Dar es Salaam. Serikali imepanga Oktoba 15, 2024 kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo (Commital Proceedings), aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande (66) na wenzake.
Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 38/2022 kukamilika.
Maelezo hayo ya mashahidi na vielelezo, yanatarajia kusomwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo, kama Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) atawasilisha hati ya kuruhusu Mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi hiyo, shauri hilo litasikilizwa hapo.
Lakini kama hatawasilisha hati hiyo, basi kesi hiyo itahamishiwa Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, kwa ajili ya usikilizwaji wa ushahidi.
Kipande na wenzake wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya dola za Marekani 1.85 milioni sawa na Sh4.2 bilioni.
Uamuzi huyo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu, baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilia.
Kasala ameieleza Mahakama hiyo, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Kasala alidai kuwa wamewasilisha vijalada vyenye taarifa muhimu Mahakama Kuu.
Alifafanua vijalada hivyo vyenye taarifa hizo tayari vimeshasajiliwa Mahakama Kuu, hivyo anaomba Mahakama ipange terehe nyingine ili waweze kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Hakimu Magutu baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka, alisema ‘commital’ hiyo itasikilizwa Oktoba 15, 2024 na kisha kuahirisha kesi hiyo.
Washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana, baada ya kwenda kuomba Mahakama Kuu.
Mbali na Kipande, washtakiwa wengine ni Peter Gawile (58) aliyekuwa Ofisa Rasilimali Watu wa TPA na mkazi wa Mianzini; Casmily Lujegi (65)aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi wa TPA na mkazi wa Mbezi Juu.
Wengine ni Mashaka Kisanta (59) aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi pamoja na Kilian Chale (51) aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kati ya Oktoba Mosi, 2014 na Oktoba Mosi 2020 Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa la kuisababishia TPA hasara ya Sh4.2 bilioni.
Pia, kati ya Januari Mosi, 2015 hadi Februari 17, 2015 washitakiwa kwa pamoja wakiwa maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni namba AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia dola za Marekani 1,857,908.04 .
Shtaka la tatu, inadaiwa kati ya Oktoba Mosi, 2014 na Oktoba Mosi, 2020 eneo la TPA na maeneo mengine ya Dar es Salaam, washtakiwa kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP) bila kupata kibali cha bodi ya zabuni ya Mamlaka hiyo na kushindwa kufuata kanuni za zabuni hivyo kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya bodi hiyo, jambo lililosababisha TPA hasara ya dola za Marekani 1.8 milioni ambazo ni sawa na Sh 4.2 bilioni.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Juni 30, 2022 na kusomewa mashtaka yao.