ni lazima uwe umejiandikisha kwenye daftari la mkazi, niwaombe sote kwa pamoja itakapofika Oktoba 11, 2024 tukajiandikishe tayari kutimiza wajibu wetu wa kidemokrasia na kikatiba ifikapo Novemba,” amesema.
Mtambi amesema uchaguzi huo ni wa muhimu katika maendeleo ya nchi, hivyo kila Mtanzania mwenye sifa anapaswa kushiriki kikamilifu.