Mpalestina atunukiwa Tuzo Mbadala ya Nobel – DW – 03.10.2024

Akitangaza tuzo hiyo mkurugenzi Ole von Uexküll amesema washindi hao wametunukiwa tuzo hiyo kutokana na mchango wao katika mataifa yao na jukwaa la kimataifa. 

Mpalestina Issa Amro na vijana wake wa kundi linalopinga ukaliaji haramu wa Israel katika maeneo ya wapalestina ni miongoni mwa waliopokea tuzo hiyo mbadala ya Nobel. Kundi lake la (YAS) linafanya harakati za kutafuta haki za kiraia za wapalestina kwa amani.

Mwingine aliyepokea tuzo hiyo ni Joan Carling raia wa Ufilipino. Katika juhudi zake Carling amefahamika kwa kupaza sauti za wenyeji katika masuala ya ikolojia ya kimataifa na uongozi wake katika kutetea haki za watu, ardhi na utamaduni.

Soma pia: Mshindi wa Tuzo ya Nobel ahukumiwa miaka 10 jela Belarus

Kutoka Msumbiji Anabela Lemos akiongoza shirika lisilo la kiserikali la Justica Ambiental ametunukiwa, kwa jukumu lake katika kupinga miradi ya uchimbaji wa gesi kimiminika kaskazini mwa Msumbiji.

Forensic Architecture ya Uingereza ilipokea tuzo hiyo kwa kuanzisha njia za uchunguzi wa kidijitali ili kuhakikisha haki na uwajibikaji kwa waathirika wa ukiukwaji wa haki za binadamu na mazingira.

Tuzo yenye hadhi

Norway Oslo 2023 | Tuzo ya Amani ya Nobel | Narges Mohammadi
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2023 Narges Mohammadi.Picha: Sergei Gapon/Anadolu/picture alliance

Hata hivyo Tuzo ya Nobel itatangazwa wiki ijayo kutoa taji la mafanikio yaliyoifanya dunia kuwa mahali pazuri zaidi, kutoa mwanga wa matumaini huku kukiwa na mzozo wa Mashariki ya Kati, vita nchini Ukraine, njaa nchini Sudan na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kwa ajili ya Tuzo ya Amani, yenye hadhi kubwa kati ya washindi sita wa tuzo ya Nobel, wataalam wanasema wakati huu ni vigumu zaidi kutabiri uteuzi wa Kamati ya Nobel ya Norway, utakaofichuliwa tarehe 11 Oktoba.

Soma pia: Tuzo mbadala ya Nobel yatunukiwa Wasaudi Arabia

Miongoni mwa wanaotajwa kwamba huenda wakashinda tuzo hiyo ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi la Palestina (UNRWA), Mahakama ya Kimataifa ya Haki na mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Kwa jumla wagombea 286 wamependekezwa kwa mwaka huu.

Mchango muhimu kwa amani

Uchaguzi Afrika Kusini 2024
Mchango wa waangalizi katika uchaguzi kwenye mataifa mbalimbali ni muhimu katika amani na utulivu.Picha: Alet Pretorius/REUTERS

Akizungumzia matarajio katika ushindani, Henrik Urdal, mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Oslo amesema:

“Mwaka huu, nadhani tunaweza kuona waangalizi wa uchaguzi wakishinda Tuzo ya Amani ya Nobel. Tunajua kwamba mataifa ya kidemokrasia ni tulivu na yenye amani zaidi, na mwaka huu, zaidi ya nusu ya watu duniani wanapiga kura.”

“Sio wote katika mataifa ya kidemokrasia, lakini waangalizi wa uchaguzi wanaangalia uadilifu wa uchaguzi na kuhakikisha kuwa unakuwa huru na wa haki, na kwa hivyo, uangalizi wa uchaguzi ni mchango muhimu sana kwa amani na utulivu.”

Tuzo ya mwaka jana ilikwenda kwa Narges Mohammadi, mfungwa mtetezi wa haki za wanawake wa Iran, katika harakati zake za kupaza sauti wakati wa maandamano ya wanaoipinga serikali.

 

 

Related Posts