Huku maofisini tuna watu wa kila aina. Wapo wenye makuzi ya kimjinimjini na wanaoyaishi mafunzo ya wazazi wao toka kijijini. Kuna wahuni, wastaarabu, wenye hasira na wapole.
Pia, tunao wachapakazi, wavivu, wakweli na wenye husda. Mtu huonekana vizuri jinsi alivyo anapochanganya tabia zilizo kwenye makundi hayo kutegemeana na mtu alipotoka, elimu yake, uzoefu wa kazi na tabia yake kiujumla. Kwa mfano utampenda yule mchapakazi na mkweli.
Kwa bahati mbaya tunao waliokimbia umande halafu wasio wakweli, na usiombe wachanganye na uvivu. Ni rahisi kwao kuanzisha migogoro na taharuki kazini, hujifanya kujua na kuweza kila jambo. Hawaheshimu wakubwa wala sheria za kazi. Uvivu wao huwashurutisha kuiga ubosi, na mara nyingi wanapofanya makosa na kuadhibiwa huleta jeuri na ubabe.
Wana mazoea ya kuwasema mabosi wao: “Nimempokea mwenyewe hapa akiwa hana lolote!”
Hata kama ni kweli alimsaidia kufika hapo, jambo hilo lina maana gani kwenye timu inayofanya kazi pamoja? Tangu lini kidole kimoja kikajitegemea kuvunja chawa. Chukua mfano wa timu ya Taifa iliyopata ushindi; je, mlinda mlango atajigamba kuwa bila yeye wasingeshinda? Kadhalika mlinzi, kiungo na mshambuliaji gani anayeweza kusema hivyo? Kama ndivyo, kwa nini asicheze peke yake?
Serikali ni taasisi kiongozi ndani ya jamii. Ni dola yenye mamlaka ya kutawala na kufanya maazimio kwa wote. Inatunza na kutekeleza sheria, kanuni na miongozo na kuendesha shughuli muhimu za umma. Hivyo ni chombo kinachostahili kuheshimiwa na wote kutoka katika kila kundi la kijamii. Hii ni kwa sababu shabaha kuu ya serikali ni kutunza amani na usalama wa raia wote katika jamii.
Vilevile, ni timu inayoundwa kutokana na kiongozi mmoja mmoja na makundi yanayotoka kwenye jamii. Wote wanapaswa kufanya kazi pamoja kulingana na kanuni zilizowekwa kama kuheshimu wasemaji wa Serikali badala ya kila mmoja kujisemea anavyotaka, na kuwa wanyenyekevu kwa wananchi, maana hao ndio wanaowaweka hapo. Inapotokea mmoja wao akakengeuka huivuruga Serikali nzima. Ule usemi wa “Samaki mmoja akioza…” unaihusu sana Serikali hii.
Hivi sasa tabia za ajabu zimezuka na kuchukua nafasi kwenye chama tawala na Serikali yetu. Viongozi wamekuwa wakiwakejeli viongozi wenzao hadharani, na kuropoka hisia zao kwa kisingizia Serikali. Kiongozi anadiriki kubwata mbele ya kadamnasi kuwa kiongozi mwenzake asingekuwapo bila msaada wake. Kuna mmoja amediriki kusema ati madiwani na wabunge hawakuwa na ulazima wa kufanya kampeni, kwani walitengenezewa nafasi na Serikali.
Huku mtaani kwetu, walikuwapo wazee wa mjini waliokosa elimu, lakini waliojawa na tambo za kuwajua matajiri wote tangu wakiwa makapuku. Wanadai kuwa na uswahiba na watu wote maarufu, lakini pia viongozi wote wa juu wa Serikali tangu awamu ya kwanza tangu wakiwa chekechea. Wanasema viongozi hawakohoi mbele zao kwani wanazo siri zote. Hii ni kefule mbaya sana inayorithiwa na vizazi, ndiyo maana tunayaona haya yakijitokeza leo.
Mimi sijawahi kuwa kiongozi hata wa darasa. Lakini nahisi hata kwenye uongozi kuna makundi kama yale niliyoyataja pale mwanzoni, hasa ya nongwa na husda, uvivu na uongo. Badala ya kuwekeza kwenye ubunifu wa mambo yatakayoleta tija kwa wananchi, viongozi wanakalia kuchokonoa wenzao. Viongozi wasio na sera wala maono yenye kuleta tija, bali wanaoendekeza ubabe kwenye masuala ya kisera.
Hivi karibuni kumejitokeza sintofahamu kwa wananchi kuhusiana na haki zao kidemokrasia. Hayo ni baada ya kauli za makada wa CCM ambao baadhi yao ni viongozi wakubwa Serikalini kudai kwamba hakuna muujiza unaoweza kuwang’oa madarakani.
Wamekwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa hawana haja ya kutegemea masanduku ya kura, wananchi wapige kura au wasipige kwao siyo ishu, kwani wamejiandaa kwa ushindi hata wa kutokana na “magoli ya mikono”.
Kauli hizi zimekuwa zikiwavunja mioyo vijana wengi wenye nia ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu hapo mwakani. Vijana wanafifishwa mioyo kiasi cha kuondoa imani juu ya Serikali yao. Hawana nguvu tena kusimamia haki yao ya kuchagua na kuchaguliwa iliyopo kikatiba, na sasa wimbo wa “uwike usiwike kutakucha” unajirudia masikioni mwao.
Kitendo cha Serikali kuhusishwa kwa upande fulani kwenye mizozo ya vyama vya siasa ni kosa na aibu kubwa. Ni ukiukwaji wa viapo vya uaminifu vilivyoshuhudiwa na Katiba na misahafu ya dini kulingana na imani ya kiongozi, hivyo ni kumkosea Mwenyezi Mungu waziwazi. Hivyo mtu yeyote anayetangaza kuwa Serikali ilimkingia kifua kwenye uchaguzi anafanya makosa makubwa zaidi ya uhaini.
Hili si jambo jipya kutokea hapa nchini. Tangu tulipokuwa kwenye awamu za awali za Serikali, viongozi kadhaa wameshawahi kuchukuliwa hatua kwa vitendo vya aina hiyo.
Lakini kwa vile linajirudia, Serikali haina budi kuangalia njia bora zaidi katika uteuzi wa viongozi, huku wanaohusika wakiwajibishwa hadharani. Vinginevyo tutaendelea kutenda dhambi ya kuurithisha uchafu huu kwa vizazi vinavyokuja.
Kila mgombea alikuja kuomba ridhaa mbele ya wananchi akiwa mguu sawa, mikono nyuma na kichwa chini.