Tanga. Siku tisa tangu yalipotokea mauaji ya Jonais Shao, aliyekuwa Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, pamoja na mwanawe na msichana wake wa kazi za ndani, Jeshi la Polisi limesema linawashilikia watuhumiwa sita.
Tukio hilo la mauaji ya Jonais (46), mwanawe Dedan Shao (8), mwanafunzi wa darasa la tatu na Salha Hassan (18), msichana wake wa kazi waliochomwa moto yalitokea Septemba 23, 2024 ndani ya msitu wa Hifadhi ya Korogwe, uliopo Kijiji cha Sindeni wilayani Handeni.
Jonais na mwanawe Dedan walizikwa Septemba 28, 2024 katika Kijiji cha Maring’a Kondiki, Mwika wilayani Moshi, Kilimanjaro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Oktoba 2, 2024 amesema uchunguzi na msako wa jeshi hilo umewezesha kuwakamata watuhumiwa hao sita.
Amewataja kuwa ni wakulima Bernard Kizughuto (31), mkazi wa Msambiazi Korogwe, Marko Jambia maarufu Rajabu Mhilu (28) wa Lushoto, Peter Jambia au jina lingine Johson (31) wa Msambiazi Korogwe, na Hassan Kitombo ‘Jombi’ (53) mkazi wa Kwamaraha Handeni.
Wengine ni James Mkama maarufu Teacher (42), mfanyabiashara na mkazi wa Mtonga Korogwe na Omary Salehe ‘Mwiba’ (20), ambaye ni mkulima na mkazi wa Kwamaraha Handeni.
“Upelelezi wa shauri hili unaendelea, ili hatua nyingine za kisheria zifuate. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linalaani vikali vitendo vyote vya kihalifu na halitamuonea muhali wala halitasita kumchukulia au kuwachukulia hatua za kisheria yeyote au kikundi cha watu wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu,” amesema Mchunguzi.
Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Polisi katika kubaini na kuzuia uhalifu, ili kuendelea kuuweka mkoa huo kuwa salama.
Septemba 24, 2024 akizungumzia tukio hilo, Kamanda Mchunguzi alisema lilitokea Septemba 23, saa tatu usiku.
Alisema Polisi lilipokea taarifa kuwa ndani ya msitu wa Hifadhi Korogwe kuna gari aina ya Toyota IST lenye namba za usajili T 305 EAL linaungua moto na pembeni yake kuna watu wawili wakiungua.
Mchunguzi alisema askari walifika eneo hilo na kukuta kuna gari ndogo likiungua na pembeni yake kukiwa na watu wawili walioungua kwa moto na kufariki dunia wakiwa pembeni ya gari hilo.
Alisema baada ya uchunguzi wa awali ilibainika miili iliyokuwa nje ya gari ni ya jinsia ya kike na ndani ya gari kiti cha nyuma ulionekana mwili mwingine ambao nao umeungua moto hadi kupoteza sura na haukubainika ni wa jinsia gani.
Akizungumza na Mwananchi wakati huo, Lameck Shao, mume wa marehemu Jonais alisema alikuwa akiwasiliana na mkewe hadi Septemba 23 saa tatu usiku kabla ya mawasiliano kukatika.
“Tuliwasiliana vizuri hadi saa tatu usiku kwamba amefika nyumbani baada ya hapo akawa hapatikani, nilijaribu kutafuta namna ya kupata mawasiliano hadi asubuhi ya leo (Septemba 24) nilipomtuma kijana wa shamba aende pale nyumbani.
“Baada ya kufika pale, yule kijana hakukuta mtu na alipozungumza na majirani walibaini milango iko wazi. Tulianza kufuatilia ndipo mchana tuliposikia taarifa kwamba kuna watu wameungua kwenye gari,” alisema.
Wakati wa maziko ya Jonais na wanawe Dedan, wito ulitolewa kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha watuhumiwa wanapatikana na sheria ichukue mkondo wake.
Dainess Shao, mama mzazi wa Jonais alisema alikuwa ndiye tegemeo lake baada ya baba yake mzazi, Edward Shao kufariki dunia miaka michache iliyopita.
Aliviomba vyombo vya dola vichunguze tukio hilo, ili mwanaye na mjukuu wake wapate haki zao.
Akisoma historia ya marehemu, Mchungaji Jesse Shao, ambaye ni mwanafamilia alidai kina Jonais walivamiwa nyumbani kwao na watu wasiojulikana na kisha kuondoka nao zaidi ya kilomita 50 ambako walichomwa moto msituni.
Akihubiri wakati wa ibada ya mazishi, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Barikiel Panga alilaani tukio hilo la mauaji, akisema hakuna kabila lolote wala dini inayoruhusu mtu kutolewa uhai.
Aliitaka jamii kukemea na kuwaombea wote wenye tabia za kinyama wakutane na neema ya Mungu, ili waache maovu na kuwakatili wenzao.