Shambulizi la bomu lililotegwa ndani ya gari limemuua afisa huyo wa usalama wa kinu kinachokaliwa na Urusi leo Ijumaa. Haya yanajiri huku Kremlin ikionya mamlaka ya Ukraine kwamba “inacheza na moto”.
Kyiv imekuwa ikiwalenga watu kadhaa mashuhuri inaowataja kama “washirika” na “wasaliti” kwa kufanya kazi na vikosi vya Urusi tangu Moscow ilipoivamia Februari 2022.
Soma pia: Ukraine yashambulia bohari ya mafuta ya Urusi
Idara ya kijasusi ya kijeshi ya Ukraine, GUR, imesema mlipuko wa bomu lililotegwa ndani ya gari umemuua Andriy Korotky, ambaye ilimtaja kama “mkuu wa usalama” katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia.
Lakini idara hiyo imemtaja Korotky kama “mhalifu wa kivita” ambaye alishirikiana kwa hiari na wavamizi wa Urusi, na kwamba alikuwa akitoa maelezo juu ya wafanyikazi wa kiwanda cha wanaopinga Ukraine na alishiriki katika ukandamizaji wa wafanyikazi wa mtambo huo.
Aidha walichapisha video ya ubora wa chini inayoonyesha gari aina ya SUV nyeupe ikiendeshwa polepole kabla ya kulipuka, na kuharibika vibaya na kutapakaza vipande vya gari hilo la moshi.
Mamlaka yapendekeza adhabu kali
Mamlaka zinazoungwa mkono na Urusi katika kituo hicho cha nyuklia zililaani shambulizi hilo na kusema Korotky aliuawa katika shambulio la kigaidi lililofanywa na serikali ya Kyiv. Mkurugenzi wa mmea huo, Yury Chernichuk, aliyeteuliwa na Urusi amesema lazima adhabu kali zichukuliwe.
Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema wamewasiliana na wakala wa shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nyuklia IAEA:
“Kyiv inaendelea kucheza na moto, na katika mawasiliano yetu na IAEA, tumeliweka wazi tukio hili kwa wawakilishi wa IAEA. Kwa sasa, mawasiliano na Grossi hayako katika mipango ya Putin.”
Hata hivyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine Heorhiy Tykhyi amekanusha madai kwamba Ukraine inafanya mashambilizi katika au karibu na mmea wa nyuklia Zaporizhzhia.
Huku haya yakijiri Urusi imemuhukumu mwanamume mmoja mkaazi wa Crimea kifungo cha miaka 14 katika jela ya adhabu kali kwa makosa ya uhaini baada ya kumtuhumu kusaidia jeshi la Ukraine.
Vyombo vya habari vya Urusi vimeripoti kuwa idara ya usalama ya Urusi, FSB imemshutumu Igor Kopyl mwenye umri wa miaka 47 kwa kusaidia wanajeshi wa Kyiv kuandaa kile ilichokiita shambulio la “kigaidi”.
Mara kwa mara Moscow imekuwa ikiwatia hatiani watu ambao inawatuhumu ima kufanya kazi na Ukraine au kukosoa mashambulizi yake kijeshi.