Mamilioni ya watu nchini Ghana wanakabiliwa na matokeo ya hatari ya uchimbaji haramu wa dhahabu ambao umesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira hasa katika jamii za vijijini.
Licha miito ya kitaifa, uchimbaji madini haramu unaendelea nchini Ghana na kudhoofisha uwezo wa kilimo na kuhatarisha afya ya umma. Mito imechafuliwa na kemikali zenye sumu huku wenyeji na wageni wakihusika katika biashara hiyo ya uchimbaji haramu wa dhahabu inayojulikana zaidi nchini humo kama “galamsey”.
Rais Nana Akufo-Addo aliahidi kukomesha vitendo hivyo baada ya kuingia madarakani mwaka 2017. Lakini licha ya mipango kadhaa ya serikali, bado utekelezaji wake ni dhaifu. Wanaharakati katika jamii zilizoathiriwa wanaendelea kutoa miito ya kuchukuliwa hatua za haraka.
Athari za “galamsey” kwa akina mama wajawazito
Daktari wa Ghana Prof. Paul Poku Sampene Ossei anapigia upatu hatua ya kupiga marufuku kabisa aina zote za uchimbaji wa madini kwa viwango vya chini. Utafiti uliofanywa na timu yake unaonyesha uharibifu unaozidi kuongezeka kutokana na uchimbaji madini haramu.
Katika wilaya ya Bibiani-Anhwiaso-Bekwai, ambako ni kitovu cha uchimbaji madini haramu magharibi mwa Ghana, timu yake iligundua uwepo kwa chembechembe za madini ya chuma kwenye mfuko wa uzazi wa wanawake wajawazito, ambazo zilisababisha kasoro kwa watoto wanaozaliwa.
Soma pia: Jimbo lenye utajiri wa madini DRC lasimamisha uchimbaji
Matokeo hayo yanathibitisha tafiti zingine zilizochapishwa kuhusu uhusiano kati ya uchimbaji madini haramu na kasoro za kimaumbile zinazoshuhudiwa kwa watoto wanaozaliwa.
Erastus Asare Donkor, mwandishi wa habari za uchunguzi na mazingira ameiambia DW kuwa karibu mito yote mikubwa kote nchini Ghana imechafuliwa.
Wachimbaji haramu ni akina nani?
Donkor ambaye ameripoti kwa kina kuhusu vitendo vya “galamsey” nchini Ghana, anasema vikosi kazi vya serikali vilivyoundwa kwa miaka mingi kupambana na uchimbaji madini haramu vimethibitisha kushindwa kwao kwa sababu kwa kiasi kikubwa baadhi ya walio madarakani wanahusika pia na vitendo hivyo.
“Kuhusika kwa watendaji wa kisiasa, maafisa wa serikali na watu mashuhuri ndio sababu kuu inayopelekea vitendo hivi kutokomeshwa. Uchimbaji haramu wa madini una athari kubwa kwa maisha, hali ya hewa, afya na kilimo ambavyo kwa ujumla huwa na athari pia kuhusu viwango vya umaskini hasa kwa jamii za vijijini.”
Soma pia: UN: Uchimbaji rasilimali za dunia kuongezeka asilimia 60
Mwandishi huyo wa habari wa Ghana ameeleza kuwa alishuhudia wanasiasa na maafisa wa serikali wakijihusisha na shughuli haramu za uchimbaji madini ndani ya hifadhi za misitu. Wanajeshi walipotumwa maeneo hayo wamekuwa wakizuiwa kutimiza wajibu wao na maafisa wa serikali.
Hatua gani zichukuliwe kukomesha vitendo hivyo?
Wataalamu pia wanasema kuwa uchimbaji madini haramu umeenea pia nchini Afrika Kusini ambako raia wa kigeni, wanasiasa na watu mashuhuri wamekuwa wakijihusisha na shughuli hizo.
Soma pia:Senegal yasimamisha shughuli za uchimbaji madini karibu na mpaka na Mali
Enoch Randy Aikins, mchambuzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Usalama (ISS), ameiambia DW kuwa anaamini njia pekee ya kukomesha vitendo hivyo ni kuwachukulia hatua watu wa ngazi za juu wanaohusika. Anasema ni lazima hatua hiyo ianzie kwa watu walioko serikalini na wenye ushawishi na ndiyo wananchi watafahamu kuwa serikali imeamua kulikemea ipasavyo suala hilo na ndipo watazingatia hatua zozote zinazochukuliwa.
Uchimbaji haramu wa madini ni tatizo ambalo limeyakumba mataifa mengi ya Afrika. Ripoti ya Interpol inaonyesha kuwa wachimbaji wadogo mara nyingi ni watu walio katika mazingira magumu na wanaotumiwa na wafanyabiashara wakubwa, vikundi vya uhalifu, wanasiasa pamoja na makundi yenye silaha katika maeneo yenye migogoro katika nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.