Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Msanii maarufu wa Bongo Fleva nchini Tanzania, Faustina Mfinanga, anayefahamika zaidi kwa jina la Nandy, ametajwa kuwania tuzo ya Msanii Bora wa Kike (Best Female Artist) kwenye tuzo za African Entertainment Awards USA (AEAUSA).
Katika kipengele hiki, Nandy atachuana na mastaa wakubwa wa muziki barani Afrika kama Yemi Alade, Tiwa Savage, Simi, Ayra Starr, Tems, Makhadzi, Tyla, Aya Nakamura, na Niniola.
Kwa upande mwingine, Diamond Platnumz—msanii maarufu wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul—anachuana na mastaa kutoka Nigeria na kwingineko Afrika katika kipengele cha Msanii wa Mwaka (Artist of the Year). Diamond atakutana na majina makubwa kama Burna Boy, Davido, Wizkid, Ayra Starr, Rema, Asake, Adekunle Gold, na Tyla kutoka Afrika Kusini.
Tuzo hizi za AEAUSA zinatarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu, ambapo wasanii mbalimbali wa Kiafrika watapambanishwa katika vipengele mbalimbali. Orodha hii ya wasanii wanaowania tuzo imetolewa rasmi na inatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi wa muziki barani Afrika na duniani kote.
Mbali na kipengele cha Msanii wa Mwaka, Diamond Platnumz pia ametajwa katika vipengele vingine, hivyo kumuweka katika nafasi kubwa ya kushinda zaidi ya tuzo moja mwaka huu. AEAUSA ni tuzo zinazotambua na kuenzi mchango wa wasanii wa Kiafrika kwenye burudani na utamaduni kwa ujumla.
Mashabiki sasa wanatazamia kuona nani ataibuka na ushindi mkubwa katika tuzo hizo zinazokuja.