Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 17 wa taasisi ya IIA, jijini Arusha. |
CPA Benjamin Mashauri Mkaguzi Mkuu wa ndani Tanzania Bara akizungumza kwenye mkutano huo. |
Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA), CPA Dkt. Zelia Njeza akizungumza na Wataalamu viongozi wa kada hiyo ya wakaguzi wa ndani katika mkutano Mkuu wa 17, wa mwaka, jijini Arusha. |
Wakaguzi wa Ndani nchini Tanzania (IIA), na wadau wengine wakiwa katika mkutano huo. |
Na Mwandishi Wetu, Arusha
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka Wakaguzi wa Ndani nchini Tanzania (IIA), kufanya kazi kuendena na mabadiliko ya kukua kwa teknolojia, ikiwa ni pamoja na kutumia changamoto za kiuchumi katika mataifa ya Afrika kama fursa kuweza kufikia malengo yao.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Makamu huyo wa Pili wa Rais, Mhe Suleiman Abdulla amesema ipo haja kwa wakaguzi wa ndani kuendana na mabadiliko ya ukuaji wa teknolojia ili kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu ya Wataalamu wa kada hiyo.
“Serikali itaendelea kushirikiana na wakaguzi wa ndani ili kuendelea kuimarisha shughuli za maendeleo ya wananchi na Taifa kupitia kazi za wakaguzi, kubwa zaidi ni kuendelea kuwa wabunifu, na uwajibikaji katika kazi hiyo.
Mhe. Makamu wa Pili wa Rais amebainisha kuwa kada ya ukaguzi wa ndani ni ya msingi katika kuongeza tija na chachu ya maendeleo kwenye taasisi za umma na binafsi kwani inaelekeza kuzingatiwa maadili na miiko ya kazi, hivyo kuondokana na dhana ya kukinzana na Serikali licha ya kuwa imekuwa msaada mkubwa kwa kile kuibua mambo mbalimbali yanayo kinzana na maendeleo ya taasisi na Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia suala la urasimishaji, wa Sheria ya taaluma ya ukaguzi ambayo ndio miongoni mwa ajenda za msingi kwa IIA, Mhe. Suleiman Abdulla amesema tayari Serikali imeendelea na mchakato katika kupata Suluhu ya uwepo wa Sheria itakayo ongoza na kusimamia kada ya ukaguzi wa ndani kwa maendeleo endelevu.
Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani nchini Tanzania (IIA) CPA, Dkt. Zelia Njeza amesema kwa muda mrefu kada hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kupatikana kwa Sheria ya wakaguzi wa ndani pamoja na muundo utakao saidia kufikisha ajenda na mawazo yatolewayo na kazi ya wakaguzi katika taasisi zao.
“Kiu yetu kubwa ni kuona Serikali inafanyia kazi ombi letu la kuwepo kwa Sheria ya ukaguzi wa ndani, na tunashukuru mchakato wa kufanikisha hilo umesha anza hivyo tunaomba kufanyiwa kazi kwa haraka na kukamilika ili tuweze kuendana na kasi ya mabadiliko tunayoyaongelea katika mkutano huu wa 17 wa mwaka. Pia tunaomba miundo ya wakaguzi wa Ndani pia iweze kuangaliwa maana asilimia kubwa bado hawako vizuri kwenye miundo yao,” alisema CPA, Njeza Rais wa IIA nchini Tanzania.
Katika hatua nyengine, Dkt. Njeza akizungumzia suala la umuhimu wa maboresho ya muundo wa ripoti za kazi za wakaguzi kuzingatiwa katika taasisi mbalimbali kwa kuzingatia mnyororo wa Uongozi.
“Mkaguzi wa ndani anatakiwa kuripoti kwa Mkuu wa Taasisi, Utawala na wakati mwingine kwenye Bodi ya Uongozi moja kwa moja, hivyo tunaomba miundo hiyo pia iangaliwe ili kuongeza tija itokanayo na kazi ya ukaguzi wa ndani nchini.” Alisema rais wa (IIA).
Naye Mkaguzi Mkuu wa ndani Tanzania Bara, CPA Benjamin Mashauri akizungumza katika mkutano huo, amesema zipo changamoto muhimu ambazo zikifanyiwa kazi kada hiyo itaendelea kuthaminika zaidi na mchango wake kuonekana wazi.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kuwepo kwa viongozi wa taasisi kujichukulia maamuzi pasi na kufata taratibu za kisheria suala ambalo lina ondoa hadhi ya kada hiyo katika mazingira ya utawala bora.
“Bado Kuna taasisi za umma na binafsi wakaguzi wa ndani, mfano wakati mwingine wakaguzi wanakosa vitendea kazi ikiwemo Kompyuta, magari, suala ambalo linadhohofisha ufanisi wakati wa utekelezaji wa majukumu ya mkaguzi wa ndani,” alisema CPA Mashauri.
Katika mkutano huo Mkuu wa 17 wa mwaka kwa wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA), zaidi ya washiriki 70 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika yameshiriki, ukitanguliwa na jukwaa la viongozi wa taasisi, huku lengo kuu ikiwa ni kubadilishana uzoefu juu ya namna bora ya kufanya kazi za wakaguzi katika taasisi na kuleta tija kwa wananchi katika mataifa yao.