Wananchi kushirikishwa mchakato wa kumng’oa Gachagua

Nairobi. Spika wa Bunge la Kitaifa la Kenya, Moses Wetang’ula ametangaza ushiriki wa umma katika hoja ya kumng’oa madarakani Naibu Rais, Rigathi Gachagua Ijumaa, Oktoba 4, 2024.

Kwa mujibu wa tovuti ya The Standard, mchakato huo utafanyika katika kaunti zote 47 na Katibu wa Bunge atatoa taarifa kamili kupitia matangazo ya vyombo vya habari kuanzia leo Jumatano Oktoba 2, 2024.

Wetang’ula amebainisha kuwa shughuli zote za Bunge kuanzia Alhamisi, Oktoba 3, 2024 hadi Jumatatu Oktoba 7, 2024 zitasitishwa ili kupokea maoni ya umma.

Kamati ya Shughuli za Bunge itaweka azimio la kuahirisha kikao cha Bunge kesho Alhamisi na kufanya kikao cha asubuhi Jumanne, Oktoba 8, 2024 kujadili hoja hiyo.

Gachagua anaweza kujitokeza ana kwa ana au kupitia uwakilishi wa kisheria.

Hatua hiyo inafuatia baada ya Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse kuwasilisha rasmi hoja ya kumtimua Gashagua, akisema hoja za kufikia uamuzi huo ni sahihi na zinajitosha kumwondoa ofisini.

Wetang’ula alisoma hoja hiyo Jumanne Oktoba Mosi, 2024 na kuthibitisha kuwa wabunge 291 waliiunga mkono hoja hiyo, na kuvuka idadi ya wabunge 117 wanaohitajika ili kuunga mkono hoja hiyo.

Mutuse alitoa waraka wa kurasa 100 za ushahidi zinazoelezea sababu zake za kutaka kiongozi huyo atimuliwe.

“Ibara ya 145 (1) ya Katiba inatamka kwamba mjumbe wa Bunge akiungwa mkono na angalau theluthi moja ya wabunge wote, anaweza kutoa hoja ya kushitakiwa kwa Rais au naibu wake kwa sababu ya ukiukwaji wa Katiba,” amesema Wetang’ula.

Related Posts