Staa Srelio aionya Dar City

BAADA ya Srelio kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), kocha msaidizi wa timu hiyo, Miyasi Nyamoko amesema mkakati waliouweka ni kuhakikisha wanaiondoa Dar City katika hatua hiyo.

Srelio imepata nafasi hiyo ni baada ya kuifunga Mgulani JKT kwa pointi 45-35, hali iliyofanya ishike nafasi ya nane kwenye msimamo wa mashindano hayo.

Kwa mujibu wa sheria na kanuni ya mashindano, timu itakayoshika nafasi ya kwanza itacheza na inayoshika nafasi ya nane katika mchezo wa robo fainali.

Wakati huohuo kamishna wa Ufundi na Mashindano hayo,  Haleluya Kavalambi alisema robo fainali itaanza Oktoba 8.

Akizungumzia robo fainali hiyo, alisema mshindi wa kwanza atacheza na wa nane, wa pili na wa saba, wa tatu na wa sita ilhali yule wa nne atakipiga na namba tano.

Kavalambi alisema ratiba kamili itapangwa baada ya JKT, Mchenga Star na ABC kukamilisha michezo 30.

Timu zilizotinga robo fainali ni Dar City, UDSM Outsiders, JKT, Savio, Mchenga Stars, ABC, Vijana (City Bulls) na Srelio.

Related Posts