KOCHA wa Singida Black Stars, Patrick Aussems anakabiliwa na kibarua cha kuiongoza timu hiyo kumaliza unyonge dhidi ya Mashujaa kwenye hekaheka za Ligi Kuu Bara ambazo zinatarajiwa kuendelea kesho, Jumatano, katika viwanja viwili tofauti – Lake Tanganyika, Kigoma na Jamhuri, Dodoma.
Aussems na vijana wake watakuwa wageni wa Mashujaa katika Uwanja wa Lake Tanganyika, huku mchezo mwingine ukiwa kati ya Dodoma Jiji ambao wametoka kupoteza siku chache zilizopita dhidi ya Simba, lakini safari hii wataikaribisha Tabora United.
Rekodi zinaonyesha katika michezo mitatu ambayo Singida Black Stars (wakati huo ikiitwa Ihefu) imecheza dhidi ya Mashujaa hakuna hata mmoja ambao iliibuka na ushindi, imepoteza mara moja na ni msimu uliopita kwa mabao 2-0 kwenye uwanja ambao leo itacheza mara ya pili tangu kupanda daraja.
Matokeo ya mechi nyingine ambazo walikutana ziliisha sare, moja ikiwa ya mzunguko wa pili (1-1) katika ligi msimu wa 2023/24 na nyingine robo fainali ya Kombe la FA (0-0) ambapo Singida Black Stars (Ihefu) ilivuka kwa mikwaju ya penalti (4-3).
Akizungumzia mchezo huo, Aussems alikiri ugumu mbele yao, lakini anaamini kikosi chake kina uwezo wa kupambana na kufanikisha mipango yao.
“Ni mechi ngumu, lakini tumejiandaa vyema. Tunajua changamoto zilizopo mbele yetu, lakini nina imani wachezaji wangu watajituma na kupambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema.
“Tunacheza dhidi ya timu yenye ubora, lakini tulijipanga kwa mikakati ya kuwazuia na kutumia nafasi zetu ipasavyo. Kila mchezaji ana jukumu muhimu na natumaini wataonesha juhudi uwanjani. Ushindi ni muhimu lakini nidhamu na mchezo wa pamoja ndiyo msingi wa mafanikio yetu.”
Kocha wa Mashujaa, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ alisema: “Tunajua Singida ni timu nzuri na ina wachezaji wenye uwezo, lakini tumejipanga vilivyo. Lengo letu ni kushinda mchezo huu na kuendelea kujiimarisha kwenye ligi.
“Hakuna mechi nyepesi katika ligi, lakini nawahakikishia mashabiki wetu kuwa tutaonesha kandanda safi na kupambana kwa kila hali.”
Katika michezo mitano iliyopita ya mwanzoni mwa msimu Mashujaa imeshinda miwili na sare tatu ikiwa na pointi tisa, huku Singida Black Stars ikishinda minne na sare moja na ni vinara wa ligi wakiwa na pointi 13.
DODOMA JIJI vs TABORA
Hii ni mechi nyingine kali ambayo itachezwa makao makuu ya nchi, Dodoma, kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Jiji watakapokuwa na nafasi ya kujiuliza baada ya kupoteza mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Simba.
Dodoma Jiji itaingia katika mchezo huo ikiwa na rekodi nzuri kwenye uwanja wake wa nyumbani Jamhuri dhidi ya Tabora United, msimu uliopita waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Hassan Mwaterema.
Timu hizo kila moja imepoteza mara moja katika michezo mitano iliyopita ya ligi zote zikiwa nyumbani – Dodoma Jiji dhidi ya Mnyama (1-0), huku Tabora ikifungwa na Fountain Gate kwa mabao 3-1.