Kim atishia kuisambaratisha Korea Kusini kwa nyuklia – DW – 04.10.2024

Haya ni kulingana na taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari nchini humo. Hii ni baada ya kiongozi wa Korea Kusini kuuonya utawala wa Kim kwamba utaangushwa iwapo atathubutu kutumia zana za nyuklia. Kim ametoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara katika kitengo cha operesheni maalum cha jeshi.

“Iwapo Korea Kusini itajaribu kutumia jeshi kuingilia uhuru wa Korea Kaskazini, hali kama hiyo ikitokea, Seoul na Jamhuri ya Korea zitaangamia,” alisema Kim.

Uhasama kutangazwa rasmi

Taarifa ya Kim ni jawabu kwa hotuba ya Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol,katika siku ya jeshi la taifa lake hapo Jumanne.

Majibizano kama hayo baina ya mataifa hayo mawili si jambo geni ila yanafanyika wakati ambapo kuna uhasama mkubwa baina ya mataifa hayo kutokana na hatua ya Korea Kaskazini hivi majuzi kufichua kwamba ina kinu cha nyuklia na hatua yake ya kuendelea kufanyia majaribio makombora.

Südkorea - US Militärübung Ulchi Freedom Shield
Marekani na Korea Kusini wakifanya mazoezi ya pamoja ya kijeshiPicha: Yonhap/picture alliance

Wachambuzi wanasema wiki ijayo, bunge la Korea Kaskazini linatarajiwa kupitisha na kutangaza rasmi uhasama baina ya mataifa hayo mawili katika Rasi ya Korea, hatua itakayokuwa kiashiria rasmi cha kukataa maridhiano na Korea Kusini na kuweka mipaka mipya ya mataifa hayo.

Tangu mwaka 2022, Kim mara kwa mara amekuwa akitishia kutumia silaha za nyuklia ila wachambuzi wanasema hakuna uwezekano wake wa kutumia silaha hizo kwa kuwa jeshi la Korea Kaskazini ni dogo likilinganishwa na jeshi la Marekani na wandani wake.

Mnamo mwezi Julai, Korea Kusini na Marekani zilisaini mwongozo wa ulinzi utakaozijumuisha silaha za Korea Kusini na zile za nyuklia za Marekani, kwa ajili ya kukabiliana vyema na Korea Kaskazini na mpango wake wa nyuklia unaozidi kuimarika. Korea Kusini haina zana za nyuklia.

Maputo ya taka yaanza tena kurushwa

Uhasama baina ya mataifa hayo ya Korea uko katika kiwango kibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka kadhaa, huku uchokozi wa Kim wa majaribio ya makombora na mazoezi ya kijeshi ya Korea Kusini kwa ushirikiano na Marekani, vikionekana kama vitendo vya kulipiziana kisasi.

Nordkoreas Ballonprovokation
Picha: Yonhap/picture alliance

Hakuna mawasiliano kati ya Korea hizo mbili tangu mwaka 2019.

Jeshi la Korea Kusini Ijumaa iliyopita lilisema kwamba Korea kaskazini imeanza tena kurusha maputo yaliyobeba takataka kuelekea nchini humo.

Pyongyang ilikuwa ikirusha maelfu ya maputo hayo tangu mwishoni mwa mwezi Mei jambo lililoipelekea Korea Kusini kuanza tena kutangaza propaganda dhidi ya utawala wa Korea Kaskazini katika maeneo ya mpakani.

Chanzo: APE

Related Posts