UAMUZI TCRA KUFUNGIA MAUDHUI MITANDAO MCL WAISHTUA TEF


JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeshtushwa na taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusitisha kwa siku 30 leseni za huduma za maudhui mtandaoni za kampuni ya Mwananchi Communications Limited (The Citizen, Mwananchi Digital, Mwananchi na MwanaSpoti) kutoa huduma za maudhui mtandaoni nchini.

Taarifa iliyotolewa Oktoba 2, 2024 na Mkurugenzi mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri K. Bakari inasema kampuni hiyo ilichapisha maudhui yaliyokiuka kanuni ambayo yameleta tafsiri hasi kwa taifa, jambo ambalo linaathiri na kuharibu umoja, amani na mshikamano wa kitaifa.

Kwa muda mrefu TEF tumekuwa tukilalamikia mamlaka makubwa yanayotolewa kisheria kwenye taasisi au wakuu wa taasisi ya kuwa walalamikaji, waendesha mashitaka na watoa hukumu bila upande wa pili unaotuhumiwa kupewa fursa ya kusikilizwa wazi hadharani.

Tutaendelea kudai haki hii ya asili (natural justice) ya chombo cha habari kinachotuhumiwa kupewa hati ya mashitaka, kikajitetea mbele ya taasisi huru au Mahakama, kisha uamuzi ufanyike ambao ndiyo utawala wa sheria badala ya sasa ambapo sheria inatoa mamlaka kwa mtu mmoja kufanya uamuzi mzito kama huu. Mwananchi walipaswa kufunguliwa mashataka katika chombo huru na wao kujitetea, kisha chombo hicho kutoa hukumu kulingana na mashtaka yaliyowasilishwa mbele yake.

Tumeviona pia vibonzo au maudhui yaliyolalamikiwa na TCRA. Tunawasihi wahariri na watendaji wa vyombo vya habari kufahamu kuwa sheria mbaya inaendelea kuwa sheria hadi itakapobadilishwa.

Tunawasihi wahariri na waandishi nchini kufahamu ukweli kuwa utamaduni unatofautiana nchi hadi nchi na zipo njia za kufikisha ujumbe kwa njia sahihi badala ya kujiingiza katika mazingira yanayoweza kutafsiriwa kama kejeli.

Kwa vyovyote vile, tayari tatizo limetokea na kinachotakiwa sasa tunashauri pande zote mbili; Serikali na Mwananchi Communications, wakutane na kujadili suala hili na kulimaliza kwa masilahi mapana ya taifa na uhuru wa vyombo vya habari ndani ya muda mfupi kadri inavyowezekana.

Related Posts