Iran yawaita mabalozi wa Ulaya baada ya kuikosoa – DW – 03.10.2024

Hatua hiyo ya Iran imechukuliwa baada ya hatua sawa na hiyo kuchukuliwa pia na Ujerumani na Austria, kumuita balozi wa Iran kumhoji juu ya shambulizi la taifa hilo kwa Israel lililotokea siku ya Jumanne. Katika taarifa yake, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Abbas Araghchi amesema mashambulizi yaliyofanywa na nchi yake yalikuwa muhimu na halali yaliolenga kuiadhibu serikali ya Israel aliyoiita ya kichokozi.

Israel yasema wanamgambo 15 wameuwawa Lebanon

Iran ilivurumisha makombora zaidi ya 180 nchini Israel, ikisema inajibu mashambulizi inayofanya Lebanon na Gaza. Shambulizi hilo lilisababisha nchi hiyo kukosolewa vikali na mataifa kadhaa ya Magharibi. Msemaji wa wizara hiyo ya kigeni ya Iran  Esmail Baghaei amekosoa kile alichokiita undumilakuwili unaoendelea ndani ya kund la G7 baada ya kundi hilo kulaani shambulio dhidi ya Israel. Amelikosoa pia kwa kutaka Iran iekewe vikwazo zaidi vya kiuchumi.

Israel imeshasema kupitia Waziri Mkuu wake Benjamin Netanyahu kwamba itajibu muda wowote shambulizi hilo ililoliita kosa kubwa, lakini Rais wa Marekani Joe Biden ameondoa wasiwasi huo akisema haamini Israel itatekeleza shambulizi hilo hii leo. Alizungumza hayo katika ikulu ya White House alipoulizwa na waandishi habari iwapo ataridhia Israel, kujibu shambulizi hilo la Iran.

Uamuzi wa kumzuia Guterres kuingia Israel wakosolewa

UN |Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: William Volcov/ZUMA Press Wire/picture alliance

Huku hayo yakiarifiwa Ufaransa imeikosoa hatua ya Israel ya kumtangaza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuwa mtu asiyetakiwa kuonekana nchini humo kwa madai ya kushindwa kuyalaani vikali mashambulizi ya makombora ya Iran dhidi ya taifa hilo. Ufaransa imesema uamuzi huo haufai. Wizara ya kigeni ya Ufaransa imesema inamuunga mkono kikamilifu na kumuamini Antonio Gutteres ikisema Umoja wa Mataifa umekuwa na jukumu muhimu kwa udhabiti wa kikanda

Mashirika kadhaa ya ndege yasimamisha safari zake kwenda Mashariki ya Kati

Kando na hayo waziri wa afya wa Lebanon Firass Abiad, amesema zaidi ya wahudumu 100 wa afya na wafanyakazi wa zimamoto wameuwawa na wengine 220 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel yanayofanywa nchini humo. Mashambulizi hayo yanasemekana kulenga hospitali 9, tasisi nyengine 45 za afya na tariban magari 130 ya kubebea wagonjwa pamoja na zimamoto.

Waziri huyo wa afya wa Lebanon amewaambia waandishi habari kwamba Israel inachokifanya ni ukiukwaji wa sheria ya kimataifa na bila shaka kuwa uhalifu wa kivita. Amesema kisingizio cha Israel kusema kuwa magari hayo na maeneo yalioshambuliwa yanasheheni silaha za Hezbollah ni uwongo mtupu uliotumika pia katika vita vya Gaza.

Israel yaendeleza mashambulizi Lebanon

Lebanon
Lebanon imesema mashambulizi ya Israel yamewaua zaidi ya wahudumu 100 wa afya na wafanyakazi wa zimamoto nchini humoPicha: Amr Abdallah Dalsh/REUTERS

Israel bado imeendelea na mashambulizi yake nchini Lebanon, na safari hii imetoa onyo kwa wakaazi kuondoka kusini mwa nchi hiyo ikiashiria kutanua operesheni yake ya ardhini iliyoanzishwa mapema wiki hii dhidi ya kundi la Hezbollah. Watu hao wameamriwa kuondoka Nabatieh eneo la Kusini na jamii nyengine ya watu ikitakiwa kuondoka eneo la kaskazini mwa mto Litani.

Israel: Mashambulizi ya Iran ni kitendo kikubwa cha uchokozi

Hayo yanaripotiwa wakati Uingereza ikisema raia wake wanaendelea kuhamishwa kutoka Lebanon baada ya kufanikiwa kuwaondoa wengine 150. Wizara ya mambo ya nje imesema usalama wa raia wake unapewa kipaumbeloe ndio maana wameongeza idadi ya ndege ndogo zinazopaswa kuwaonda raia wake wanaotaka kurejea nyumbani. Ujerumani pia ni miongoni mwa mataifa yaliowarejesha raia wake nyumani kutoka Lebanon.

Kwengineko waziri wa uchukuzi wa Lebanon Ali Hamieh amesema mipaka yote ipo chini ya uchunguzi kufuatia madai ya Israel kwamba Hezbollah inapitisha silaha kimagendo kutoka Syria kupitia mpaka wa Masnaa

Mzozo kati ya Israel na Hezbollah wapamba moto

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

reuters/afp/ap

Related Posts