Akizungumzia shambulizi hilo rais Zelenskiy amesema tukio hilo ni mfululizo wa mashambulizi ya Urusi, akisisitiza haja ya msaada muhimu na wakutosha kutoka kwa washirika wake wa Magharibi akitataja shambulizi la Iran kuelekea Israeli kama mfano wa ushiriakiano wa washirika wanaofanya kazi pamoja.
“Kwa muda mrefu Ukraine imekuwa ikiwaambia majirani zake wote, washirika wake wote wakuu, kwamba tunahitaji kushirikiana, tunahitaji kwa pamoja kuziangusha ndege zisizo na rubani za Shahed na makombora, haswa katika maeneo ya karibu na nchi za NATO.”
“Hili linawezekana kabisa. Kila wakati katika Mashariki ya Kati, wakati wa mashambulizi ya kikatili ya Iran, tunaona muungano wa kimataifa ukifanya kazi pamoja.”
Soma pia: Urusi yauteka mji muhimu wa mashariki mwa Ukraine
Gavana wa mkoa wa Kharkiv Oleh Syniehubov amesema kuwa bomu hilo lililenga kati ya ghorofa ya tatu na ya nne ya jengo hilo la makaazi katika wilaya ya Saltivka, na kwamba operesheni ya uokoaji inaendelea wakiohofia kuwa baadhi ya watu wangali wamefunikwa kwenye vifusi.
Gavana wa mkoa wa Kharkiv Oleh Syniehubov amesema,”Hili ni eneo la makazi, hii si sehemu yenye umuhimu wa kijeshi na wala haina miundombin hiyo.”
Meya wa Kharkiv Ihor Terekhov amesema watu 10 wamejeruhiwa akiwemo mtoto wa miaka mitatu. Hata hivyo Urusi inakanusha kuwalenga raia, lakini imekuwa mara kwa mara ikishambulia miji na maeneo karibu na mstari wa mbele wa vita.
Ukraine yajibu kwa makombora
Kujibu mashambulizi Jeshi la Ukraine limesema limetumia makombora kulenga Kituo cha rada cha Urusi ili kupunguza uwezo wa Moscow “kugundua, kufuatilia na kukatiza shabaha za makombora yake”.
Hata hivyo jeshi la Ukraine halikutoa maelezo zaidi kuhusu ni lini shambulizi hilo lilifanywa au kutaja eneo la kituo cha rada kilichoshambuliwa katika taarifa yake.
Mamlaka ya Urusi mapema leo Alhamisi imeripoti kwamba watu watatu wameuwawa na wengine 24 kujeruhiwa katika shambulizi la guruneti la Ukraine katika eneo la mpaka wa la Belgorod.
Kwa mujibu wa mkuu wa mamlaka ya afya ya kikanda, Andrei Ikonnikov, miongoni mwa waliojeruhiwa katika shambulizi hilo ni watoto wawili.